123. Dalili ya nne kufaa kwa mwanamke kuyatembelea makaburi

4 – Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kumkubalia kwake mwanamke aliyemuona kaburini. Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipita kando ya mwanamke kaburini na huku alikuwa analia ambapo akamwambia: ”Mche Allaah na kuwa na subira… ”

Ameipokea al-Bukhaariy na wengineo. Tayari imekwishatangulia kwa ukamilifu wake katika masuala ya 19, uk. 22. Ameiwekea kichwa cha khabari ”Mlango unaozungumzia kuyatembelea makaburi.” Haafidhw amesema katika ”al-Fath”:

”Dalili ya ruhusa hapa ni kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumkemea mwanamke huyo kwa kukaa kwake karibu na kaburi. Kulikubali kwake jambo ni hoja.”

al-‘Ayniy amesema katika ”al-‘Umdah” (3/76):

“Ndani yake kuna ruhusa ya kuyatembelea makaburi kwa ujumla, ni mamoja anayefanya hivo awe ni mwanamume au mwanamke, ni mamoja anayetembelewa ni muislamu au kafiri, kwa sababu hakukutolewa upambanuzi juu ya hilo.”

Haafidhw pia ametaja maneno yenye maana kama hiyo mwishoni mwa maelezo yake juu ya Hadiyth hiyo ambapo akasema baada ya kusema ”… kwa sababu hakukutolewa upambanuzi juu ya hilo”:

”an-Nawawiy amesema: ”Kikosi kikubwa cha wanazuoni wamesema kwa kukata kabisa ya kwamba inafaa.” Mtunzi wa ”al-Haawiy” amesema: ”Haijuzu kuzuru kaburi la kafiri”, jambo ambalo ni kosa.”[1]

Yale yanayofahamishwa na Hadiyth kuhusu ruhusa ya mwanamke kuyatembelea makaburi ndiyo yanayodhihirika kwa uwazi kutoka ndani ya Hadiyth hiyo. Haya hivyo hali hiyo itakuwa kamili ikiwa tukio hilo halikutokea kabla ya katazo, jambo ambalo ndio dhahiri endapo tutakumbuka tulivyotangulia kusema kuwa katazo lilikuwa Makkah na kwamba tukio hili limepokelewa na Anas ambaye ni mkazi wa Madiynah ambaye aliletwa na mama yake Umm Sulaym kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofika Madiynah. Kipindi hicho Anas alikuwa na umri wa miaka kumi. Basi tukio hili lilitokea Madiynah na hivyo imethibiti ya kwamba ni baada ya katazo. Kwa hiyo imesimama hoja ya ruhusa.

Kuhusu maneno ya Ibn-ul-Qayyim katika ”Tahdhiyb-us-Sunan” (4/350):

“Kumcha Allaah ni kutekeleza aliyoamrisha na kuacha aliyoyakataza na miongoni mwa hayo ni katazo la matembezi.”

Ni sahihi iwapo mwanamke huyo alikuwa na elimu ya kwamba wanawake wamekatazwa kuyatembelea na kwamba katazo hilo halikufutwa. Hapo ndipo maneno yake:

”… miongoni mwa hayo ni katazo la matembezi.”

yangekuwa sahihi. Lakini kwa kuwa hili halijulikani kwetu, basi hoja hiyo si sahihi. Hilo linatiliwa mkazo kwamba lau katazo lingekuwa bado lipo, basi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angemkataza moja kwa moja mwanamke huyo kufanya matembezi na kumbainishia hilo. Kwa maana nyingine ni kwamba asingelitosheka tu kwa kumwambia “Mche Allaah” kwa namna ya jumla, jambo ambalo liko wazi – Allaah (Ta´ala) akitaka.

[1] Dalili ya hilo ipo katika suala linalofuata.  Mtunzi wa ”al-Haawiy” ni Abul-Hasan al-Mawardiy, ambaye alifariki 450.

  • Muhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 233-235
  • Imechapishwa: 04/08/2026