Sunnah hii tukufu ya kuswali kwenye jangwa  ina hekima ilio kubwa na ya kina. Waislamu wana siku mbili kwa mwaka ambapo watu wa mji wote wanaume, wanawake na watoto wanakusanyika. Wanaelekea kwa Allaah kwa mioyo yao. Neno moja tu ndio lenye kuwakusanya. Wanaswali nyuma ya imamu mmoja. Wanasema “Allaahu Akbar” na “Laa ilaaha illa Allaah” na wanamuomba Allaah hali ya kuwa ni wenye kumtakasia nia. Ni kana kwamba wako katika moyo wa mtu mmoja; ni wenye furaha na kuburudika na neema za Allaah ambazo amewatunukia. Kwa hivyo sikukuu kwao inakuwa kweli ni sikukuu.

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewaamrisha wanawake wote kutoka kwenda kuswali swalah ya ´Iyd pamoja na wengine. Hakumbakiza yeyote na wala hakumpa udhuru mwanamke yoyote ambaye hakuwa na kitu cha kuvaa. Bali amemuamrisha aazime nguo kutoka kwa mwengine. Kadhalika amewaamrisha wanawake walio na udhuru wenye kuwazuia kuswali watoke wende mahali uwanjani ili washuhudie mema na du´aa ya waislamu.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), makhaliyfah na viongozi manaibu walikuwa wakiwaswalisha watu swalah ya ´Iyd. Halafu wanawakhutubia, wanawawaidhi na wanawafunza mambo yenye faida na wao katika dini na dunia yao na kuwaamrisha kutoa swadaqah ili tajiri aweze kumuonea huruma masikini na yule masikini aweze kufurahikia fadhila za Allaah ambazo amemtunukia kutoka kwenye mkusanyiko huu uliobarikiwa wenye kushukiwa juu yake na rehema na radhi. Pengine waislamu wakaifuata Sunnah ya Mtume wao na wakazihuisha desturi za dini yao ambazo ndio msingi wa utatuzi na mafanikio yao:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ اسْتَجِيبُواْ لِلّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُم لِمَا يُحْيِيكُمْ

“Enyi mlioamini! Muitikieni Allaah na Mtume anapokuiteni katika yale yenye kukupeni uhai.”[1]

[1] 8:24

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swalaat-ul-´Iydayn, uk. 37-38
  • Imechapishwa: 13/05/2020