Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Swalah na amani ziwe juu ya bwana wetu na Mtume Wake Muhammad, kizazi chake, wake zake na dhuriya yake.

MAELEZO

Mtunzi (Rahimahu Allaah) wa kitabu hichi kitukufu amemalizia kwa kumswalia na kumtakia amani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni lazima kufanya hivo kwa sababu Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

”Hakika Allaah anamsifu na Malaika wake wanamuombea msamaha Mtume. Hivyo enyi walioamini mswalieni na mumsalimu kwa salamu.”[1]

Miongoni mwa haki ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu yetu ni kumswalia na kumtakia amani wakati anapotajwa. Pindi tunapomaliza kutunga kitabu basi tunamaliza kwa kumswalia na kumtakia amani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Katika Tashahhud tunamswalia na kumtakia amani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hiyo ni nguzo ya swalah.

Haitoshi kumswalia na kumtakia amani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilihali humfuati. Ni lazima kumfuata. Baadhi ya watu wanasema kwamba yule ambaye anataka kulipwa thawabu basi ahakikishe daima anamswalia na kumtakia amani na kwamba watu wako huru kufikiria wanavotaka. Si sahihi. Wewe ni mja wa Allaah (´Azza wa Jall). Unatakiwa kujisalimisha na amri ya Allaah. Wewe hauko huru kwa maana ya kwamba unaweza kufanya upendavyo. Wewe uko huru kwa maana ya kwamba unatakiwa kuchukua msimamo madhubuti dhidi ya mielekeo na ´Aqiydah mbalimbali na badala yake kutendea kazi yaliyo ya sawa na kujiepusha na ya makosa. Huu ndio uhuru sahihi. Uhuru sahihi ni kwa kufuata Qur-aan na Sunnah. Qur-aan na Sunnah vinamfanya mtu kuwa huru kutokamana na fikira chafu na potofu. Uhuru mkubwa ni kwamba vinamsalimisha mtu kutokamana na shirki, Bid´ah na ukhurafi. Huu ndio uhuru sahihi. Uhuru si kwa wewe kufanya vile unavopenda na kuitakasa nafsi yako. Huo sio uhuru. Mwenendo huo ni wa wanyama na watumwa. Amesema (Ta´ala):

أَفَرَأَيْتَ مَنِ اتَّخَذَ إِلَـٰهَهُ هَوَاهُ وَأَضَلَّهُ اللَّـهُ عَلَىٰ عِلْمٍ وَخَتَمَ عَلَىٰ سَمْعِهِ وَقَلْبِهِ وَجَعَلَ عَلَىٰ بَصَرِهِ غِشَاوَةً فَمَن يَهْدِيهِ مِن بَعْدِ اللَّـهِ ۚ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ

“Je, umemuona yule aliyejichukulia matamanio yake kuwa ndio mwabudiwa wake na Allaah akampotoa licha ya kuwa na elimu na akapiga muhuri juu ya masikio yake na moyo wake na akaweka kifuniko juu ya macho yake? Basi ni nani atamuongoa baada ya Allaah? Je, basi kwa nini hamkumbuki?”[2]

Yule anayeabudu matamanio yake ukweli wa mambo ni kwamba ameabudu matamanio yake; kule matamanio yanakomvuta ndipo anakokwenda na yale yanayopingana na matamanio yake anayaacha. Amesema (Ta´ala):

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ وَقَفَّيْنَا مِن بَعْدِهِ بِالرُّسُلِ ۖ وَآتَيْنَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ الْبَيِّنَاتِ وَأَيَّدْنَاهُ بِرُوحِ الْقُدُسِ ۗ أَفَكُلَّمَا جَاءَكُمْ رَسُولٌ بِمَا لَا تَهْوَىٰ أَنفُسُكُمُ اسْتَكْبَرْتُمْ فَفَرِيقًا كَذَّبْتُمْ وَفَرِيقًا تَقْتُلُونَ

“Hakika Tulimpa Muusa Kitabu na tukafuatisha baada yake Mitume na Tukampa ‘Iysaa, mwana wa Maryam, hoja za wazi na tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Je, basi kila anapokujieni Mtume kwa yale yasiyoyapenda nafsi zenu, basi mlitakabari, hivyo kundi [katika nyinyi] mlilikadhibisha na kundi [jengine] mnaliua.”[3]

Ni kwa nini walifanya hivo? Kwa sababu Mitume wanawalingania katika haki na wao wanachotaka ni kuyafuata matamanio yao.

Uhuru sahihi ni kwa kufuata Qur-aan na Sunnah, kwa sababu viwili hivyo vinamfanya mtu kuwa huru kutokamana na matamanio, maoni na fikira potofu. Qur-aan na Sunnah vinawafanya watu kuwa huru kutokamana na kuabudia miti, mawe, Shaytwaan na waliochupa mpaka. Kwa msemo mwingine huo ndio uhuru sahihi. Vyengine vyote ni utumwa na sio uhuru. Wengine wote ni watumwa wa matamanio, matashi, fikira zao na wale wanaowafata kichwa mchunga.

[1] 33:56

[2] 45:23

[3] 2:87

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 90-91
  • Imechapishwa: 08/09/2021