9 – Kujenga misikiti juu ya makaburi. Kuna Hadiyth kadhaa juu ya hilo:

1 – ´Aaishah na ´Abdullaah bin ´Abbaas wameeleza wote kwa pamoja:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa katika hali ya kukata roho alianza kuweka kishuka chake usoni mwake. Kila alipoona uzito alikiondoa usoni mwake na akasema hali hiyo ikiendelea:

”Laana ya Allaah iwe juu ya mayahudi na manaswara. Wameyafanya makaburi ya Manabii wao kuwa ni misikiti.” Anawahadharisha [mfano wa] waliyoyafanya.”

Ameipokea al-Bukhaariy (1/422, 6/386, 8/116), Muslim (2/67), an-Nasaa’iy (1/115), ad-Daarimiy (1/326), al-Bayhaqiy (4/80) na Ahmad (1/218, 6/34, 229, 275). Ziada hiyo ipo kwa Muslim, ad-Daarimiy na wengineo.

2 – ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Laana ya Allaah iwe juu ya mayahudi na manaswara. Wameyafanya makaburi ya Manabii wao kuwa ni misikiti.” Anatahadharisha [mfano wa] waliyoyafanya.” ´Aaishah akasema: ”Lau si hivyo, kaburi lake kingedhihirishwa wazi, lakini alikhofia lisifanywe msikiti.”

Ameipokea al-Bukhaariy (3/156, 198, 8/114), Abu ‘Awaanah (2/399) na Ahmad (6/80, 121, 255). Vilevile kuna njia nyingine kwa Ahmad (6/146, 252).

3 – Abu Hurayrah ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah awaue mayahudi… ”

Imekuja katika upokezi mwingine:

”Laana ya Allaah iwe juu ya mayahudi na manaswara. Wameyafanya makaburi ya Manabii wao kuwa misikiti.”

Ameipokea al-Bukhaariy (1/422), Muslim na Abu ‘Awaanah (2/400), Abu Daawuud (2/71), al-Bayhaqiy (4/80) na Ahmad (2/284, 366, 396, 453, 518). Upokezi wa pili uko kwa Muslim na Abu ‘Awaanah kupitia njia nyingine ya Abu Hurayrah.

4 – Kutoka kwake tena (Radhiya Allaahu ´anh) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Ee Allaah, usifanye kaburi langu kuwa sanamu linaloabudiwa. Allaah awalaani watu walioyafanya makaburi ya Manabii wao kuwa misikiti.”

Ameipokea Ahmad (2/246), Ibn Sa’d katika ”at-Twabaqaat” (2/362), Abu Nu’aym katika “al-Hilyah” (7/317) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.”

Kuhusu maneno ya al-Haythamiy katika “Majma’-uz-Zawaa’id” (2/23) aliposema:

“Amepokea Abu Ya’laa na ndani yake yupo Ishaaq bin Abiy Israa’iyl ambaye ana maneno kuhusu msimamo wake juu ya Qur-aan. Hata hivyo wengine ni wenye kuaminika”, basi kuna mambo kadhaa:

1 – Alimtaja tu Abu Ya’laa kana kwamba haipo kwa Ahmad, ilihali imo kama tulivyotaja.

2 – Ishaaq ni mwenye kuaminika. Kuchukua kwake msimamo wa kusimama juu ya Qur-aan hakumjeruhi, kama ilivyobainishwa katika elimu ya Hadiyth.

3 – Hajaipokea peke yake, kwani pia imo kwa Ahmad kutoka njia nyingine. Kwa hivyo Hadiyth ni Swahiyh bila shaka. Isitoshe kuna nyenginezo ambayo kuna Swahabah anayekosekana katika cheni yake ya wapokezi. Ameipokea Maalik katika “al-Muwattwa´” (1/185–186) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. Pia imesimuliwa kwa njia yenye cheni inayoungana kupitia kwa Abu Sa’iyd al-Khudriy.

5 – Jundub ameeleza ya kwamba amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku tano kabla ya kufariki akisema:

“[Nilikuwa na ndugu na marafiki katika nyinyi]. Hakika mimi najitenga kwa Allaah kuwa na kipenzi wa hali ya juu miongoni mwenu, kwani hakika Allaah (Ta´ala) amenifanya kuwa kipenzi wa hali ya juu kama alivyomfanya Ibraahiym kuwa kipenzi wa hali ya juu. Lau ningemfanya yeyote kutoka katika ummah wangu akawa kipenzi wa hali ya juu, basi ningelimfanya Abu Bakr kuwa kipenzi wa hali ya juu. Tanabahini! Hakika wale waliokuwepo kabla yenu walikuwa wakiyafanya makaburi ya Manabii wao na watu wao wema kuwa misikiti. Tanabahini! Msiyafanye makaburi kuwa misikiti, hakika mimi nakukatazeni jambo hilo.”

Ameipokea Muslim (2/67–68) pekee pasi na wale wengine sita. Ash-Shawkaaniy (2/114) ameihusisha kwa an-Nasaa´iy pia. Pengine anakusudia katika “as-Sunan al-Kubraa” yake. Hakumhusisha kwa ”ad-Dhakhaa-ir” isipokuwa Muslim peke yake. Ameipokea Abu ‘Awaanah katika “al-Musnad” (2/401) na ziada hiyo ni yake.

6 – ´Abdullaah bin Mas’uud amesimulia ya kwamba amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisenma:

“Hakika miongoni mwa watu waovu zaidi ni wale ambao Qiyaamah kitawakuta wakiwa hai na wale wanaofanya makaburi kuwa misikiti.”

Ameipokea Ahmad (na. 3844, 4143, 4144, 4342) kwa cheni mbili ambazo ni nzuri kutoka kwake. Vilevile ameipokea pia Ibn Abiy Shaybah katika “al-Muswannaf” na Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake. Ibn Taymiyyah amesema: “Cheni yake ya wapokezi ni nzuri.” al-Haythamiy alikosea alipodai haimo ndani ya “al-Musnad” ya Ahmad ambapo akasema (2/27): “Ameipokea at-Twabaraaniy katika “al-Kabiyr” na cheni ya wapokezi wake ni nzuri.

7 – ´Aaishah amesema:

”Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa mgonjwa baadhi ya wake zake walitaja kanisa moja lililoko Uhabeshi kwa jina “Maariyah”. Umm Salamah na Umm Habiybah walikwishafika huko na wakataja uzuri wake na picha zilizomo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Hakika hao watu walipokuwa miongoni mwao mtu mwema [akifa] basi wanajenga juu ya kaburi lake msikiti, kisha wakitengeneza ndani yake picha hizo. Hao ndio viumbe waovu zaidi mbele ya Allaah [siku ya Qiyaamah].”

Ameipokea al-Bukhaariy (1/416, 422), Muslim (2/66–67), an-Nasaa’iy (1/115). Vilevile Abu ‘Awaanah (2/400–401), al-Bayhaqiy (4/80), Ahmad (6/51) na Ibn Abiy Shaybah (4/140). Ziada zote mbili ni za al-Bukhaariy na wengineo.

Katika mlango huu zipo Hadiyth nyingine kutoka kwa Maswahabah wengine wengi. Nimezitaja katika kitabu changu: “Tahdhiyr-us-Saajid min Ittikhaadh-il-Qubuur Masaajid”. Zote hizi zinafahamisha waziwazi kwamba kufanya makaburi kuwa misikiti ni haramu, kwa kuwa kuna laana juu ya wanaofanya hivyo. Ndiyo maana al-Faqiyh al-Haytamiy amesema katika “az-Zawaajir” (1/120–121):

“Dhambi kubwa ya tisini na tatu ”Kufanya makaburi kuwa misikiti.”

Kisha akataja baadhi ya Hadiyth zilizotangulia na nyingine ambazo si katika masharti yetu, halafu akasema:

“Kuzingatia haya miongoni mwa madhambi makubwa kumeonekana katika maneno ya baadhi ya ash-Shaafi´iyyah. Huenda wamechukua hilo kutoka katika yale aliyoyataja miongoni mwa Hadiyth hizi ambayo maana yake iko wazi, kwa sababu amemlaani aliyefanya hivyo katika makaburi ya Manabii wake. Aidha akafanya waliotenda hivyo katika makaburi ya waja wake wema kuwa viumbe waovu kabisa mbele ya Allaah siku ya Qiyaamah. Hivyo basi ndani yake kuna onyo kwetu, kama ilivyokuja katika upokezi mwingine:

“Anawahadharisha yale waliyoyafanya.”

Kwa maana ya kwamba anawaonya (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ummah wake kwa kuwatolea mfano huo ili wasifanye kama walivyofanya wale ambapo wakalaaniwa kama wao walivyolaaniwa… Baadhi ya Hanaabilah wamesema: “Makusudio ya mtu kuswali karibu na kaburi kwa kutaka baraka ni upinzani wa wazi kwa Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Aidha ni uzushi wa dini ambao Allaah hakutoa ruhusa yake. Haikukatazwa jambo hilo kwa sababu nyingine, bali ni maafikiano. Hakika miongoni mwa madhambi makubwa na sababu kubwa za shirki ni kuswali karibu na makaburi na kuyafanya misikiti au kuyajengea. Maoni yanayosema kuwa inachukiza yanahusiana na mengine, kwani haiwezekani kudhani kuwa wanazuoni wanaruhusu jambo ambalo limepokewa kwa wingi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alimlaani mwenye kufanya hivo. Kwa hivyo inawajibika kuharakisha kuyabomoa hayo na kubomoa mabanda yaliyojengwa juu ya makaburi, kwani hizo ni khatari zaidi kuliko msikiti wa Dhwiraar kwa sababu zimejengwa juu ya kumuasi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amekataza hilo. Isitoshe ameamrisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kubomoa makaburi yaliyotukuzwa. Inawajibika kuondoa kila taa au mwangaza uliowekwa juu ya kaburi. Haifai kuweka waqf au nadhiri kwa hilo.”

Kufanya hilo lililotajwa katika Hadiyth zilizotangulia linajumuisha mambo kadhaa:

1 – Kuswali kuelekea makaburi kwa kuyakabili.

2 – Kusujudu juu ya makaburi.

3 – Kujenga misikiti juu yake.

Maana ya pili imo wazi ndani ya neno “kuyafanya” na mawili ya mwisho, pamoja na kuwa yameingizwa ndani yake, yamepokelewa kwa andiko maalum katika baadhi ya Hadiyth zilizotangulia. Nimefafanua maneno juu ya hilo na kutaja maneno ya wanazuoni kwa kujengea hoja katika kitabu chetu maalum “Tahdhiyr-us-Saajid min Ittikhaadh-il-Qubuur Masaajid”. Nimetaja ndani yake historia ya kuingizwa kwa kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndani ya msikiti Mtukufu na yaliyomo ndani yake ya kwenda kinyume na Hadiyth zilizotangulia na kwamba kuswali ndani yake si jambo linalochukiza kwa muktadha huo maalum. Kwa hiyo anayependa ufafanuzi wa yote haya, basi na arejee huko.

  • Muhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 275-280
  • Imechapishwa: 12/08/2026