Kuhusu wale wanaolingania katika fikira nyenginezo, kama mfano wa ulinganizi wa Qaadiyaaniyyah na wengine ambao wanawaita watu kumfuata Nabii mpya, Mtume mpya, basi itambulike kuwa ulinganizi wao ni batili na fikira zao ni zenye kupotosha na za uongo. Kwa sababu Allaah (´Azza wa Jall) amebainisha ndani ya Kitabu Chake kinachobainisha ya kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye mwisho wa Manabii. Hayo vilevile yamepokelewa katika Hadiyth tele kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Mitume waliomtangulia walimbashiria. Allaah (Ta´ala) amesema:

مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ

“Hakuwa Muhammad baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Mtume wa Allaah na ni mwisho wa Manabii.”[1]

Lakini wako watu wanaofanana na wanyama. Wanatatizwa na kila dai, kimefichika kwao kila kitu na hawapambanui haki na batili na wala hawafarikishi kati ya uongofu na upotofu. Wanatatizika na kila madai na kelele. Yote haya ni kwa kukosa elimu na uelewa. Kwa ajili hii ndio maana akapata kunyanyua sauti yake mtu huyu kwa jina Mirzaa Ghulaam Ahmad kwa ulinganizi wake wa batili. Matokeo yake akafuatwa na watu ambao wamefanana na wanyama na wakayaamini yale aliyoyasema na kuyaandika yanayohusiana na maudhui haya, mambo yanayokwenda kinyume na Kitabu kitukufu na yale yaliyopokelewa kwa Sunnah tele kutoka kwa Mteule (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba yeye ndiye mwisho wa Manabii na Mitume. Inakuweje kutokee kitu kama hiki? Ni vipi kitu kama hiki kiwatatize wale wanaotokana na wanaadamu ambao ni katika watu wenye akili na ambao wanasoma na wanaandika ilihali upotofu wake ni miongoni mwa mambo yaliyo wazi zaidi? Lakini Allaah anataka kuwaonyesha waja Wake maajabu na mafunzo ambayo ndani yake kuna mawaidha na ukumbusho kwa kila mwenye akili. Amesema (Subhaanah):

فَإِنَّهَا لَا تَعْمَى الْأَبْصَارُ وَلَـٰكِن تَعْمَى الْقُلُوبُ الَّتِي فِي الصُّدُورِ

“Hakika hayapofuki macho, bali zinazopofuka ni nyoyo ziliomo vifuani.”[2]

[1] 33:40

[2] 22:46

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahamiyyat-ul-´Ilm https://binbaz.org.sa/discussions/33/اهمية-العلم-في-محاربة-الافكار-الهدامة
  • Imechapishwa: 15/05/2022