10 – Kuyafanya makaburi kuwa ni sikukuu. Kwa maana ya kwamba mtu akayatembelea katika nyakati maalum au misimu maarufu kwa ajili ya kufanya ´ibaadah karibu nayo au kwa sababu nyingine. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msilifanye kaburi langu kuwa sikukuu na wala msifanye nyumba zenu kuwa makaburi. Popote mlipo niswalieni, kwani hakika swalah zenu zinanifikia.”

Ameipokea Abu Daawuud (1/319) na Ahmad (2/367) kwa cheni ya wapokezi nzuri. Hadiyth iko katika sharti za Muslim. Ni Swahiyh kutokana na njia na nyenginezo zinazoiunga mkono. Ina njia nyingine kutoka kwa Abu Hurayrah kwa Abu Nu´aym katika “al-Hilyah” (6/283). Kuna nyingine yenye kuiunga mkono kwa cheni ya wapokezi yenye nguvu kupitia kwa Suhayl ambaye amesema:

“al-Hasan bin al-Hasan bin ´Aliy bin Abiy Twaalib aliniona karibu na kaburi. Akaniita naye yupo ndani ya nyumba ya Faatwimah anakula chakula cha jioni ambapo akasema: ”Njoo ule chakula.” Nikasema: ”Sihitaji.” Akasema: ”Kwa nini nimekuona karibu na kaburi?” Nikasema: ”Nimemsalimia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”
Akasema: ”Ukiingia msikitini, msalimie!” Kisha akasema: ”Hakika Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msilifanye kaburi langu kuwa sikukuu wala msizifanye nyumba zenu kuwa makaburi. Niswalieni, kwani hakika swalah zenu zinanifikia popote mlipo. Allaah awalaani mayahudi wameyafanya makaburi ya Manabii wao kuwa misikiti.”
Ninyi na walioko Andalusia ni sawasawa.”

Ameipokea Sa’iyd bin Mansuwr, kama ilivyo katika “al-Iqtidhwaa´” ya Ibn Taymiyyah. Vilevile ipo kwa Shaykh Ismaa’iyl bin Ishaaq al-Qaadhwiy katika “Fadhwl-us-Swalaah ´ala an-Nabiyy (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)” (na. 30), isipokuwa bila ya maneno: “Allaah awalaani mayahudi…” Vilevile amepokewa na Ibn Abiy Shaybah (4/140) kwa kutaja tu kwamba yametoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Aidha kuna nyingine inayoiunga mkono kwa maana hii kutoka kwa ´Aliy bin al-Husayn, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ameipokea Ismaa’iyl al-Qaadhwiy (na. 20) na wengineo. Tazama “Tahdhiyr-us-Saajid”, uk. 98–99.

Hadiyth hii ni dalili ya uharamu wa kuyafanya makaburi ya Manabii na waja wema kuwa ni sikukuu. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema katika “al-Iqtidhwaa´”, uk. 155–156:

“Dalili ya hilo ni kuwa kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndilo kaburi bora zaidi duniani, lakini akakataza kulifanya kuwa sikukuu. Basi makaburi mengine ni zaidi ya kukatazwa, pasi na kujali nani awe. Kisha akalifungamanisha na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”.. wala msifanye nyumba zenu kuwa makaburi.”

Kwa maana ya kwamba msiache kuswali ndani ya nyumba zenu, kuomba du´aa na kusoma Qur-aan zikawa mithili ya makaburi. Hivyo basi akaamrisha kujitahidi kufanya ´ibaadah ndani ya nyumba na akakataza kujitahidi kufanya ´ibaadah karibu na makaburi, kinyume na wanavyofanya washirikina miongoni mwa wakristo na wanaowashabihisha nao.”

Akaendelea kusema:

”Huyu ni bora ya wanafunzi wa Maswahabah miongoni mwa watu wa Nyumba yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kwa maana ´Aliy bin al-Husayn (Radhiya Allaahu ´anhum). Alimkataza yule mtu kuomba du´aa maalum kwenye kaburi lake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akajengea hoja kwa Hadiyth aliyosikia kutoka kwa baba yake al-Husayn kutoka kwa babu yake ´Aliy.”

Naye ndiye anayejua zaidi maana yake kuliko wengine. Hivyo ikabainika kuwa lengo lake ni kuwa mtu akusudie kaburi kwa ajili ya kumtolea salamu na mfano wake bila ya kuingia msikitini. Aidha akaona kuwa jambo hilo linakuwa kama ni du´aa na mfano wa kufanya mahali hapo kuwa kama sikukuu. Vivyo hivyo binamu yake Hasan bin Hasan, ambaye ni Shaykh wa watu wa nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), alichukia kufanya kaburi hilo kuwa kama sikukuu. Tazama jinsi Sunnah hii inavyotoka kwa watu wa Madiynah na watu wa nyumbani mwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), waliokuwa karibu naye kwa nasaba na kwa makazi, kwani wao walikuwa na haja zaidi ya kuinusuru Sunnah kuliko wengine na hivyo walikuwa wenye kushikamana nayo zaidi.

Neno ”sikukuu” likiwa jina la mahali, basi maana yake ni mahali panapokusudiwa kukutanika kwa ajili ya ´ibaadah au mengineyo, kama vile msikiti Mtukufu, Minaa, Muzdalifah na ´Arafah Allaah amezifanya kuwa ni sikukuu na mahali pa marejeo kwa watu ambapo wanakusanyika humo kwa ajili ya kuomba du´aa, Dhikr na tararibu za ´ibaadah ya hajj. Washirikina walikuwa na maeneo wanayokusanyika humo. Hata hivyo Uislamu ulipokuja basi Allaah akafuta hayo yote. Aina hii ya maeneo yanajumuisha makaburi ya Manabii na watu wema.”

Kisha Shaykh akasema, uk. 175–181:

”Kwa ajili hiyo Imaam Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) na wanazuoni wengine wa Madiynah walichukia mtu wa Madiynah kila anapoingia msikitini aende moja kwa moja kutoa salamu kwenye kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake wawili.”

Akasema:

”Hilo litafanyika tu iwapo mtu huyo atakuwa amewasili kutoka safarini au anakusudia kusafiri au hali mfano wa hiyo. Wengine wameruhusu kutoa salamu tu akapoingia msikitini kwa ajili ya swalah au mfano wake. Ama kumkusudia kila wakati kwa ajili ya salamu na du´aa basi sijui yeyote aliyeliruhusu hilo, kwa sababu kufanya hivo ni aina ya kulifanya kaburi kuwa ni sikukuu. Pamoja na kwamba imewekwa katika Shari´ah wetu tunapoingia msikitini tuseme:

”Amani, rehema na baraza za Allaah ziwe juu yako, ee Mtume.”[1]

kama tunavyosema mwishoni mwa swalah zetu.”

Akaendelea kusema:

”Ndipo Maalik na wengine wakaogopa kuwa kurudia jambo hilo mara kwa mara pembeni ya kaburi ni aina ya kulifanya kuwa sikukuu. Isitoshe kitendo hicho ni Bid´ah, kwa sababu Muhaajiruun na Answaar katika zama  za Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan na ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhum) walikuwa wakija msikitini kila siku wakijua (Radhiya Allaahu ‘anhum) yale ambayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) anayachukia na yale aliyowakataza kuyafanya. Aidha wanamtolea salamu pale wanapoingia na kutoka msikitini na katika Tashahhud, kama walivyokuwa wakimtolea salamu katika uhai wake. Ni uzuri uliyoje wa yale aliyosema Maalik:

”Hautofaulu mwisho wa ummah huu isipokuwa kwa yale yaliyowafanya kufaulu wa mwanzo wao.”[2]

Lakini kila ummah unavyozidi kudhoofika katika kushikamana na maagano ya Manabii wao na imani yao kupungua ndipo wakaziba mapengo hayo kwa kuzusha Bid´ah na shirki na mengineyo. Kwa sababu hiyo ummah ukachukia kubusu na kugusa kaburi.
Wakaweka ujenzi juu yake na wakawazuia watu kuswali mbele yake.”

Akaendelea kusema:

”Tumetaja kutoka kwa Ahmad na wengine kuwa aliagiza kuwa anayemsalimia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake wawili, kisha akataka kuomba du´aa, basi ageuke kuelekea Qiblah. Hayo yametajwa na wanazuoni waliotangulia, kama Maalik na wengine, na waliokuja baadaye, kama Abul-Wafaa´ bin ´Aqiyl, Abul-Faraj bin al-Jawziy. Sijui kutoka kwa Swahabah yeyote, mwanafunzi wa Maswahabah wala imamu anayetambulika kuwa aliona ni jambo linalopendekezwa kukusudia kaburi lolote kwa ajili ya kuomba du´aa pale. Wala hakuna yeyote aliyepokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), si kutoka kwa Maswahabah wake wala kutoka kwa imamu yeyote anayefahamika, chochote kinachoonyesha fadhilah za kuomba du´aa kando ya makaburi. Watu wameandika vitabu kuhusu du´aa, nyakati zake, mahala pake na wakataja masimulizi. Lakini hakuna hata mmoja wao aliyesema lolote kuhusu fadhilah za du´aa pembeni ya kaburi, hata neno moja, kwa mujibu wa ninavyofahamu. Basi vipi jambo kama hilo liwe ni bora na lenye kuitikiwa zaidi – hali Salaf hawakulijua, walilikataa na hawakuliamrisha?”

Akaendelea kusema:

”Kukusudia kuwa du´aa pembeni ya kaburi inajibiwa zaidi na ina fadhilah zaidi kumepelekea watu waanze kwenda huko kwa makusudi na kukusanyika kwa ajili hiyo hata katika nyakati maalum. Hili ndilo jambo alilolikataza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale aliposema:

“Msilifanye kaburi langu kuwa sikukuu.”

Akaendelea kusema:

”Hata baadhi ya makaburi hukusudiwa kila mwaka kwa siku maalum na watu husafiri kuyafikia mara katika Muharram, Rajab, Sha´baan, Dhul-Hijjah na kadhalika. Mengine hukusudiwa siku ya ´Aashuraa´, siku ya ´Arafah, katikati ya Sha´baan na mengine wakati mwingine. Mpaka kaburi linakuwa na siku yake maalum ya mwaka inayokusudiwa na watu hukusanyika mahali hapo – kama ´Arafah, Muzdalifah na Minaa zinavyokusudiwa katika siku zake maalum, au kama sehemu ya kuswalia swalah ya ´iyd. Bali watu wengine hujali zaidi mikusanyiko hiyo ya kaburini kuliko masuala mengine ya kidini na kidunia.
Baadhi ya makaburi husafiriwa kutoka miji mbalimbali kwa ajili ya kwenda kuomba du´aa au ´ibaadah pale, kama vile watu wanavyoikusudia Nyumba Takatifu ya Allaah kwa ajili hiyo. Sijui makinzano yoyote baina ya waislamu kuhusu uharamu wa safari hii.”

Akaendelea kusema:

”Mengine hukusudiwa siku maalum ya juma. Kwa ujumla yale yanayofanywa katika makaburi haya ndiyo yenyewe aliyokataza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale aliposema:

“Msilifanye kaburi langu kuwa sikukuu.”

Kwa sababu kurudia kwenda sehemu maalum katika muda maalum kwa mwaka, mwezi au wiki, hilo ndilo lenyewe maana ya sikukuu. Kisha akakataza dogo na kubwa la hilo. Haya ndiyo yaliyopokelewa kutoka kwa Ahmad kuwa aliyakaripia. Watu wamezidisha mno katika jambo hili na wakapitiliza.”

Akataja yaliyokuwa yakifanyika katika kaburi la al-Husayn. Kisha Shaykh akaendelea kusema:

”Haya pia yanafanyika huko Misri kwenye kaburi la Nafiysah na mengineyo. Aidha yale yanayofanyika huko ´Iraaq katika kaburi linalodaiwa kuwa ni la ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh), kaburi la al-Husayn, Hudzayfah bin al-Yamaan n.k. Vilevile yanayofanywa katika kaburi la Abu Yaziyd al-Bustwaamiy hadi kwenye makaburi mengi katika maeneo mengi ya Kiislamu yasiyohesabika.”

Akaendelea kusema:

“Kuzoea kwenda katika makaburi haya kwa wakati maalum na mikusanyiko mikubwa katika wakati maalum ndilo khaswa kufanya kaburi kuwa sikukuu, kama tulivyotangulia kusema. Sijui baina ya wanazuoni wa Kiislamu makinzano yoyote juu ya hili. Wala mtu asije akadanganyika na wingi wa ada potofu, kwa kuwa hiyo ni miongoni mwa kujifananisha na watu wa vitabu viwili ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametueleza kuwa jambo hilo litatokea katika ummah huu. Msingi wa yote haya ni kuamini kuwa kufanya du´aa kaburini kuna fadhilah. Vinginevyo kama hili halingekuwa limejengeka ndani ya nyoyo, basi mambo haya yote yangekuwa yamefutika. Ikiwa kukusudia makaburi kunaleta madhara haya yote, basi ni haramu kama kuswali pale, bali zaidi ya hivyo. Aidha jambo hilo limekuwa ni mtihani kwa watu, kufungua mlango wa shirki na huku kufungwa mlango wa imani.”

Miongoni mwa mambo yanayoingia katika hayo nafasi ya mbele kabisa ni kile kinachoonekana leo hii al-Madiynah al-Munawwarah. Watu wanapokusudia kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya kila swalah ya faradhi kwa ajili ya kumsalimia na kuomba du´aa pembeni ya kaburi au kupitia yeye na wanapaza sauti zao hapo kaburini mpaka msikiti unazizima kwa kelele zao, khaswa katika msimu wa Hajj kiasi kwamba mtu anaweza kufikiri kuwa hilo ni sehemu ya Sunnah ya swalah. Bali wanalishikia zaidi kuliko kushikilia Sunnah. Haya yote yanatokea mbele ya macho na masikio ya watawala na hakuna yeyote katika wao anayekataza. Hakika sisi ni wa Allaah na hakika Kwake Yeye ndio tutarejea. Ninasikitika kwa ugeni wa dini na watu wa dini. Hali hii ni katika msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao ulipaswa kuwa mbali zaidi na kila kinachokwenda kinyume na Shari´ah yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya msikiti Mtakatifu.

Haya licha ya kwamba tayari kumetangulia katika maneno ya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah kuwa baadhi ya wanazuoni wametoa ruhusa ya kuja katika kaburi tukufu kwa ajili ya kutoa salamu ikiwa mtu ataingia msikitini kwa ajili ya swalah au mfano wake. Ni kama kwamba hilo limewekewa kikomo cha kutofanya sana na kurudiarudia, kwa dalili ya maneno yake baada ya hayo:

”Ama kulikusudia daima kwa ajili ya swalah na salamu, basi simjui yeyote aliyetoa ruhusa hiyo.”

Ruhusa hii aliyoitaja Shaykh kutoka kwa baadhi ya wanazuoni ndicho kilichopokelewa na tunategemea juu yake kwa sharti ya kikomo kilichotajwa. Kwa hiyo inajuzu kwa aliyeko mjini Madiynah katika baadhi ya nyakati kuja kwenye kaburi tukufu kwa ajili ya kumtolea salamu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kwa sababu kufanya hivo sio kulifanya sikukuu, kama inavyodhihiri.

Kumtolea salamu yeye na marafiki zake wawili ni jambo lililowekwa katika Shari´ah kutokana na dalili zilizoenea. Basi si sahihi kupinga yaliyowekwa katika Shari´ah kwa sababu ya katazo lake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya kulifanya kaburi lake kuwa sikukuu, kwa kuwa kuna uwezekano wa kuyaoanisha maneno mawili hayo kwa kuzingatia sharti tulilotaja. Haiwezi kusemwa kuwa hatujui kuwa mmoja katika Salaf alikuwa akifanya hivyo, kwa sababu kutokujua kitu si dalili ya kutokuwepo kwake, kama wanavyosema wanazuoni. Basi katika hali kama hii, inatosha kuthibitisha uwekwaji wa Shari´ah wa jambo hilo kutokana na dalili za jumla muda wa kuwa hakuna kinachokinzana nazo katika tulichonacho. Licha ya kwamba Shaykh-ul-Islaam ametaja katika ”al-Qaa’idah al-Jaliylah”, uk. 80, chapa ya al-Manaar, kutoka kwa Naafiy´ kwamba amessema:

”Ibn ´Umar alikuwa akilitolea salamu kaburi. Nimemuona mara mia au zaidi akija kwenye kaburi na akisema:

السلام على النبي صلى الله عليه وسلم، السلام على أبي بكر، السلام على أبي

”Amani iwe juu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), amani iwe juu ya Abu Bakr, amani iwe juu ya baba yangu.”,

kisha anaondoka zake. Dhahiri ya hilo ni kuwa alikuwa akifanya hivyo akiwa katika hali ya ukazi na si safarini, kwa sababu maneno yake ”… mara mia… ” kunafanya iwe mbali kwamba amehesabu hilo akiwa safarini.

[1] Sikuona namna hii katika chochote cha Hadiyth zilizotaja katika adabu za kuingia msikitini na kutoka humo. Ameichukua kutoka katika maana ya jumla ya maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Ikiwa mmoja wenu ataingia msikitini, basi na amsalimie Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)…. ”

Hadiyth hii ameipokea Abu ‘Awaanah katika ”as­-Swahiyh” yake (1/414) na Abu Daawuud katika ”as-Sunan” yake (na. 465). Hili ni jambo lisilofichika umbali wake, khaswa ukizingatiwa kuwa maneno yenyewe yamekuja katika Hadiyth ya Faatwimah (Radhiya Allaahu ´anhaa) kwa tamlo lisemalo:

السلام على رسول الله، اللهم صل على محمد وعلى آل محمد

”Amani iwe juu ya Mtume wa Allaah. Ee Allaah! Msifu Muhammad na jamaa zake Muhammad.”

Ameipokea al-Qaadhwiy Ismaa´iyl (82–84) na wengine. Tazama ”Nuzul-ul-Abarar” (72) na ”al-Kalim at-Twayyib” (na. 63 – kwa ukaguzi wangu wa chapa ya al-Maktabah al-Islaamiy).

[2] Tazama ”al-Qaa´idah al-Jaliylah fiyt-Tawassul wal-Wasiylah”, uk. 53-62.

  • Muhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 280-285
  • Imechapishwa: 12/08/2026