138. Maandiko yaliyo wazi yasiyokubali tafsiri nyingine

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Aidha kila mmoja katika hawa anapinga kwa hoja aina ileile. Hilo ni kwa njia nyingi:

1 – Akili haipelekei katika hayo yaliyotajwa hapo juu.

2 – Maandiko yaliyopokelewa hayatakiwi kupindishwa maana.

3 – Kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifikisha elimu ni jambo halina shaka kama ambavyo alifikisha elimu kuhusu vipindi vitano vya swalah na kufunga mwezi wa Ramadhaan. Kuyapindisha maana hayo kumefanana na tafsiri mbovu za Qaraamitwah na Baatwiniyyah wakati walipofasiri hajj, swawm, swalah na mengine yote waliyokuja nayo Mitume.

4 – Akili timamu inaafikiana na Qur-aan na Sunnah. Ingawa akili haiwezi kuyaelewa kwa upambanuzi yale yote yaliyomo ndani ya Qur-aan na Sunnah isipokuwa tu anaweza kufahamu kwa njia ya ujumla. Kwa kuongezea ni kwamba wanamme mashuhuri zaidi wa nadharia hizi wao wenyewe wamekiri kuwa akili haiwezi kamwe kuchangia yakini katika mambo mengi ya kiungu. Mambo yakishakuwa hivo, basi ni lazima kupokea elimu ya mambo hayo kutoka kwa Mitume kama jinsi ilivyo.

MAELEZO

Kusema kwao kwamba akili inazuia kadhaa na kadhaa ni jambo lisilokuwa na dalili yoyote. Jengine ni kwamba dalili haiwezi kutumiwa kama dalili juu ya kitu isichokizunguka wala kukifahamu. Kwa hiyo hii ndio dalili ya kwanza juu ya ubatili wa maoni yao.

Jambo la pili ni kwamba Maandiko yaliyokuja juu yake yako wazi. Si kwamba Maandiko yanaweza kufahamika kwa namna mbalimbali mpaka uweze kusema kuwa kinachokubali kupindishwa maana ni kile kisicho wazi. Kwa mfano maneno Yake (Subhaanahu wa Ta´ala):

الرَّحْمَنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَى

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”[1]

yako wazi katika kuthibitisha kuwa Allaah amelingana juu ya ´Arshi. Haiwezekani kubeba maana nyingine isipokuwa kulingana Kwake (Ta´ala) juu ya ´Arshi. Maneno Yake (Ta´ala) tena Aliposema:

وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ

“Naye yujuu kabisa, Ametukuka.”[2]

yako wazi katika kuthibitisha ujuu. Maneno Yake (Ta´ala):

وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ

“Naye ni Mshindi Mwenye kudhibiti [aliye] juu ya waja Wake.”[3]

yako wazi katika kuthibitisha kuwa Allaah yuko juu ya viumbe Vyake. Hayawezi kuwa na tafsiri nyingine. Maneno Yake (Ta´ala):

وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

”Naye kwa kila kitu ni Mjuzi.”[4]

yako wazi katika kuthibitisha ujuzi wa Allaah. Hayawezi kuwa na tafsiri nyingine. Maneno Yake (Ta´ala):

وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

“Naye juu ya kila kitu ni Muweza.”[5]

yako wazi katika kuthibitisha uwezo wa Allaah. Hayawezi kuwa na tafsiri nyingine.

[1] 20:5

[2] 2:255

[3] 6:18

[4] 2:29

[5] 5:120

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 226-227
  • Imechapishwa: 15/07/2026