Mabwana hawa hawana mategemezi yoyote isipokuwa maneno ya ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) aliposema kuhusu Tarawiyh:

”Ni uzuri wa Bid´ah iliyoje!”[1]

Vilevile wamesema kwamba kuna mambo yaliyozuliwa ambayo Salaf hawakuyapinga. Moja katika mambo hayo ni kukusanywa kwa Qur-aan sehemu moja na kuandika Hadiyth katika vitabu. Tunajibu hayo kwa kusema kwamba mambo haya yana msingi katika Shari´ah na hayakuzuliwa. Kuhusiana na maneno ya ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) aliposema:

”Ni uzuri wa Bid´ah iliyoje!”,

anachokusudia ni Bid´ah upande wa kilugha na si upande wa Shari´ah. Kunaposemwa kuwa jambo fulani ni Bid´ah miongoni mwa mambo ambayo yana msingi katika Shari´ah ambayo yanautegemea, basi kunamaanishwa Bid´ah kwa mujibu wa lugha na si kwa mujibu wa Shari´ah. Kwa sababu Bid´ah kwa mujibu wa Shari´ah ni ile ambayo haina msingi wowote unaotegemewa katika Shari´ah. Kukusanya Qur-aan sehemu moja ni jambo lililo na msingi katika Shari´ah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiamrisha Qur-aan iandikwe. Hata hivyo ilikuwa inaandikwa sehemu mbalimbali. Ndipo Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) wakawa wameikusanya kwenye Kitabu kimoja ili kuilinda.

Kuhusiana na Tarawiyh Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliiswali pamoja na Maswahabah zake nyusiku kadhaa. Lakini hata hivyo akawa ameacha kuendelea kuswali nao kwa kuchelea isije ikafaradhishwa kwao. Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) wakaendelea kuiswali kila mtu kivyake wakati ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa bado yuhai na baada ya kufa kwake. Hali iliendelea hivyo mpaka hapo ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) alipowakusanya nyuma ya imamu mmoja kama walivyokuwa wakiswali nyuma ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa maana nyingine huku sio kuzua katika dini.

Kadhalika inahusiana na kitendo cha kuandika Hadiyth. Ni kitu kilicho na msingi katika dini. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaamrisha baadhi ya Maswahabah zake kuandika Hadiyth kadhaa pindi walipokuwa wamemwomba hilo. Mwanzoni alipokuwa amewakataza kufanya hivo kwa sura ya kijumla pindi alipokuwa bado yuko hai (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilikuwa ni kwa sababu ya kuchelea Qur-aan isije ikachanganyike na kitu kingine. Wakati alipokufa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kizuizi hiki kikawa kimeondoka. Hilo ni kwa sababu Qur-aan ilikuwa tayari imeshakamilika na kudhibitiwa kabla ya kufa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baada ya hapo waislamu wakawa wameziandika Hadiyth ili kuzilinda zisipotee. Allaah awajaze kwa hilo kwa kule kulinda Kitabu cha Mola Wao na Sunnah za Mtume wao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) visipotee na kuchezewa.

Pia tunahoji ni kwa nini shukurani hiyo, kwa mujibu wa madai yenu, haikufanywa na karne bora zaidi za Maswahabah, wanafunzi wa Maswahaba na wanafunzi wa wanafunzi wa Maswahabah, ambao walikuwa na mapenzi makubwa zaidi kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na walikuwa na pupa zaidi ya kufanya mema na kushukuru? Je, wale waliyozua maulidi walikuwa na uongofu zaidi na shukurani kubwa zaidi kwa Allaah kuliko wao? Hapana kabisa!

[1] al-Bukhaariy (02/252) (nr. 2010) kwa cheni ya wapokezi pungufu, al-Fath (04/294).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Huquwq-un-Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) bayn al-Ijlaal wal-Ikhlaal, uk. 154-155
  • Imechapishwa: 06/09/2025