79 – Yuusuf bin Muusa na wengine wametuhadithia: Jariyr ametuhadithia, kutoka kwa Qaabuus, kutoka kwa baba yake aliyesema:

”Nilikutana na Jariyr bin ´Abdillaah alipokuwa anarudi kutoka Shaam, akanitembeza kisha akasema: ”Nilifika mara moja kwenye mti ambapo chini yake kulikuwa mtu kasimama chini ya kivuli cha mkeka wake, jua likamzidi mkeka, basi nikamuwekea sawa juu yake. Kisha mtu huyo alipoamka, nikagundua kuwa ni Salmaan al-Faarisiy. Nikamweleza nilichofanya, akaniambia: “Ee Jariyr, jinyenyekeze kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall) katika dunia, kwani anayejinyenyekeza kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall) duniani, basi Allaah humuinua siku ya Qiyaamah. Ee Jariyr, je unajua nini maana ya giza la Moto siku ya Qiyaamah?” Nikasema: ”Hapana.” Akasema: “Ni dhuluma ya baadhi ya watu kwa wengine katika dunia.”

80 – ´Aliy bin al-Ja´d ametuhadithia, kutoka kwa Mis´ar, kutoka kwa Sa´iyd bin Abiy Burdah, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa al-Aswad, kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa), ambaye ameeleza:

“Hakika nyinyi mnaghafilika ´ibaadah bora zaidi – nayo ni kunyenyekea.”

81 – ´Abdur-Rahmaan bin Yuunus ametuhadithia: Sufyaan ametuhadithia, kutoka kwa ´Amr, kutoka kwa Yahyaa bin Ja´dah, aliyesema:

“Alikuja mtu mweusi mwenye kovu la ndui na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anakula, basi kila alipoketi karibu na mtu mtu huyo aliondoka pembeni mwake, lakini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamketisha karibu naye.”[1]

82 – Imekuja ndani ya kitabu cha baba yangu kwa hati yake ya mkono: Jariyr ametukhabarisha, kutoka kwa Mansuur, kutoka kwa Ibraahiym, ambaye amesema:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa na baadhi ya Maswahabah wake ndani ya nyumba wanakula. Tahamaki akaja ombaomba mlangoni akiwa na ulemavu unaochukiza. Akapewa idhini ya kuingia ndani. Alipoingia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamketisha juu ya paja lake, kisha akasema: ”Kula.” Na alikuwa mtu mmoja wa Quraysh alichukizwa naye na akamchukia. Basi bwana yule hakufa isipokuwa naye alipatwa na ugonjwa huyo ambao ulikuwa ukimchukiza.”[2]

83 – Muhammad bin Haatim na wengine wamenihadithia: Yuunus bin Muhammad al-Mu´allim ametuhadithia, kutoka kwa al-Mufadhdhwal bin Fadhwaalah, kutoka kwa Habiyb bin ash-Shahiyd, kutoka kwa Muhammad bin al-Munkadir, kutoka kwa Jaabir bin ´Abdillaah, aliyesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alishika mkono wa mtu mwenye ukoma, akauingiza pamoja na wake kwenye sahani na kusema: ”Kula kwa jina la Allaah, ukiwa na unamwamini kwa Allaah na kumtegemea Allaah.”[3]

84 – ´Abdur-Rahmaan bin Swaalih amenihadithia: Abun-Nadhwr ametuhadithia, kutoka kwa al-Mas´uudiy, kutoka kwa ´Awn bin ´Abdillaah, ambaye amesema:

”Ilikuwa inasemwa kwamba anayekuwa katika sura nzuri, yuko katika nafasi isiyomdhalilisha, akapewa wasaa wa riziki kisha akanyenyekea kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall), basi huyo ni miongoni mwa wateule wa Allaah (´Azza wa Jall).”

85 – Ishaaq bin Ismaa´iyl ametuhadithia: Jariyr ametuhadithia, kutoka kwa ´Atwaa’ bin as-Saa-ib, kutoka kwa ash-Sha´biy, ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mola wangu alinitaka nichague kati ya mambo mawili: kuwa mja na Mtume au kuwa mfalme na Nabii. Sikumjua ni lipi nichague. Nilikuwa na rafiki yangu katika Malaika Jibriyl. Nikainua kichwa changu ambapo akasema: ”Nyenekea kwa Mola wako.” Nikasema: ”Mja na Mtume.”[4]

[1] al-´Iraaqiy amesema:

”Siwezi kupata tamko hili. Kinachojulikana ni kwamba yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikula pamoja na watu wenye ukoma.” (Takhriyj-ul-Ihyaa’ (3/340))

[2] al-´Iraaqiy amesema:

”Siwezi kupata asili ya tamko hili. Kinachojulikana ni kwamba yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikula pamoja na watu wenye ukoma.” (Takhriyj-ul-Ihyaa’ (3/340))

[3] at-Tirmidhiy (1817), ambaye amesema kuwa ni ngeni. Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan at-Tirmidhiy” (1817).

[4] Ahmad (2/231) na Ibn Hibbaan (2137). Wote wawili wameipokea kupitia kwa Muhammad bin Fudhwayl, kutoka kwa ´Amaarah bin al-Qa´qaa´, kutoka kwa Abu Zur´ah, kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”as-Swahiyhah” (¾).

  • Muhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa (afk. 281)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Khumuul wat-Tawaadhwu´, uk. 105-115
  • Imechapishwa: 29/01/2026