7 – Kuswali kuelekea makaburi, kutokana na Hadiyth iliyotangulia punde kidogo:

”Msiswali kuelekea makaburi…”

Ndani yake kuna dalili ya uharamu wa kuswali kuelekea kaburi kutokana na udhahiri wa katazo hilo. Huu ndio msimamo wa an-Nawawiy. al-Manaawiy amesmea katika ”Faydhw-ul-Qadiyr” alipokuwa akitoa maelezo ya Hadiyth hiyo:

”Kwa maana hali ya kuyaelekea, kwa sababu kufanya hivo kunaashiria matukuzo ya hali ya juu ambalo ni kiwango cha kuabudiwa. Imekusanya – kwa maana ya Hadiyth yote kwa ujumla – kati ya katazo la kudharau utukufu na utukufu wa hali ya juu.”

Kisha akasema katika sehemu nyingine:

”Hakika hilo linachukiza. Ikiwa mtu atakusudia kutafuta baraka kwa kuswali katika eneo hilo, basi amezusha jambo katika dini ambalo Allaah hakuliruhusu. Makusudio hapa ni machukizo ya kuchukiza kabisa. an-Nawawiy amesema: ”Hivo ndivo wamesema wenzetu. Lau mtu atasema ni haramu kwa dhahiri ya Hadiyth itakuwa haiko mbali. Inachukuliwa kutokana na Hadiyth hiyo katazo la kuswali kwenye makaburi. Kwa hiyo inachukiza machukizo ya uharamu.”

Inapaswa kujulikana kwamba hiyo haramu iliyotajwa ni pale tu ikiwa mtu kwa kuelekea kwake hakukusudia kulitukuza kaburi. Vinginevyo ni shirki. Shaykh ‘Aliy al-Qaariy amesema katika ”al-Mirqaat” (2/372) alipokuwa anaitolea maelezo Hadiyth hiyo:

”Lau heshima hiyo ingekuwa ya kweli juu ya kaburi na kwa mwenye kaburi, basi aliyemtukuza angekuwa kafiri, basi kujifananisha naye kunachukiza. Katika hali hiyo inapasa iwe machukizo ya uharamu. Katika maana hiyo – bali zaidi – ni jeneza lililowekwa chini, na hilo ndilo ambalo watu wa Makkah wamepatiwa mtihani kwalo, ambapo huweka jeneza mbele ya Ka‘bah kisha huswali kulielekea.”

  • Muhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 269
  • Imechapishwa: 12/08/2026