123 – Mtu asitembee kati ya makaburi ya waislamu akiwa amevaa viatu vyake. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Bashiyr al-Handhwaliy ambaye amesema:

”Nilipokuwa nikitembea pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)… alipita kwenye makaburi ya waislamu … alipokuwa akitembea, mara akatazama kwa haraka na tahamaki akamuona mtu anatembea kati ya makaburi akiwa amevaa viatu ambapo akasema: ”Ee mwenye viatu vua viatu vyako!” Akaangalia na alipomtambua mtu huyo kuwa ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivua viatu vyake na kuvitupa.”

Wameipokea watunzi wa as-Sunan na wengineo na imekwishatangulia kwa ukamilifu wake katika masuala ya 88.

Haafidhw amesema katika ”al-Fath” (3/160):

”Hadiyth inafahamisha ya kwamba inachukiza kutembea kati ya makaburi ukiwa umevaa viatu. Ibn Hazm amesema jambo la ajabu kwamba ni haramu kutembea kati ya makaburi kwa viatu vya ngozi ya mnyama iliyonyambuliwa (النعال السبتية) bila vya aina nyingine, jambo ambalo ni ugumu mkali. Kuhusu maneno ya al-Khattwaabiy kwamba huenda kukatazwa huko ni kwa sababu ya majivuno yaliyomo katika viatu hivyo, basi imejibiwa kwamba Ibn ´Umar alikuwa akivaa viatu aina hiyo na akisema kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akivivaa, nayo ni Hadiyth Swahiyh. at-Twahaawiy amesema:

”Kukatazwa kwa mtu huyu kulitokana na kuwepo uchafu katika viatu vyake, kwani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali akiwa amevaa viatu vyake muda wa kuwa haoni kuwa vina uchafu.”

Uwezekano huu uko mbali kabisa. Bali Ibn Hazm amethibitisha (5/137) kuwa ni batili na kwamba ni uzushi juu ya Allaah (´Azza wa Jall). Lililo karibu zaidi ni kuwa kukatazwa huku ni kwa ajili ya kuwaheshimu wafu, nalo ni kama katazo la kukalia kaburi lililotajwa katika masuala ya 128 kifungu cha 6. Kwa hiyo hakuna tofauti kati ya viatu vya ngozi ya mnyama iliyonyambuliwa na vingine vyenye manyoya, kwani vyote vinafanana katika suala la kutembea navyo kati ya makaburi na kuwa kinyume na heshima kwa wafu. Hili limefafanuliwa na Ibn-ul-Qayyim katika ”Tahdhiyb-us-Sunan” (4/343–345) na amesimulia kutoka kwa Imaam Ahmad ya kuwa amesema:

”Hadiyth ya Bashiyr cheni ya wapokezi wake ni nzuri na naitendea kazi isipokuwa kutokana na kasoro.”

Imekwishathibiti ya kuwa Imaam Ahmad alikuwa akiifanyia kazi Hadiyth hii. Abu Daawuud amesema katika ”Masaa-il” yake, uk. 158:

”Nilimuona Ahmad akisindikiza jeneza na akakaribia kufika makaburini, basi huvua viatu vyake.”

Allaah amrehemu. Ni namna gani iliyoje alivyokuwa akifuata Sunnah!

  • Muhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 252-253
  • Imechapishwa: 10/08/2026