Inampasa mwalimu awape nasaha. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Dini ni kupeana nasaha.” Wakasema: ”Kwa nani, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: ”Kwa Allaah, na Kitabu Chake, Mtume Wake na kwa viongozi wa waislamu na watu wao wa kawaida.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Miongoni mwa nasaha kwa Allaah na kwa Kitabu Chake ni kumheshimu msomaji wake na mwanafunzi wake, kumwelekeza katika manufaa yake, kumfanyia upole, kumsaidia katika kuitafuta kwa kadiri iwezekanavyo, kuleta mapenzi katika moyo wa mwanafunzi, awe mwepesi katika kumfundisha kwa upole, akimtendea kwa huruma na kumhamasisha katika kujifunza.

Aidha inampasa amkumbushe ubora wa hilo ili iwe sababu ya uchangamfu wake, kuongeza katika hamu yake, amfanye kuipa nyongo dunia, amgeuze asiwe ni mwenye kuitegemea na kudanganyika nayo. Amkumbushe ubora wa kushughulika na Qur-aan na elimu nyingine za Kishari´ah na kwamba hiyo ndio njia ya wenye kumtambua Allaah na waja wema wa Allaah na kwamba hilo ni daraja ya Manabii (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam).

Inampasa amhurumie mwanafunzi, ajishughulishe na manufaa yake kama anavyojishughulisha na manufaa ya mwanawe na manufaa yake mwenyewe, na amfanye mwanafunzi kama mwanawe katika kumhurumia na kusubiri juu ya ukavu wake na ubaya wa adabu yake, na amsamehe katika uchache wa adabu yake katika baadhi ya nyakati, kwani mwanadamu anakabiliwa na upungufu, khaswa ikiwa ni mdogo wa umri.

Inampasa ampendelee yale anayojipendea nafsi yake katika kheri na amchukie yale anayoyachukia nafsi yake katika upungufu kwa ujumla. Kwani imethibiti ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Haamini mmoja wenu mpaka ampendelee ndugu yake yale anayojipendea nafsi yake.”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

”Mtu anayeheshimiwa zaidi kwangu ni yule anayekaa nami ambaye anawavuka watu mpaka anakaa kwangu. Lau ningeweza nisiruhusu nzi kumtua usoni mwake basi ningefanya.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

”Hakika nzi humtua ambapo akaniudhi.”

[1] Muslim (55).

[2] al-Bukhaariy (13), Muslim (45), at-Tirmidhiy (2515), an-Nasaa’iy (5016-5017) na Ibn Maajah (66).

  • Muhusika: Imaam Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy (afk. 677)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tibyaan fiy Aadaabi Hamalat-il-Qur-aan, uk. 29-30
  • Imechapishwa: 19/08/2026