12. Shikamana na Sunnah na jiepusha na Ahl-ul-Bid´ah wal-Furqah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

يَوْمَ تَبْيَضُّ وُجُوهٌ وَتَسْوَدُّ وُجُوهٌ ۚ فَأَمَّا الَّذِينَ اسْوَدَّتْ وُجُوهُهُمْ أَكَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنتُمْ تَكْفُرُونَ

“Siku [baadhi ya] nyuso zitang´ara na [nyingine] zitafifia. Basi wale ambao nyuso zao zitafifia [wataambiwa:] “Je, mlikufuru baada ya kuamini kwenu? Basi onjeni adhabu kwa yale mliyokuwa mkikufuru.” (03:106)

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Wale walioshikamana na Sunnah na kuungana ndio nyuso zao zitang´ara na wale walioshikamana na Bid´ah na tofauti ndio nyuso zao zitafifia.”[1]

´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ummah wangu utafikwa na yale yaliyowafika wana wa israaiyl kiasi cha kwamba, ikiwa kuna katika wao aliyemwingilia mama yake hadharani basi kutapatikana katika Ummah wangu ambaye atafanya vivyo hivyo. Hakika wana wa israaiyl walifarikiana katika makundi sabini na mbili na Ummah wangu utafarikiana katika makundi sabini na tatu; yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni lipi hilo?” Akasema: “Ni lile linalofuata yale mimi na Maswahabah zangu tunayofuata.”[2]

Muumini ambaye anataraji kukutana na Allaah azingatie maneno ya mkweli na msadikishwaji na khaswa pale aliposema:

“Ni lile linalofuata yale mimi na Maswahabah zangu tunayofuata.”

Ni mawaidha yaliyoje lau yatazifikia nyoyo zilizo hai!”

Ameipokea at-Tirmidhiy.

MAELEZO

Ni lile linalofuata yale mimi… – Bi manaa lile litalolazimiana na haki kuwa na msimamo juu ya yale waliyoyaashiria Maswahabah na wale waliowafuata kwa wema. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Sabini na mbili yote yataingia Motoni.”

Mtu anatakiwa kujiepusha na maoni ya Ahl-ul-Bid´ah wal-Furqah na watu wa tofauti:

”Sabini na mbili yote yataingia Motoni.”

Miongoni mwa hao wako ambao ni wahalifu, wazushi na watenda maasi. Lakini Ahl-us-Sunnah ndio wale ambao wamefuata mfumo wa Maswahabah na wakawa na msimamo juu ya dini. Hawa ndio ambao wataokoka. Kuhusu makundi mengine yako ambayo ni makafiri, wazushi na walioenda kinyume na Shari´ah kwa sababu hawakushikamana na haki.

[1] Ibn Abiy Haatim (3/729), al-Khatwiyb al-Baghdaadiy katika ”Taariykh Baghdaad” (7/379) na al-Laalakaa’iy katika ”Sharh Usuwl I´tiqaad Ahl-is-Sunnah wal-Jama´ah” (1/72).

[2] at-Tirmidhiy (2641).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Fadhwl-il-Islaam, uk. 21-22
  • Imechapishwa: 25/10/2020