Epuke kuelekea Qiblah wakati wa kukidhi haja ukiweza

Swali: Je, kuelekea Qiblah wakati wa kujisaidia haja ndogo au haja kubwa kunajuzu ndani ya jengo? Ni ipi dalili ya hilo ikiwa kunajuzu?

Jibu: Lililopasa ni kutoelekea Qiblah wala kuipa mgongo, si ndani ya jengo wala nje yake. Kwa sababu katika Hadiyth zilikataza jambo hilo zimetaja kwa jumla. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikataza kuelekea Qiblah au kuipa mgongo wakati wa haja ndogo na haja kubwa. Hivyo inampasa muumini asielekee wala asiipe mgongo, ni mamoja ndani ya jengo wala jangwani. Lakini ndani ya jengo ni jambo lililo rahisi zaidi. Jopo la wanazuoni wameonelea kufaa kufanya hivo akiwemo al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah) na wengine. Wamejengea dalili kwa Hadiyth ya Ibn ´Umar katika ”as-Swahiyh” mbili ya kwamba alimwona Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akitua haja juu ya matofali mawili katika nyumba ya Hafswah akikielekea Shaam na akiipa mgongo Ka´bah. Wakasema kwamba hilo linafahamisha kujuzu katika jengo, baina ya kuta. Ama jangwani, hapana. Wengine miongoni mwa wanazuoni wamesema kuwa katazo ni lenye kuenea, katika jangwa na jengo na kwamba pengine kitendo alichokifanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndani ya nyumba ya Hafswah kilikuwa kabla ya katazo au kilikuwa maalum kwake. Kwa hiyo kilicho bora kwa muumini kujihadhari na kutoelekea ikiwa inawezekana, si katika jangwa wala katika jengo kwa sababu ya kufuata kuenea kwa Hadiyth, kutoka katika makinzano ya wanazuoni na kuchukua tahadhari ya dini.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1082/حكم-استقبال-القبلة-او-استدبارها-عند-قضاء-الحاجة
  • Imechapishwa: 29/01/2026