12. Umuhimu wa elimu ya misingi na kanuni inapokuja katika sifa za Muumba

Hapana shaka yoyote kwamba kule kuwa na utambuzi kuhusu kanuni, misingi na vigezo ni miongoni mwa elimu muhimu na zenye manufaa zaidi. Kwa sababu “misingi na kanuni ni sawa na msingi wa jengo na mzizi wa mti –  hayawezi kusimama isipokuwa kwayo. Matawi hukua kutoka kwenye mizizi ilihali mizizi inakuwa imara na kuimarisha matawi. Kwa kanuni na misingi elimu inakuwa imara na nguvu na kukua. Kupitia yenyewe ndio kunatambulika  chanzo cha misingi na upambanuzi kati ya maswali mengi yanayotatiza. Isitoshe hukusanya mlinganisho na mfanano ambavyo ni vitu vizuri ambavyo elimu inaweza kukusanywa”[1]. Aidha zipo faida nyingi na manufaa mengi ambayo hayadhibitiwi. Bali ”miongoni mwa uzuri wa Shari´ah, ukamilifu wake na utukufu wake ni kwamba hukumu zake za kimsingi na zenye matawi, ´ibaadah, miamala yake na mengineyo vyote hutegemea misingi na kanuni zinazosimamia hukumu yake, zinazokusanya zile nyanja zake zilizotawanyika, zinazoeneza matawi yake na kuirejesha katika misingi yake”[2].

Kanuni ni jambo lililoenea linalotumika kwa mambo mengi ambapo hukumu zake zinafahamika kutoka humo[3]. Wakati kanuni inadhibitiwa na msingi ukaeleweka, basi inawezekana kutambua masuala mengine mengi ambayo yanafanana na matawi ya kanuni hii. Isitoshe inakuwa rahisi kujilinda dhidi ya masuala ambayo pengine yakawa na mkanganyiko. Aidha inakuwa rahisi kuelewa, kuihifadhi na kuidhibiti elimu. Kutokana na hali hii maneno yanakuwa yamejengeka juu ya elimu thabiti, uadilifu na inswafu. Kwa ajili hiyo Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Ili mtu aweze kuzungumza kwa elimu na uadilifu ni lazima awe na misingi yenye kuenea ambayo anarejesha pambanuzi. Isitoshe ni lazima atambue pambanuzi  na ni vipi zimejitokeza ili asibaki katika uwongo na ujinga katika yale mambo ya pambanuzi pamoja na ujinga na dhuluma katika yale mambo ya misingi na hivyo ikasababisha maharibifu makubwa.”[4]

Kutokana na sababu hiyo ndio wanazuoni wakatilia bidii kuweka misingi na kuikusanya katika masomo mbalimbali. Unakaribia kutopata somo lolote ambalo halina kanuni na misingi inayokusanya matawi yake, kubainisha yale mambo yake yanayotatiza, kuangazia miale yake na kurahisisha ufahamu, uhifadhi na udhibiti wake[5]. Licha ya ufupi  wake inaweza kunufaisha na kufaidisha zaidi kuliko yale yanayopatikana katika maneno marefu[6]. Hivyo basi kule kutilia bidii kanuni na misingi, ambayo imepokelewa kutoka kwa Salaf (Rahimahumu Allaah), hupelekea faida na manufaa ambayo hakuna ayajuaye isipokuwa Allaah pekee. Kwa sababu mambo hayo, ni kama inavosemwa, ni kuweka nukta juu ya herufi. Isitoshe ni mambo yanayoweka mambo wazi, kuondosha yale mambo yanayotatiza, kujilinda dhidi ya mkanganyiko na mengi mengine.

[1] Twariyq-ul-Wusuul, uk. 4, ya as-Sa´diy.

[2] ar-Riyaadhw an-Naadhwirah, uk. 243, ya as-Sa´diy.

[3] Tazama ”Sharh-ul-Kawkab al-Munayyir”, uk. 6, ya al-Fatuuhiy.

[4] Majmuu´-ul-Fataawaa (19/203).

[5] Tazama dibaji ya “Faa-idah Jaliylah fiy Qawaa´id-il-Asmaa’ al-Husnaa”, ambayo imenukuliwa kutoka katika “Badaa-i´-ul-Fawaa-id” ya Ibn-ul-Qayyim kwa ukaguzi wangu.

[6] Taysiyr-ul-Kariym (3/5) ya as-Sa´diy.

  • Muhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Allaamah ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad al-Badr
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Athar al-Mash-huur ´an-il-Imaam Maalik fiy Swifat-il-Istiwaa’, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 28/11/2025