5- Mfungaji anazo furaha mbili; furaha ya kwanza ni pale anapokata swawm na furaha ya pili ni pale atapokutana na Mola Wake. Ama kuhusu furaha yake wakati wa kufutari ni kwamba anafurahi kwa yale ambayo Allaah amemneemesha katika kutekeleza ´ibaada ya swawm ambayo ni miongoni mwa matendo mema bora. Ni watu wangapi hawakujaaliwa kufunga? Pia anafurahi kwa kile chakula na kinywaji ambacho Allaah amemhalalishia na pia tendo la ndoa ambalo lilikuwa haramu kwake kipindi cha funga.

Kuhusu furaha yake wakati wa kukutana na Mola Wake ni kwamba atafurahi kwa swawm yake wakati atapokutana na malipo Yake mbele ya Allaah (Ta´ala) hali ya kuwa yametimizwa kikamilifu katika wakati ambapo ndipo atakuwa ni mwenye kuyahitajia zaidi wakati atapoambiwa:

“Wako wapi wafungaji waingie Peponi kupitia mlango wa ar-Rayyaan ambao haupitiwi na yeyote zaidi yao?”

Katika Hadiyth hii kuna maelekezo kwa mfungaji pindi anapotukanywa na yeyote au kutaka kupambana naye kwamba asimkabili kwa mfano wake. Lengo ni ili matusi na mapigano yasizidi na asidhoofike mbele yake kwa kuwa kimya. Bali anapaswa kumweleza kwamba yeye amefunga. Hiyo ni ishara kwamba yeye hatomkabili kwa mfano wake. Hayo ni kwa ajili ya kuiheshimu funga na si kushindwa kulipiza. Hapo matusi na mapigano yatasita:

ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ فَإِذَا الَّذِي بَيْنَكَ وَبَيْنَهُ عَدَاوَةٌ كَأَنَّهُ وَلِيٌّ حَمِيمٌ وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا الَّذِينَ صَبَرُوا وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا ذُو حَظٍّ عَظِيمٍ

“Lipiza [uovu] kwa ambalo ni zuri zaidi. Tahamaki yule ambaye kati yako na yeye kuna uadui, atakuwa kama ni rafiki mwandani. Hapewi hayo isipokuwa wale wenye subira na hapewi hayo isipokuwa mwenye fungu kuu.” [1]

[1] 41:34-35

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 16-17
  • Imechapishwa: 09/04/2020