Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Madhehebu ya Salaf yako kati ya ukanushaji na kufananisha. Kwa maana nyingine ni kwamba hawazifananishi sifa za Allaah na sifa za viumbe Wake kama ambavyo hawafananishi dhati Yake kwa dhati za viumbe Wake. Wala hawamkanushii yale aliyojisifia Mwenyewe na akasifiwa na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hawayakanushi majina mazuri ya Allaah na sifa Zake kuu, hawapotoshi maneno kuyaondoa mahali pake stahiki na wakayaharibu majina ya Allaah na Aayah Zake.

MAELEZO

Madhehebu ya Salaf yako kati na kati. Wako kati na kati ya wakanushaji ambao ni madhehebu ya wakanushaji katika Jahmiyyah, Mu´tazilah na Ashaa´irah ambao wamepitiliza katika kutakasa mpaka wakamkanushia Allaah yale majina na sifa Alizojithibitishia Mwenyewe kwa sababu eti ya kukimbia kufananisha, na kati na kati ya wafananishaji ambao wamepitiliza katika kuthibitisha majina na sifa, wakazifananisha sifa za Allaah na sifa za viumbe Wake. Wakanushaji wamepitiliza katika kutakasa, wafananishaji wamepitiliza katika kuthibitisha. Ama Ahl-us-Sunnah wakawa wastani. Wakamthibitishia Allaah majina na sifa kinyume na wakanushaji, na wakamkanushia kufanana na viumbe kinyume na wafananishaji na washabihishaji. Hivyo wao ni watu wa kati na kati – na himdi zote njema ni za Allaah. Wamesalimika na maafa mawili; ukanushaji na ufananishaji.

Huu ndio msingi kwamba daima ´Aqiydah ya Salaf ni ya kati na kati:

وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَاكُمْ أُمَّةً وَسَطًا

”Namna hiyo ndivyo hivyo Tumekufanyeni ummah kati na kati na adilifu.”[1]

Kama ummah huu ulivyo wa kati na kati baina ya mataifa, basi Ahl-us-Sunnah wako kati na kati baina ya makundi yaliyopotea.

Kinyume na wafananishaji na washabihishaji. Kwani kumfananisha Muumba na kiumbe ni upungufu katika haki ya Allaah. Wala hawapitilizi katika kutakasa mpaka wakakanusha yale majina na sifa Alizojithibitishia Mwenyewe.

Kupotoa kunamaanishwa kupotoka kutoka katika haki. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَلِلّهِ الأَسْمَاء الْحُسْنَى فَادْعُوهُ بِهَا وَذَرُواْ الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَآئِهِ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُواْ يَعْمَلُونَ

”Allaah ana majina mazuri mno; hivyo basi muombeni kwayo na waacheni wale wanaopotoa katika majina Yake. Watalipwa yale waliokuwa wakifanya.”[2]

Wanaopotoka ima kwa kuyakanusha na kuyakengeusha au kwa kuyafanyia namna na kuyafananisha. Haki ni kuyathibitisha kama yalivyokuja na kutokana na vile yanavyojulisha.

[1] 2:143

[2] 7:180

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 213-214
  • Imechapishwa: 10/07/2026