133. Dalili ya ulazima wa kufanya Hijrah na matishio kwa anayeacha ilihali ana uwezo


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

إِنَّ الَّذِينَ تَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ ظَالِمِي أَنفُسِهِمْ قَالُوا فِيمَ كُنتُمْ ۖ قَالُوا كُنَّا مُسْتَضْعَفِينَ فِي الْأَرْضِ ۚقَالُوا أَلَمْ تَكُنْ أَرْضُ اللَّـهِ وَاسِعَةً فَتُهَاجِرُوا فِيهَا ۚ فَأُولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا إِلَّا الْمُسْتَضْعَفِينَ مِنَ الرِّجَالِ وَالنِّسَاءِ وَالْوِلْدَانِ لَا يَسْتَطِيعُونَ حِيلَةً وَلَا يَهْتَدُونَ سَبِيلًا فَأُولَـٰئِكَ عَسَى اللَّـهُ أَن يَعْفُوَ عَنْهُمْ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ عَفُوًّا غَفُورًا

“Hakika wale ambao Malaika wamewafisha hali wamejidhulumu nafsi zao, wataulizwa: “Mlikuwa katika hali gani?” Watasema: “Tulikuwa tukikandamizwa katika ardhi”, [Malaika] watasema: “Je, kwani ardhi ya Allaah haikuwa pana mkahajiri?” Basi hao makazi yao yatakuwa ni Motoni – na ubaya ulioje mahali pa kurejea! Isipokuwa wale waliokandamizwa – kati ya wanaume na wanawake na watoto – ambao hawakuweza kupata namna yoyote wala hawawezi kuongoza njia. Basi hao huenda Allaah akawasamehe – Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa kughufiria.”[1]

MAELEZO

Katika Aayah mbili hizi kuna matishio kwa yule mwenye kuacha kuhama ilihali anao uwezo wa kufanya hivo na kwamba makafio yake ni Motoni – ijapokuwa si mwenye kutoka nje ya Uislamu – lakini haya ni miongoni mwa maandiko ya matishio. Ingawa kuacha kuhama ni kuacha jambo la wajibu na anakuwa ni mtenda dhambi. Lakini mtu hatoki nje ya Uislamu kwa kuacha kuhama. Kisha juu yake kuna matishio makali. Kisha Allaah akabainisha kwa Aayah zilizo baada yake nyudhuru zinazoangusha ulazima wa kuhama. Amesema (Ta´ala):

إِلَّا الْمُسْتَضْعَفِينَ مِنَ الرِّجَالِ وَالنِّسَاءِ وَالْوِلْدَانِ لَا يَسْتَطِيعُونَ حِيلَةً ا

“Isipokuwa wale waliokandamizwa – kati ya wanaume na wanawake na watoto – ambao hawakuweza kupata namna yoyote… “

Hawana uwezo wowote.

وَلَا يَهْتَدُونَ سَبِيلًا

“… wala hawawezi kuongoza njia.”

Bi maana ambao hawakuijua njia ya kuelekea katika mji wa Madiynah. Kwa sababu kuhama kunahitajia kusafiri. Vinginevyo mtu anakuwa ni mwenye kuangamia wakati wa kuhama ikiwa hajui njia. Kwa hiyo nyudhuru zao zinakuwa kwa njia mbili:

Ya kwanza: Hawana namna yoyote.

Ya pili: Hawawezi kuongoza njia. Hata kama mtu atakuwa na uwezo wa kimali lakini hata hivyo hajui njia ya kupita wala wa kumwongoza, hizi ndio nyudhuru sahihi. Kuhusu mtu ambaye anao uwezo na anajua njia hana udhuru wowote.

[1] 04:97-100

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 267-268
  • Imechapishwa: 11/02/2021