118 – Inajuzu kutembelea kaburi la aliyekufa akiwa si muislamu kwa ajili ya kupata mazingatio tu. Kuna Hadiyth mbili juu ya hilo:

1 – Abu Hurayrah ameeleza:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alizuru kaburi la mama yake, akalia na akawaliza waliokuwa pambizoni mwake. Akasema: ”Nilimuomba ruhusa Mola wangu nimwombee msamaha, lakini hakuniruhusu, na nikamuomba idhini kutembelea kaburi lake ambapo akaniruhusu. Basi tembeleeni makaburi, kwani hakika yanakumbusha kifo.”

Ameipokea Muslim (3/65), Abu Daawuud (2/72), an-Nasaa’iy (1/286), Ibn Maajah (1/476), at-Twahaawiy (3/189), al-Haakim (1/375-376), na kutoka kwake al-Bayhaqiy (4/76) na Ahmad (2/441).

2 – Buraydah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

”Tulikuwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) [katika safari… ”

Imekuja katika upokezi mwingine:

”… katika vita vya Ufunguzi]. Basi tukapiga kambi naye na sisi tulikuwa naye takriban wapanda farasi 1, 000. Akaswali Rak´ah mbili, kisha akatuelekea kwa uso wake huku macho yake yakitiririka machozi. ´Umar bin al-Khattwaab akasimama kumwelekea na akamwambia: ”Ee Mtume wa Allaah, nini kimekufika?” Akasema: ”Nimemuomba Mola wangu (´Azza wa Jall) aniruhusu niombee msamaha mama yangu, lakini hakuniruhusu, macho yangu yakatiririka kwa kumuonea huruma kutokana na Moto. [Nikamuomba Mola wangu aniruhusu kulitembelea kaburi lake ambapo akaniruhusu]. Hakika mimi nilikuwa nimekukatazeni kuyatembelea makaburi, basi sasa yatembeleeni. Kuyatembelea kwake kuwazidishieni kheri.”

Ameipokea Ahmad (5/355, 357, 359), Ibn Abiy Shaybah (4/139). Riwaya nyingine ni ya wawili hao. Cheni ya wawili hao kwa Ibn Abiy Shaybah ni Swahiyh, al-Haakim (1/376), vilevile Ibn Hibbaan (791), al-Bayhaqiy (4/76). Ziada ya kwanza ni ya kwao. Riwaya nyingine ni ya wale ambao nimetangulia kuwataja. Ziada nyingine ni ya al-Haakim ambaye amesema:

”Swahiyh kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy na Muslim.”

adh-Dhahabiy ameafikiana naye, mambo ni kama alivosema. Vilevile at-Tirmidhiy ameipokea kwa kifupi ambaye pia ameisahihisha. Muslim na wengineo wameipokea kutoka humo ruhusa ya matembezi peke yake, kama ilivyotangulia katika suala  la 118, uk. 178 Hadiyth ya kwanza.

an-Nawawiy amesema alipokuwa akitoa maelezo ya Hadiyth ya kwanza ya Abu Hurayrah:

”Ndani yake kuna kufaa kuwatembelea washirikina katika uhai wao na makaburi yao baada ya kufa kwao, kwa sababu ikiwa kuwazuru baada ya kufa kunajuzu, basi kuwazuru katika uhai wao ni jambo lina haki zaidi.

Vilevile ndani yake kuna makatazo ya kuwaombea msamaha makafiri. ´Iyaadhw amesema: ”Sababu ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutembelea kaburi lake ni kwamba alikusudia kuimarisha mazingatio na ukumbusho kwa kuliona kaburi lake. Hili linaungwa mkono na maneno yake (Swalla Allaahu ́alayhi wa sallam):

“Yatembeleeni makaburi, kwani hakika yanakukumbusheni mauti.”

  • Muhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 237-239
  • Imechapishwa: 06/08/2026