Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

98 –Tunawaita wale wanaoswali kuelekea Qiblah kuwa ni ”waislamu” na ”waumini”, muda wa kuwa wanatambua yale yaliyokuja kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wanasadikisha yale yote aliyoyasema na kuyaeleza.

MAELEZO

Haya ni katika ´Aqiydah. Yule mwenye kutamka shahaadah na akawa na msimamo juu yake ya kwamba ni muislamu ijapo atafanya baadhi ya maasi na kutenda madhambi makubwa. Kwa msemo mwingine midhali madhambi yao ni chini ya shirki. Lakini muislamu kama huyo anazingatiwa ni mwenye Uislamu na imani pungufu na pia ni fasiki. Hata hivyo hahukumiwi kuwa ni kufuru ikiwa madhambi yake ni chini ya shirki. Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Hawamkafirishi yeyote mwenye madhambi chini ya shirki. Lakini hata hivyo yanapunguza imani ya mtu huyo na mwenye nayo anakuwa fasiki pasi na kutoka nje ya dini.

Khawaarij wanaonelea kinyume. Wanaona kuwa mtenda dhambi kubwa ni kafiri na anatoka nje ya dini. Aidha wanaona kuwa watu hao watadumishwa Motoni milele.

Mu´tazilah pia wanaonelea kinyume. Wao pia wanaona kuwa mtenda dhambi kubwa anatoka nje ya Uislamu, lakini hawamwingizi ndani ya ukafiri. Badala yake wanaona kuwa yuko kati ya ngazi ya Uislamu na ukafiri. Lakini mtu huyo akifa katika hali hiyo ya madhambi, wanaamini kama Mu´tazilah na Khawaarij, ya kwamba atadumishwa Motoni milele.

Murji-ah pia wanaonelea kinyume. Murji-ah wanaona kuwa imani haidhuriki kwa maasi. Wanaona kuwa ambaye anamsadikisha Allaah (´Azza wa Jall) basi huyo anakuwa muumini pasi na kujali yale atakayoyafanya –hata kama ataacha nguzo zote za imani. Kwa mtazamo wao wanaona kuwa jambo la muhimu ni kusadikisha na kuamini. Kuhusu matendo hayaizidishi imani wala kuipunguza kwa sababu matendo sio katika imani. Wanaona kuwa ni muumini mwenye imani kamili muda wa kuwa mtu huyo anasadikisha. Hii ndio ´Aqiydah ya Murji-ah ambayo ni wazi kabisa kuwa ni potofu.

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 131-132
  • Imechapishwa: 12/11/2024