Lengo la kutembelea makaburi ni mambo mawili:

1 – Kumnufaisha mtembeleaji kwa kukumbuka mauti na wafu na kwamba mafikio yao ya mwisho ni aidha Pepo au Moto. Hili ndilo lengo la kwanza la matembezi, kama zinavyoashiria Hadiyth zilizotangulia.

2 – Kumfaidisha maiti na kumfanyia wema kwa kumsalimu, kumuombea du´aa na kumuombea msamaha, mambo ambayo ni maalum kwa muislamu. Kuna Hadiyth kadhaa juu ya hilo:

1 – ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitoka kwenda kwenye makaburi ya Baqiy´ na akiwaombea du´aa. ´Aaishah akamuuliza juu ya hilo ambapo kasema: ”Hakika mimi nimeamrishwa kuwaombea du´aa.”

Ameipokea Ahmad (6/252) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kwa sharti za al-Bukhaariy na Muslim. Maana yake imo kwa Muslim na wengineo kwa njia nyingine kwa urefu. Imekwishatangulia kwa ukamilifu wake katika masuala ya 119.

2 – Pia kutoka kwake (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesimulia:

”Kila ilipokuwa usiku wake basi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akitoka mwishoni mwa usiku na kusema:

السلام عليكم [أهل] دار قوم مؤمنين، وإنا وإياكم وما توعدن غدا مؤجلون، وإنا إن شاء الله بكم لاحقون، اللهم اغفر لاهل بقيع الغرقد

”Amani iwe juu yenu waumini [wakazi] wa nyumba hii. Hakika sisi na nyinyi hiyo kesho tutapata kile kilichoahirishwa. Nasi – Allaah akitaka – tutakutana nanyi. Ee Allaah wasamehe wakazi wa Baqiy´ al-Gharqad.”

Ameipokea Muslim (3/63), an-Nasaa’iy (1/287), Ibn-us-Sunniy (585), al-Bayhaqiy (4/79) na Ahmad (6/180) ambaye kwake hakuna du´aa ya kuwaombea msamaha. Ziada ni ya Ibn-us-Sunniy.

3 – Pia kutoka kwake (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesimulia katika Hadiyth yake ndefu ambayo muda si mrefu sana imeashiriwa ambapo alisema: ”Niwaambieje, ee Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?” Akasema: ”Sema:

السلام على أهل الديار من المؤمنين والمسلمين، ويرحم الله المستقدمين منا والمستأخرين، وإنا إن شاء الله بكم للاحقون

”Amani iwe juu ya wenyeji wa nyumba hii, miongoni mwa waumini na waislamu, Allaah awarehemu waliotutangulia na watakaokuja nyuma, na sisi – Allaah akitaka – tutakutana nanyi.”

Ameipokea Muslim na wengineo.

4 – Buraydah ameeleza:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anawafundisha walipotoka kwenda makaburini, basi msemaji wao alikuwa husema:

السلام عليكم أهل الديار من المؤمنين والمسلمين، وإنا إن شاء الله [بكم] للاحقون، [أنتم لنا فرط، ونحن لكم تبع]، أسأل الله لنا ولكم العافية

“Amani iwe juu yenu, enyi wakazi wa nyumba hii, miongoni mwa waumini na waislamu, na sisi – Allaah akitaka – tutakutana [nanyi]. [Nyinyi ni mtangulizi wetu na sisi ni wenye kukufuatane.] Ninamuomba Allaah atujaalie sisi na nyinyi usalama.”

Ameipokea Muslim (3/65), an-Nasaa’iy na Ibn Maajah (1/469), pamoja na Ibn Abiy Shaybah (4/138), Ibn-us-Sunniy (582), al-Bayhaqiy na Ahmad (5/353, 359, 360). Ziada zote mbili ni zao, isipokuwa Ibn Majah na Muslim. ziada ya pili ameipokea Ibn Abiy Shaybah kutoka katika Hadiyth ya ´Aliy na cheni yake ya wapokezi ni Swahiyh na kutoka katika Hadiyth ya Salmaan (na cheni yake ya wapokezi ni nzuri), na zote mbili ni masimulizi ya wawili hao.

5 – Abu Hurayrah ameeleza:

”Hakika Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuja makaburini ambapo akasema:

السلام عليكم دار قوم مؤمنين، وإنا إن شاء الله بكم لا حقون

”Amani iwe juu yenu, enyi watu wa nyumba ya waumini, na sisi – Allaah akitaka – tutaungana na nyinyi.”

Nimetamani lau tungaliwaona ndugu zetu.” Wakasema: “Je sisi si ndugu zako, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “[Bali] nyinyi ni Maswahabah wangu. Ndugu zetu ni wale watakaokuja baadaye [nami nitawatangulia katika Hodhi].”
Wakasema: “Utawezaje kuwajua wale ambao bado hawajaja miongoni mwa ummah wako, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: ”Mnaonaje lau mtu ana farasi wenye alama nyeupe na miguu yenye weupe kati ya farasi weusi wa kawaida, je, hawezi kuwajua farasi wake?” Wakasema: ”Ndio, ee Mtume wa Allaah.” Akasema: “Hakika wao watakuja [siku ya Qiyaamah] wakiwa na nyuso na miguu yenye kung’aa kwa sababu ya wudhuu´. [Haya anayasema mara tatu], nami nitawatangulia katika Hodhi. Hakika watafukuzwa watu [miongoni mwenu] mbali na Hodhi yangu kama vile ngamia wa pori wanavyofukuzwa. Nitawaita: ”Haya njooni, [haya njooni!”] Itasemwa: ”Hakika wao wamebadilisha baada yako [na walikuwa wakirudi nyuma kwa visigino vyao].” Nitasema: ”[Hapana], mbali, mbali kabisa!”

Ameipokea Muslim (1/150-151), Maalik (1/49-50), an-Nasaa’iy (1/35), Ibn Maajah (2/580), al-Bayhaqiy (4/78) na Ahmad (2/300, 408). Ziada zote ni zake isipokuwa mbili za mwisho ambazo ni za Ibn Maajah. Maalik ana tatu za mwanzo pamoja na ya sita. an-Nasaa’iy ana ya kwanza na ya tatu.

Katika mlango huu pia kuna Hadiyth kutoka kwa Bishr bin al-Khassaaswiyyah. Nimetaja matamshi yake katika maelezo ya masuala ya 88, ukurasa wa 135, pia kutoka kwa Ibn ‘Abbaas. Lakini ndani yake kuna udhaifu, kama itakavyobainishwa mwishoni mwa suala linalofuata baada ya hili na kutoka kwa ‘Umar na wengine, nazo pia zina udhaifu kama alivyobainisha Haafidhw al-Haythamiy katika ”al-Majma´” (3/60).

  • Muhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 239-241
  • Imechapishwa: 06/08/2026