Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Yule mwenye kupinga Kuonekana anadai kuwa akili ndio imemwelekeza kufanya hivo na ndio maana amelazimika kuipindishia maana. Yule mwenye kuona kuwa ujuzi na uwezo wa Allaah ni mambo yasiyowezekana na maneno Yake kutokuumbwa anafanya hivo kwa sababu anaona kuwa akili ndio imemwelekeza kufanya hivo na ndio maana akalazimika kuyapindishia maana.

MAELEZO

Mwenye kukanusha kuwa waumini watamuona Mola wao siku ya Qiyaamah, jambo ambalo dalili za kuthibitisha kwake zimefikia kiwango cha kupokelewa kwa mapokezi tele, hujenga ukanushaji wake juu ya akili. Wanasema kuwa tukithibitisha Kuonekana, basi italazimu Allaah awe katika upande. Kwa mujibu wao wanaona kuwa Allaah hayuko katika upande na hoja tata zingine kama hizo. Lau wangefuata dalili za Qur-aan na Sunnah, wakaziamini na wala wasiingize akili zao ndani yake, basi wangesalimika.

Anayesema kuwa haiwezekani Allaah kuwa na ujuzi na haiwezekani Allaah kuwa na uwezo kwa sababu hizi ni sifa za viumbe – na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) si kama viumbe. Wanaona kuwa eti wakimthibitishia Allaah ujuzi na uwezo basi watakuwa wamemfananisha na viumbe. Kwa sababu sifa hizi zipo kwao. Hii ndio hoja yao tata. Hawakutambua kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ana ujuzi na uwezo usiyofanana na ujuzi na uwezo wa viumbe. Ni kama vile dhati Yake haifanani na dhati za viumbe.

Wanasema kwa sababu tukimthibitishia Allaah kuzungumza, basi basi itapelekea matatizo. Baadhi yao husema kuwa kufanya hivo kuna kumfananisha na viumbe, kwa sababu viumbe huzungumza – na hakuna kufanana kati ya kiumbe na Muumba. Wengine husema kuwa kuzungumza ni katika mambo yanayozuka – na Allaah hawezi kuwa kitu kinachozuka. Wana mambo mengine katika ukhurafi. Lau wangejisalimisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na kuthibitisha kwamba Allaah anazungumza kwa namna inayolingana na utukufu Wake, basi wangesalimika na khatari hizi.

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 222-223
  • Imechapishwa: 14/07/2026