123. Sunnah inachukua nafasi ya mbele kabla ya elimu za kisasa

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amesema:

”… muda wa kuwa wanatambua yale yaliyokuja kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wanasadikisha yale yote aliyoyasema na kuyaeleza.”

Lakini wakipinga kitu katika yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi wanakuwa makafiri. Haijalishi kitu hata kama wataamini sehemu ya yale aliyokuja nayo; yule mwenye kukanusha kitu basi ameyakufuru yote aliyokuja nayo. Kwa msemo mwingine ni lazima kuyaamini yote, pasi na kujali yameafikiana au yameenda kinyume  na matamanio ya mtu, kwa sababu yote ni haki.

Yule mwenye kupinga baadhi tu ya Hadiyth Swahiyh ni kafiri. Mfano wa mtu huyo ni kama ambaye anapinga Hadiyth Swahiyh zilizopokelewa na al-Bukhaariy na akasema kuwa yeye haiamini wala kuisadikisha Hadiythhiyo kwa sababu inapingana na elimu ya kisasa. Hivi kweli maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yanatuhumiwa na maneno ya mtu wa kawaida hayatuhumiwi? Jengine ni kwamba elimu ya kisasa wakati mwingine inaafikiana na Hadiyth ambayo ni Swahiyh. Kwa mfano Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Nzi anapoingia ndani ya kinywaji cha mmoja wenu, basi amzamishe kisha amuopoe. Kwani katika moja ya mbawa zake kuna ugonjwa na katika mbawa nyingine kuna tiba.”[1]

Elimu ya kisasa inathibitisha jambo hili. Lakini kwa vile Hadiyth inapingana na ladha ya wajinga hawa, ndipo wakaitia mdomoni. Huu ni ukafiri. Wana maneno mabaya juu ya Sunnah. Wanairudisha na kueneza mashaka juu yake. Aidha wanajengea hoja maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposema:

“Nyinyi ni wajuzi zaidi juu ya mambo ya dunia yenu.”[2]

Wanasema namna hii ilihali wanadai kuwa wanalingania katika Uislamu. Huu ndio msimamo wao juu ya Sunnah zake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wajinga hawa wanasema kuwa jambo hilo ni katika mambo ya kidunia na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekwishasema:

“Nyinyi ni wajuzi zaidi juu ya mambo ya dunia yenu.”

Hiyo maana yake ni kwamba wanamtia ujingani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Zingatia maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah) aliposema:

”… muda wa kuwa wanatambua yale yaliyokuja kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wanasadikisha yale yote aliyoyasema na kuyaeleza.”

Haitoshi kutambua na kusadikisha. Isipokuwa tu Murji-ah ndio wanaona hivo. Bali pamoja na hilo ni lazima kutendea kazi yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hali ya kuwa mkweli katika jambo hilo.

[1] al-Bukhaariy (3142) na Abu Daawuud (3844).

[2] Muslim (2363).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 132-134
  • Imechapishwa: 12/11/2024