Mifumo ya watu juu ya maandiko haya yanayotatiza imegawanyika katika sampuli mbili:

1 – Mfumo wa wale waliobobea katika elimu ambao wameamini yale maandiko yaliyo wazi na yasiyokuwa wazi na wakasema:

كُلٌّ مِّنْ عِندِ رَبِّنَا

“Zote ni kutoka kwa Mola wetu.”[1]

Sambamba na hayo wakaacha kuingia sana kwa undani katika yale ambayo hawawezi kuyafikia wala kuyazunguka kiujuzi. Wamefanya hivo kwa ajili ya kumtukuza Allaah na Mtume Wake na kushika adabu na maandiko ya Shari´ah. Nao ni wale ambao Allaah amewasifu pale aliposema:

وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ يَقُولُونَ آمَنَّا بِهِ كُلٌّ مِّنْ عِندِ رَبِّنَا

“Na wale wenye msingi madhubuti katika elimu husema: “Tumeziamini, zote ni kutoka kwa Mola wetu.””[2]

2 – Mfumo wa wapotofu ambao wanafuata maandiko yasiyokuwa wazi kwa ajili ya kutafuta fitina na kuwazuia watu kutokana na dini yao na mfumo wa wema waliotangulia. Hivyo wakajaribu kupindisha maana ya maandiko haya yasiyokuwa wazi kwa mujibu wa vile wanavyotaka wao na si kwa mujibu wa vile anavotaka Allaah na Mtume Wake. Aidha wakafanya maandiko ya Qur-aan na Sunnah kugongana na wakajaribu kutukana majulisho yake kwa mgongano na upungufu kwa ajili ya kutaka kuwatia mashaka waislamu juu ya majulisho yake na kuwapofosha kutokana na uongofu wake. Hawa ndio waliosimangwa na Allaah pale aliposema:

فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ ۗ وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّـهُ

”Basi wale ambao katika nyoyo zao mna upotevu hufuata zile zisizokuwa wazi ili kutafuta fitina na kutafuta kuzipotosha – na hakuna ajuae uhakika Wake isipokuwa Allaah.”[3]

[1] 03:07

[2] 03:07

[3] 03:07

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 33
  • Imechapishwa: 11/10/2022