Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

101 – Ameteremka nayo roho mwaminifu akamfunza nayo bwana wa Mitume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

MAELEZO

Roho mwaminifu ni Jibriyl (´alayhis-Salaam). Ameitwa hivyo kwa sababu ni mwenye kuaminiwa hageuzi wala habadilishi. Ni mwenye kuaminiwa juu ya yale aliyombebesha Allaah.Hatuhumiwi ukhaini, kama wanavosema mayahudi. Mayahudi wanasema kuwa Jibriyl ni adui yao. Pia Shiy´ah waliochupa mipaka wanasema kuwa Ujumbe ni wa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) na kwamba Jibriyl alifanya ukhaini na akamfikishia nao Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Huku ni kumkadhibisha Allaah kwa sababu Allaah amemwita kuwa ni mwaminifu. Allaah (Ta´ala) akasema kuhusu mayahudi:

قُلْ مَن كَانَ عَدُوًّا لِّجِبْرِيلَ فَإِنَّهُ نَزَّلَهُ عَلَىٰ قَلْبِكَ بِإِذْنِ اللَّـهِ مُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ وَهُدًى وَبُشْرَىٰ لِلْمُؤْمِنِينَ مَن كَانَ عَدُوًّا لِّلَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَرُسُلِهِ وَجِبْرِيلَ وَمِيكَالَ فَإِنَّ اللَّـهَ عَدُوٌّ لِّلْكَافِرِينَ

“Sema: “Yeyote aliyekuwa adui wa Jibriyl, basi hakika yeye ameiteremsha Qur-aan katika moyo wako kwa Idhini ya Allaah inayosadikisha yaliyo kabla yake, na mwongozo na bishara njema kwa waumini. Yeyote aliyekuwa adui wa Allaah na Malaika Wake na Mtume Wake na Jibriyl na Miykaaiyl, basi hakika Allaah ni adui wa makafiri.”[1]

Yule mwenye kumfanya Jibriyl kuwa adui au Malaika miongoni mwa Malaika, basi mtu huyo ni adui wa Allaah. Vivyo hivyo yule mwenye kumfanya adui Mtume yeyote miongoni mwa Mitume – ni kafiri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) amesema kuhusu yule mwenye kumfanya adui walii miongoni mwa mawalii wa Allaah:

”Yeyote atakayemfanyia uadui walii Wangu basi ninatangaza vita dhidi yake.”[2]

Jibriyl amemfunza Qur-aan Mtume (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam). Allaah (Ta´ala) amesema:

عَلَّمَهُ شَدِيدُ الْقُوَىٰ ذُو مِرَّةٍ فَاسْتَوَىٰ وَهُوَ بِالْأُفُقِ الْأَعْلَىٰ

“… amemfunza mwenye nguvu madhubuti. Mwenye muonekano mwema na akalingamana sawasawa. Naye yuko juu kabisa katika upeo wa macho.”[3]

Mwenye nguvu madhubuti, akikusudiwa Jibriyl, ndiye ambaye amemfunza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hayo yalifanyika kwa amri ya Allaah (Ta´ala).

[1]2:97-98

[2]al-Bukhaariy (6502).

[3]53:5-7

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 136-137
  • Imechapishwa: 13/11/2024