136. Ndio maana wakapinga Kulingana kwa Allaah juu ya ´Arshi

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Na ambaye anadai kuwa Allaah hayuko juu ya ´Arshi anadai kwamba akili ndio imemwelekeza huko na ndio maana akalazimika kulipindishia maana. Inatosha kuonyesha uharibifu wa ´Aqiydah ya watu hawa kule kwamba hakuna yeyote katika wao ambaye ana kigezo imara juu ya yale yanayoelekezwa na akili. Bali ambayo baadhi wanaona kuwa akili imeyaona yanafaa bali kuyawajibisha, ilihali wengine wanaona kuwa hayafai. Laiti ningelijua ni kwa akili gani inatakiwa kuipima Qur-aan na Sunnah.

MAELEZO

Vivyo hivyo mwenye kukanusha kulingana kwa Allaah juu ya ´Arshi na kuwa Kwake juu ya viumbe anafanya hivo kwa kuona kuwa akili inakataa jambo hili. Kwa sababu tukisema kuwa Allaah amelingana juu ya ´Arshi, basi atakuwa anaihitajia ´Arshi na atakuwa katika upande na Allaah hayuko katika upande. Hivyo wameweka misingi kutoka kwa nafsi zao, kisha wakaanza kuihukumu Qur-aan na Sunnah kwa misingi hiyo.

Akili haiwezi kumfahamu Allaah (´Azza wa Jall) kwa kumzunguka. Hili ni jambo lililo nje ya uwezo wa akili kulifikia. Akili timamu hailikatai jambo hili, bali hujisalimisha kwa Allaah, humuamini Allaah, husadikisha khabari za Allaah na khabari za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), na hujua kwamba Allaah ni Muweza juu ya kila kitu na kwamba hakuna chochote kinachomshinda Allaah.

Inakutosha kuwa dalili ya ubatili wa ´Aqiydah yao ni kwamba hawakukubaliana juu ya hoja moja wanayoitegemea katika kukanusha yale waliyoyakanusha. Mgongano wao ni dalili ya ubatilifu wa ´Aqiydah yao. Hii ni dalili ya mkanganyiko wao na ubatili wa ´Aqiydah yao, kwa kuwa hawakukubaliana juu ya jambo lolote katika ´Aqiydah yao.

Je, akili ndio yenye kupima Qur-aan na Sunnah? Qur-aan na Sunnah ni wahy kutoka kwa Allaah, ambaye ni Mjuzi na Mwenye khabari zote. Ama akili ni mawazo ya wanadamu na ufahamu wao. Je, mawazo ya wanadamu na akili zao vinaweza kupimwa na wahy ulioteremshwa ambao:

لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِ تَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيد

“Haiingiliwi na batili mbele na nyuma yake – ni Uteremsho kutoka kwa Mwenye hekima, Mwenye kuhimidiwa.”[1]

Hili haliwezekani. Haiwezekani Qur-aan na Sunnah vikapimwa kwa akili.

[1] 41:42

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 224-225
  • Imechapishwa: 14/07/2026