12. Washirikina walikuwa wakimuomba Allaah usiku na mchana

kama walivyokuwa wakimuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) usiku na mchana.

MAELEZO

Hili ni jambo la pili la washirikina. Kama ambavyo walikuwa wakiitambua Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah walikuwa pia wakimuabudu Allaah. Walikuwa wakimuomba, wakihiji katika Ka´bah, wakifanya ´Umrah, wakitoa swadaqah na wakimuabudu Allaah kwa aina mbalimbali za ´ibaadah. Lakini wakizichanganya pamoja na shirki kwa kuwa walikuwa wakimuabudu Allaah na wakiwaabudu wengine. Haya hayatowafaa kitu kwa kuwa shirki inabatilisha ´ibaadah zao. ´Ibaadah haisihi isipokuwa kwa kumtekelezea Allaah pekee. Kwa ajili hii anasema (Jalla wa ´Alaa):

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote.” (04:36)

قُلْ إِنَّمَا أَنَا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُوحَىٰ إِلَيَّ أَنَّمَا إِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا

”Sema: “Hakika mimi ni mtu kama nyinyi ninayefunuliwa Wahy ya kwamba mungu wenu ni Mmoja pekee. Hivyo basi yule anayetaraji kukutana na Mola wake na atende matendo mema na wala asishirikishe katika ‘ibaadah za Mola wake yeyote.”” (18:110)

Hakuishilia tu kusema:

“… afanya matendo mema.”

Ni lazima ajiepushe na shirki. Ikiwa hajiepushi na shirki, hata kama atafanya matendo mengi, yanabatilika na yanabatilika na hayanufaishi kitu. Kuna ´ibaadah ambazo washirikina walikuwa wakimfanyia Allaah (´Azza wa Jall) ambazo zilikuwa ni katika mabaki ya dini ya Ibraahiym (´alayhis-Salaam) kipenzi wa hali ya juu wa Allaah. Mwanzoni walikuwa katika dini ya Ibraahiym. Lakini alipokuja ´Amr bin Luhayy al-Khuzaa´iy ndiye akaibadilisha dini na akawaingizia ndani yake shirki. Lakini walibaki na chembechembe za dini ya Ibraahiym hata kama walikuwa washirikina. Walikuwa wakimuomba Allaah na khaswa pale wanapotumbukia katika shida. Katika hali hiyo wanamtakasia Allaah (´Azza wa Jall) maombi na wakati huo wanaacha kuyaomba masanamu kwa kuwa [wanatambua] hayasaidii kitu katika wakati huu na hayawaokoi katika kipindi cha shida. Amesema (Subhaanah):

وَإِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فِي الْبَحْرِ ضَلَّ مَن تَدْعُونَ إِلَّا إِيَّاهُ ۖ فَلَمَّا نَجَّاكُمْ إِلَى الْبَرِّ أَعْرَضْتُمْ ۚ وَكَانَ الْإِنسَانُ كَفُورًا

“Inapokuguseni dhara baharini hupotea wale mnaowaomba isipokuwa Yeye pekee. Anapokuokoeni katika nchi kavu mnakengeuka. Hakika mwanadamu daima ni mwingi wa kukufuru.” (17:67)

وَإِذَا غَشِيَهُم مَّوْجٌ كَالظُّلَلِ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ فَمِنْهُم مُّقْتَصِدٌ ۚ وَمَا يَجْحَدُ بِآيَاتِنَا إِلَّا كُلُّ خَتَّارٍ كَفُورٍ

”Yanapowafunika mawimbi kama vivuli humuomba Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini. Anapowaokoa katika nchi kavu, basi miongoni mwao wapo wanaoshika mwendo wa wastani. Hawazikanushi alama Zetu isipokuwa kila khaini mkubwa, mwingi wa kukufuru.” (31:32)

Kwa hiyo ´ibaadah ikichanganyika na shirki inabatilika.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 24
  • Imechapishwa: 09/10/2016