8 – Kuswali karibu na makaburi hata bila kulielekea. Kuna Hadiyth kadhaa juu ya hilo:

1 – Abu Sa‘iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Ardhi yote ni sehemu ya kuswalia isipokuwa makaburi na chooni.”

Wameipokea watunzi wa as-Sunan nne isipokuwa an-Nasaa’iy na wengineo kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kwa sharti za al-Bukhaariy na Muslim, kama alivosema al-Haakim, na adh-Dhahabiy akaafikianan naye. Imekosolewa kwa kuwa ni kuna Swahabah anayekosekana katika cheni ya wapokezi, lakini hilo halidhuru. Hata tukilikubali bado Hadiyth hiyo imepokelewa kwa njia nyingine isiyo na kasoro hiyo na ni kwa mujijbu wa kwa sharti ya Muslim. Nimeelezea kwa urefu kuhusu hilo katika ”ath-Thamar al-Mustatwaab” katika utafiti wa sita wa unaohusu swalah.

2 – Anas ameeleza:

”Hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuswali kati ya makaburi.”

Kumesemwa katika ”al-Majma´” (2/27): ”Ameipokea al-Bazzaar na wanaume wake ni wasimulizi wa Swahiyh.”

Ameipokea Ibn-ul-A´raabiy katika ”al-Mu´jam” yake (1/235), at-Twabaraaniy katika ”al-Awsatw” (1/280) na adh-Dhwiyaa´ al-Maqdisiy katika ”al-Ahaadiyth al-Mukhtaarah” (2/79 na wote wameongeza:

”… juu ya majeneza.”

3 – Ibn ‘Umar ameeleza ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Fanyeni sehemu ya swalah zenu majumbani mwenu na wala msiyafanye kuwa makaburi.”

Ameipokea al-Bukhaariy (1/420), Muslim (2/187) na Ahmad (na. 4511, 4653, 6045).

4 – Abu Hurayrah amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Msiyafanye majumba yenu kuwa makaburi. Kwani hakika shaytwaan hukimbia nyumba inayosomwa ndani yake Suurah al-Baqarah.”

Ameipokea Muslim.

Hili ndilo lenye nguvu zaidi ya kwamba Hadiyth inafahamisha ya kuwa makaburi si mahali pa kuswali khaswa kwa tamkoo la Abu Hurayrah ambalo ndilo lenye uwazi zaidi katika ushahidi. Maneno ya al-Ismaa´iyliy yanajulisha kuwa inachukiza kuswali ndani ya kaburi na siyo katika makaburi, licha y a kwamba inakinzana waziwazi na Hadiyth ya Abu Hurayrah. Basi haifai kufasiri Hadiyth ya Ibn ‘Umar juu ya maana hiyo, kwa sababu kuswali ndani ya kaburi si jambo la kawaida, vipi basi maneno ya Shari´ah yafasiriwe juu ya hilo? Maneno ya Ibn-ut-Tiyn – ambaye ni mmojawapo wa wafafanuzi wa ”Swahiyh-ul-Bukhaariy” – jina lake ni ‘Abdul-Waahid:

”Wafu hawaswali.”

si sahihi, kwa sababu hakuna andiko lolote kutoka katika Shari´ah linalolikanusha hilo. Hayo ni mambo ya ghaibu ambayo haifai kutoa hukumu za yakini juu yake isipokuwa kwa andiko la wazi, jambo ambalo halipo. Kinyume chake kuna yaliyopokelewa yenye kubatilisha maneno hayo ya jumla, nayo ni swalah ya Muusa (´alayhis-Salaam) katika kaburi lakel, kama alivyomuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika safari yake ya usiku. Hayo yamepokelewa na Muslim katika ”as-Swahiyh” yake.

Vilevile swalah ya Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) kwa kumfuata yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika usiku huo, kama ilivyothibiti katika ”as-Swahiyh”. Bali imethibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

”Manabii wako hai ndani ya makaburi yao ambapo wanaswali.”

Ameipokea Ya´laa kwa cheni ya wapokezi nzuri. Nami nimeifanyia ukaguzi katika ”al-Ahaadiyth as-Swahiyhah” (622).

Bali imepokelewa kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yaliyoenea zaidi kuliko hayo tuliyotaja, nayo ni katika Hadiyth ya Abu Hurayrah kuhusu maswali ya Malaika wawili kwa muumini ndani ya kaburi:

”Huambiwa: ”Kaa!” naye ataketi na huwa ameshaonyeshwa jua kana kwamba linakaribia kuzama. Ataambiwa: ”Unaonaje kuhusu huyu aliyekuwa kati yenu? Unasemaje juu yake? Nini unamshuhudia?” Husema: ”Niache mpaka niswali.” Ataambiwa: ”Hakika utaswali.”

Ameipokea Ibn Hibbaan katika ”as-Swahiyh” yake (781), al-Haakim (1/379–380) ambaye amesema: ”Swahiyh kwa sharti za Muslim” na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Lakini ni nzuri tu, kwa sababu ndani yake yumo Muhammad bin ´Amr ambaye Muslim hakumtegemea moja kwa moja bali ameleta Hadiyth zake kwa kuziambatanisha au kuungwa mkono.

Hadiyth hii inasema wazi ya kwamba muumini naye pia anaswali ndani ya kaburi lake. Kwa namna hiyo yanabatilika maneno yanayosema kuwa wafu hawaswali na hivyo yanakuwa na nguvu makusudio ya Hadiyth ya Ibn ´Umar ni kuwa makaburi si mahali pa kuswali – na Allaah (Ta´ala) ndiye mjuzi zaidi.

Hadiyth hii na yale yaliyokuja pamoja nayo vinafahamisha juu ya machukizo ya kuswali makaburini, nayo machukizo hayo ni kwa njia ya uharamu kwa kuwa kuna maneno ya katazo yaliyo wazi katika baadhi yake. Baadhi ya wanazuoni wameenda mbali zaidi na kusema kuwa kuswali makaburini ni batili, kwa sababu katazo linamaanisha kuwa kile kilichokatazwa ni batili. Hayo ndio maoni ya Ibn Hazm na yamechaguliwa pia na Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah na ash-Shawkaaniy katika ”Nayl-ul-Awtwaar” (2/112). Ibn Hazm (4/27-28) amepokea kutoka kwa Imaam Ahmad ya kwamba amesema:

“Anayeswali karibu na makaburi au kulielekea kaburi, basi atarudia daima.”

Kisha chukizo la kuswali katika makaburi linahusisha kila sehemu ya eneo la makaburi, ni mamoja iwe kaburi liko mbele ya mwenye kuswali, nyuma yake, upande wa kulia kwake au upande wa kushoto kwake, kwa sababu katazo ni lenye kuenea. Isitoshe ni jambo lililothibitishwa katika elimu ya misingi ya kuwa muktadha wa jumla hufuatwa kwa jumla yake hadi itokee dalili ya kuuwekea mipaka, jambo ambalo hakuna kitu kilichokuja hapa kinachouwekea mipaka. Baadhi ya wanazuoni wa Hanafiyyah na wengineo wamesema wazi kuhusu haya, kama itakavyokuja. Shayk-hul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema katika ”al-Ikhtiyaaraat al-‘Ilmiyyah”, uk. 25:

“Haisihi kuswali karibu na makaburi wala kuyaelekea. Katazo hilo ni kwa ajili ya kufunga mlango wa shirki. Kundi la baadhi ya wenzetu wameeleza kuwa kaburi moja au mawili hayazuii kuswali, kwa sababu haitwi ”makaburi”, isipokuwa ni kuanzia makaburi matatu na zaidi. Lakini katika maneno ya Ahmad na wafuasi wake wote hakuna tofauti hii. Bali maana ya ujumla ya maneno yao, pamoja na sababu na hoja zao, zinawajibisha kuzuia kuswali hata mbele ya kaburi moja, jambo ambalo ndilo sahihi. Makaburi ni kila eneo lililozikwa mtu, siyo kwamba lazima iwe wingi wa makaburi. Wenzetu wamesema:

“Kila kilichoingia katika jina la makaburi katika sehemu zilizo karibu na makaburi hakuswaliwi ndani yake.”

Hii inaonyesha kuwa marufuku inahusu hata kama ni kaburi la mtu mmoja na sehemu iliyojengeka karibu nalo. al-Aamadiy na wengineo wamesema:

“Haijuzu kuswali ndani ya msikiti ambao Qiblah chake kinaelekea kaburini hadi kuwepo kizuizi kingine baina ya ukuta wa msikiti na makaburi.”

Baadhi yao wamesema: “Hili ni tamko la Imaam Ahmad.”

Katika maneno ya Shaykh (Rahimahu Allaah) kuna maneno ya wazi kuwa sababu ya katazo la kuswali makaburini ni kufunga mlango wa shirki, jambo ambalo ndio moja ya mitazamo miwili ya wanazuoni kuhusu jambo hili. Mtazamo mwingine ni kwamba sababu ni uchafu wa ardhi ya makaburi. Hii ni misimamo miwili ya madhehebu ya Hanafiyyah. Ibn ‘Aabidiyn amekosoa maoni ya pili katika ”al-Haashiyah” (1/352), kwa sababu mabadiliko ya hali ni utakaso katika madhehebu yao. Basi vipi iwe sababu sahihi?

Hakika sisi hatuna shaka ya kwamba maoni ya kwanza ndiyo sahihi. Shaykh-ul-Islaam amebainisha hilo katika vitabu vyake na akatoa hoja zisizopatikana kwa wengine, basi rejea mfano wa kitabu chake ”Iqtidhwaa’-us-Swiraatw al-Mustaqiym”, uk. 152, 193), na hilo ndilo alilolifuata katika ”al-Haaniyah” miongoni mwa vitabu vya Hanafiyyah na at-Twahaawiy akaashiria hilo katika maelezo yake ya chini ya ”Maraaqiy al-Falaah”, aliposema katika maneno ya mwenye kutoa maelezo:

“Inachukiza kuswali kwenye makaburi” (1/208), kwa sababu ni kufanana na mayahudi na manaswara. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Laana ya Allaah iwe juu ya mayahudi na manaswara. Wameyafanya makaburi ya Manabii wao kuwa ni misikiti.”

Ni mamoja iwe kaburi liko juu, nyuma au chini ya kile anachosimamia juu yake. Kinachobaguliwa ni makaburi ya Manabii (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) ambayo haichukizi kuswali karibu nayo kwa hali yoyote, ni mamoja yawe yamefukuliwa au hapana, mradi tu kaburi lisikuwepo upande wa Qiblah, kwa sababu wao wako hai ndani ya makaburi yao.”

Ubaguzi huu ni batili na ni wazi ubatili wake. Vipi hali hii ilihali unakinzana na sababu aliyoitaja na Hadiyth aliyoijengea hoja? Vipi iwe sahihi ubaguzi wa namna hii ilihali Hadiyth zimeenea kuhusu kulaaniwa kwa watu wa Kitabu kwa sababu ya kuyafanya makaburi ya Manabii wao kuwa misikiti? Isitoshe imethibiti kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametukataza hilo. Basi katazo hilo linahusu moja kwa moja kufanya makaburi ya Manabii kuwa ni sehemu ya kuswali, na wengine wanafuatwa katika hilo. Basi vipi linaeleweka jambo la kuwabagua!? Haki ni kwamba ubaguzi wa namna hii unaweza tu kueleweka kwa walioko katika maoni ya pili kuwa sababu ni najisi. Hakika makaburi ya Manabii bila shaka ni twahara, kwa kuwa amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika Allaah ameiharamishia ardhi kula miili ya Manabii.”

Lakini sababu hii ni batili. Kila kilichojengwa juu ya batili ni batili pia[1].

[1] Nimeeleza kwa kina kosa la at-Twahaawiy na mgongano wake juu ya upendeleo wake uliyotajwa hapo juu katika kitabu changu ”ath-Thamar al-Mustatwaab fiy Fiqh-is-Sunnah wal-Kitaab”.

  • Muhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 269-275
  • Imechapishwa: 12/08/2026