Miongoni mwa sababu zinazofanya familia kuwa na furaha ni wanafamilia wote kusaidiana katika kheri. Mume na mke wapupie juu ya hilo. Wazazi wawili wanatakiwa kuwalea watoto wao juu ya kusaidiana katika kheri. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ

“Saidianeni katika wema na uchaji Allaah.” 05:02

Nyumbani kukipatikana kusaidizana katika kheri basi hupatikana raha na furaha. Zingatieni pamoja nami jambo aliloelekeza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ndani ya jambo hilo mna ladha kubwa kabisa miongoni mwa ladha za duniani. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah amrehemu mwanaume aliyeamka usiku akaswali na akamuamsha mke wake na yeye akaswali. Endapo atakataa amnyunyizie usoni mwake maji. Allaah amrehemu mwanamke aliyeamka usiku akaswali na akamuamsha mume wake na yeye akaswali. Endapo atakataa amnyunyizie usoni mwake maji.” Abu Daawuud (1308), an-Nasaa´iy (1610), Ibn Maajah (1336), Ibn Khuzaymah (02/1148), Ibn Hibbaan (06/2567), al-Haakim (01/1164), Ahmad (02/250). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Haakim juu ya masharti ya Muslim. Mlolongo wa wapokezi wake ni mzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Abiy Daawuud (05/1181).

Ni uzuri uliyoje wa kusaidiana katika kheri! Mume anaamka na kuswali usiku. Hamnyimi mke wake kheri hii. Bali anamuamsha. Iwapo atakataa anachukua maji na kumnyunyizia usoni mwake ili aweze kuamka. Vivyo hivyo mke anaamka usiku na kuswali. Halafu anamuamsha mume wake. Iwapo atakataa anachukua maji na kumpaka usoni mwake. Familia iliyojengwa juu ya kusaidiana katika kheri ndio hufurahi kwa jambo kama hili. Ikiwa sio familia iliyojengwa juu ya kusaidiana katika kheri anaweza kuripuka kama inavyoripuka volikano. Matokeo yake hakutopatikana furaha.

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliymillaah ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Asbaab sa´aadat-il-Usrah, uk. 40-41
  • Imechapishwa: 09/10/2016