12 – Muheshimiwa Shaykh ´Ubayd bin ´Abdillaah al-Jaabiriy (Hafidhwahu Allaah)

Aliulizwa muheshimiwa swali lifuatalo kuhusu Shaykh Rabiy´ kwenye kanda “at-Tabyaan fiy ba´dhw Akhtwaa´ ´Adnaan ´Ar´uur”:

“Kumezungumziwa sana kuhusu Shaykh Rabiy´ na kama ni mwanachuoni katika wanachuoni wa Waislamu?”

Akajibu:

“Himdi zote njema ni Zake Allaah kwa kuwa Shaykh Rabiy´ ni mwenye kujulikana vyema kwa watu maalum na wanachuoni. Shaykh wetu ´Abdul-´Aziyz bin Baaz amemsifu. Sikufikiria kabisa kwamba nitaulizwa swali hili.”

Amesema pia (Hafidhwahu Allaah) katika kubainisha fitina ya Abul-Hasan:

“Nimesoma na kufuatilia aliyoandika muheshimiwa ´Allaamah na Shaykh Rabiy´. Nimeyafanyia utafiti kwa umakini na kuona kuwa makosa yote yaliyo kwa Abul-Hasan ni haki na sahihi.”

Amesema pia:

“Hakika Shaykh Rabiy´ (Hafidhwahu Allaah) na Shaykh Ahmad an-Najmiy (Hafidhwahu Allaah) wote wawili wana uzito katika elimu. Wao, himdi zote njema ni Zake Allaah, wanajulikana vyema kuwa na ´Aqiydah sahihi na mfumo wa salama na ulionyooka. Hakuna yeyote anayewakosoa isipokuwa yule ambaye yeye ndiye anastahiki kujeruhiwa.”

Vilevile aliulizwa (Hafidhwahu Allaah) swali:

“Ni yepi maoni yako kwa yule anayesema kuwa Shaykh Rabiy´ anawazungumzia vibaya Mashaykh, wanachuoni na walinganizi?”

Akajibu:

“Shayk Rabiy´ amebeba bendera iliokuwa na nguvu na iliyosimama, bendera ya Sunnah. Kwa ushahidi wa maimamu wamempendekeza na kumsifia. Kwa ajili hiyo ndio maana haitakikani kwa mtu kama mimi kuulizwa kuhusu yeye (Hafidhwahu Allaah). Lakini maadamu nimeulizwa, ni lazima nijibu:

Amependekezwa na Imaam, baba, ´Allaamah, Faqiyh na Shaykh ´Abdul- ´Aziyz bin Baaz (Hafidhwahu Allaah). Amependekezwa na Imaam, Faqiyh, Mujtahid, ´Allaamah na Shaykh Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn (Rahimahu Allaah). Amependekezwa na Imaam na Muhaddith wa zama hizi, Imaam Naaswir-ud-Diyn (al-Albaaniy) na kumsifu ya kwamba ndio mbebaji wa bendera ya Jarh na Ta´diyl leo. Bendera ambayo Shaykh Rabiy´ amebeba ni kama alama ya Jihaad kwa Ahl-us-Sunnah na kuitetea na watu wake na mpaka hivi leo ni kisu kwenye vifua vya watu wa Bid´ah, hajadhoofika, kulainika wala kupungua. Kwa ajili hii inapata kuwabainikia ya kwamba maneno haya yaliyotajwa yanatoka kwa aina mbili ya watu. Ima ni mtu ambaye hana uzowefu wala ujuzi juu ya kinachoendelea uwanjani na yeye anasema tu kile anachosikia, au ni mtu ambaye ni katika wapotevu hawa, wapindaji na viongozi wa fikiri ambao ni wapinzani walio dhidi ya Sunnah. Wanachukizwa na hawapumui kwa yale ambayo Shaykh Rabiy´ (Hafidhwahu Allaah) anayoandika kuwaraddi Qutbiyyuun na wengineo wakati alipoandika dhidi ya Sayyid Qutwub na kubainisha upindaji wake, ujinga wake na upotevu wake pamoja kuiweka haki wazi kwa yule anayetafuta haki. Kwa ajili hiyo ndio maana msistaajabishwe na wale wanaosema haya. Shaykh Rabiy´ hajapatapo kamwe kumsema vibaya mtu anayeita katika Uislamu juu ya elimu. Yeye pamoja na ndugu zake Waislamu na watoto, na khaswa wanafunzi, anawaongoza, anawanasihi, anawaelekeza, kuwafanya imara, anawafundisha na anawaondoshea utata wanaowekewa. Haya ndio ambayo tunayojua mpaka hivi leo kutoka kwake (Hafidhwahu Allaah).

  • Mhusika: Shaykh Khaalid bin Dhwahwiy adh-Dhwafayriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.rabee.net/ar/sharticles.php?cat=12&id=57
  • Imechapishwa: 04/12/2019