Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:
103 – Hatumkufurishi yeyote katika wanaoswali kuelekea Qiblah muda wa kuwa hajaihalalisha.
MAELEZO
Haya ni kama tulivyotangulia kusema kwamba muda wa kuwa dhambi hiyo sio kufuru au shirki inayomtoa mtu nje ya dini. Vinginevyo hatumkufurishi mtu kutokana na dhambi. Bali tunaona kuwa ni muislamu, ijapo imani yake ni pungufu na yuko katika khatari ya kuadhibiwa na chini ya utashi wa Allaah. Hii ndio ´Aqiydah ya muislamu. Lakini akihalalisha kile alichokiharamisha Allaah, anakufuru. Yule anayehalalisha kile alichoharamisha Allaah kama mfano wa ribaa, pombe, mzoga, nyama ya nguruwe au uzinzi, anamkufuru Allaah. Vivyo hivyo yule anayeharamisha kile alichohalalisha Allaah anakufuru:
اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ وَالْمَسِيحَ ابْنَ مَرْيَمَ
“Wamewafanya marabi wao na watawa wao kuwa ni waungu badala ya Allaah na al-Masiyh, mwana wa Maryam.”[1]
´Adiyy bin Haatim (Radhiya Allaahu ´anh) wakati alipomsikia Mtume (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) akisoma Aayah hii akasema:
“Ee Mtume wa Allaah! Tulikuwa hatuwaabudu.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Je, si walikuwa wakihalalisha yale yaliyoharamishwa na Allaah nanyi mnayahalalisha na wakiharamisha yale yaliyoharamishwa na Allaah nanyi mnayaharamisha?” Akajibu: “Ndio.” Akasema: “Huku ndio kuwaabudu.”[2]
Lakini akifanya dhambi pasi na kuona kuwa ni halali, anakubali kuwa ni haramu, mtu huyo hakufuru, hata kama dhambi hiyo ni kubwa chini ya shirki na kufuru. Mtu kama huyo anakuwa muumini mwenye imani pungufu au pia ni fasiki kwa dhambi yake kubwa, muumini kwa imani yake. Mtunzi wa kitabu amesema:
“… muda wa kuwa hajaihalalisha.”
Haichukuliwi namna hii kwa njia isiyofungamana. Kwa mfano mwenye kuacha swalah kwa makusudi ni kafiri. Hivyo ndivo inafahamisha Qur-aan na Sunnah.
[1] 9:31
[2]at-Tirmidhiy (3095), at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Kabiyr” (218), al-Bayhaqiy katika ”as-Sunan al-Kubraa” (20137). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Ghaayat-ul-Maraam” (6).
- Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 139-140
- Imechapishwa: 17/11/2024
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)