12. Wajibu mkubwa kabisa na makatazo makubwa kabisa

Kubwa aliloamrisha Allaah ni Tawhiyd. Tawhiyd maana yake ni kumpwekesha Allaah katika ´ibaadah. Ina maana kwamba unatakiwa kumuabudu Allaah peke yake pasi na wengine wote. Usimuabudu pamoja Naye si sanamu, Mtume, Malaika, jiwe, jini wala kitu kingine. Allaah (Subhaanah) amesema:

وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Lau wangemshirikisha yangebatilika yale waliyokuwa wakitenda.” (06:88)

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Hakika umefunuliwa Wahy wewe na kwa wale walio kabla yako ya kwamba ukifanya shirki bila shaka yatabatilika matendo yako na utakuwa miongoni mwa waliokhasirika.” (39:65)

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa:

“Ni dhambi ipi kubwa?” Akasema: “Ni kumfanyia Allaah mwenza ilihali Yeye ndiye kakuumba.” Kukasemwa: “Kisha ipi?” Akasema: “Kumuua mwanao kwa kuchelea asije kula na wewe.” Kukasemwa: “Halafu ipi?” Akasema: “Kuzini na mke wa jirani yako.” al-Bukhaariy (447) na Muslim (86). al-Bukhaariy (447) na Muslim (86).

Akabainisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba shirki ndio dhambi kubwa, mbaya na khatari zaidi. Katika Hadiyth nyingine amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nisikuelezeni dhambi kubwa kabisa?” Wakasema: “Ndio, ee Mtume wa Allaah.” Akasema: “Ni kumshirikisha Allaah.” al-Bukhaariy (5976) na Muslim (87).

Tawhiyd ni kumpwekesha Allaah katika ´ibaadah.

Shirki ni kumuomba mwingine asiyekuwa Allaah, kumkhofu mwingine asiyekuwa Allaah, kutaraji kwa mwingine asiyekuwa Allaah, kuchinja kwa ajili ya mwingine asiyekuwa Allaah, kumuwekea nadhiri mwingine asiyekuwa Allaah au kumtekelezea aina zengine za ´ibaadah asiyekuwa Allaah. Yote haya ni shirki kubwa. Ni mamoja yule mwenye kuombwa akawa ni Mtume, Malaika, jini, mti, jiwe au kitu kingine. Kwa ajili hiyo Allaah (Ta´ala) amesema:

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe Yeye na chochote.” (04:36)

Neno “chochote” limetajwa kwa fomu ya uhakika katika mazingira ya kukataza na hivyo inahusu kila kitu. Allaah (Subhaanah) amesema:

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamuabudu Allaah kwa kumtakasia Yeye dini.” (98:05)

Kubwa aliloamrisha Allaah ni Tawhiyd, nayo ni kumpwekesha Allaah katika ´ibaadah, na kubwa aliloharamisha Allaah ni shirki, nako ni kumshirikisha Allaah (´Azza wa Jall). Kwa ajili hii inatokea mara nyingi Allaah (Subhanaahu wa Ta´ala) anaamrisha Tawhiyd na kukataza shirki katika Kitabu Chake.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 19-20
  • Imechapishwa: 15/10/2016