Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:
111 – Imani ni kukubali kwa ulimi na kusadikisha kwa moyo.
MAELEZO
Huu ni utambulisho wa Murji-ah. Wameifupisha imani kwa kutamka kwa ulimi na kusadikisha kwa moyo. Maoni sahihi ni kwamba imani ni kutamka kwa ulimi, kuamini moyoni na matendo ya viungo vya mwili. Matendo yanaingia katika imani na sio kitu kilicho nje ya imani. Yule anayetosheka na kutamka kwa mdomo na kusadikisha kwa moyo pasi na kufanya matendo, sio katika watu wenye imani sahihi.
Imani ni kutamka kwa ulimi, kuamini moyoni na matendo ya viungo vya mwili. Inazidi kwa matendo mema na inashuka kwa maasi. Allaah (Ta´ala) amesema:
إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ
“Hakika si venginevyo waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah, basi nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayah Zake huwazidishia imani na kwa Mola wao wanategemea.”[1]
وَإِذَا مَا أُنزِلَتْ سُورَةٌ فَمِنْهُم مَّن يَقُولُ أَيُّكُمْ زَادَتْهُ هَـٰذِهِ إِيمَانًا ۚ فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا فَزَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَهُمْ يَسْتَبْشِرُونَ
“Na inapoteremshwa Suurah, basi miongoni mwao wako wanaosema: “Nani kati yenu [Suurah] hii imemzidishia imani?” Ama wale walioamini huwazidishia imani nao wanafurahia.”[2]
وَيَزْدَادَ الَّذِينَ آمَنُوا إِيمَانًا
“… na iwazidishie imani wale walioamini.”[3]
Aayah hizi zinajulisha kuwa imani inashuka. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Yule katika nyinyi atakayeona maovu, basi ayakemee kwa mkono wake. Asipoweza, afanye hivo kwa ulimi wake. Asipoweza, basi afanye hivo kwa moyo wake – na hiyo ni imani dhaifu kabisa.”[4]
Hiyo ikafahamisha kuwa imani inashuka. Imekuja katika upokezi mwingine:
”… mpaka inakuwa sawa na uzito wa mbegu ya haradali.”[5]
Hiyo inafahamisha kuwa imani inashuka mpaka inakuwa na uzito sawa na mbegu ya hadarali. Katika Hadiyth nyingine anasema Allaah (Tabaarak wa Ta´ala):
“Mtoeni Motoni yule ambaye moyoni mwake kuna imani sawa na dinari, kisha yule ambaye moyoni mwake kuna imani sawa na nusu dinari, kisha yule ambaye moyoni mwake kuna imani sawa na kokwa ya tende, kisha yule ambaye moyoni mwake kuna imani sawa na dudu mchungu na halafu yule ambaye yuko na imani ya chini chini chini kabisa kuliko dudu mchugu.”[6]
Imani ni kutamka kwa ulimi, kuamini moyoni na matendo ya viungo vya mwili. Inazidi kwa utiifu na inapungua kwa kuasi. Hii ndio maana sahihi ya imani iliyochukuliwa kutoka katika Qur-aan na Sunnah.
[1]8:2-4
[2]9:124
[3]74:31
[4]Muslim (49).
[5]Muslim (50).
[6]al-Bukhaariy (7510) na Muslim (193).
- Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 145-146
- Imechapishwa: 19/11/2024
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)