Swali 115: Ni sifa zipi za wanazuoni wanaotakiwa kufanywa marejeo?
Jibu: Ni wale wanaotambua Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), wameielewa Qur-aan na Sunnah, wakawa na elimu yenye manufa na matendo mema. Wanazuoni wanaotakiwa kufanywa marejeo ni wale waliokusanya elimu yenye manufaa na matendo mema. Mwanachuoni asiyeifanyia kazi elimu yake hatakiwi kuchukuliwa kama marejeo, wala ambaye ni mjinga mwenye kufanya matendo mema. Hachukuliwi kama marejeo isipokuwa ambaye amekusanya kati ya mambo hayo mawili.
Wale ambao ni marejeo nchini mwetu na ambao watu wanatakiwa kufaidika na kanda zao ni wengi na watu wote wanawatambua. Hakuna asiyekosa kuwatambua, ni mamoja mtu wa mashambani au mtu wa mjini, si mkubwa si mdogo. Ni wale wanaofanyia kazi mambo ya fatwa, hukumu, kufunza na mengineyo. Wanatambulika kuwa na elimu, uchaji Allaah na kujichunga, khaswakhaswa Shayk ´Abdul-´Aziyz bin Baaz[1]. Ni mtu ambaye Allaah amemneemesha elimu iliobobea, matendo mema, kulingania kwa Allaah, kumtakasia Allaah nia, ukweli na mengine mengi yanayotambulika kwa kila mtu. Amechangia kheri nyingi katika vitabu, mihadhara na darsa.
Vivyo hivyo wale wanazuoni ambao wanatoa fatwa katika barnamiji ”Nuur ´alaad-Darb”. Hao pia wanatambulika kwa fataawaa sahihi na maoni yenye manufaa. Nao ni Shaykh ´Abdul-´Aziyz bin Baaz, Shaykh Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn na ndugu zao waheshimiwa katika mahakama. Hakuna ambaye atajishughulisha na mahakama na watu wakamwamini katika damu, mali na ndoa zao isipokuwa tu yule ambaye ni mwenye kuaminika katika elimu yake. Hakika watu hawa wana juhudi kubwa katika kulingania kwa Allaah, kumtakasia nia Allaah na kuwaraddi watu ambao wanataka kupinda kutoka katika ile njia sahihi, ni mamoja wamefanya hivo kwa kukusudia au pasi na kukusudia. Hawa ni marejeo, wajuzi juu ya maoni mbalimbali na utambuzi wa kilico cha sawa na cha makosa. Kwa hivyo ni wajibu kueneza mihadhara na darsa zao na watu wafaidike nayo kwa sababu inayo faida kubwa kwa waislamu.
Vilevile kila mwanachuoni ambaye hatambuliki kwa makosa au upindaji kuchukuliwe faida kutoka kwake. Haijuzu kuchukua elimu kutoka kwa wajinga ingawa watajifanya ni wajuzi. Wala haijuzu kuchukua elimu kutoka kwa watu ambao wamepinda kutokana na ´Aqiydah kwa shirki au kuzikanusha sifa za Allaah wala kuchukua elimu kutoka kwa wazushi, ijapo watazingatiwa kuwa ni wanazuoni. Sampuli za watu ni tatu: watu wenye elimu ya manufaa na matendo mema, watu wenye elimu pasi na matendo na watu wenye matendo pasi na elimu. Allaah (Ta´ala) ametaja aina hizi mwishoni mwa Suurah ”al-Faatihah” na akatuamrisha kumuomba atuongoze katika njia ya sampuli ya watu wa kwanza na atulinde na njia ya sampuli mbili za mwisho:
اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ
“Tuongoze njia iliyonyooka; njia ya wale Uliowaneemesha, si ya walioghadhibikiwa wala waliopotea!”[2]
Aina ya kundi la kwanza wameneemeshwa na aina ya pili wameghadhibikiwa na aina ya tatu wamepotea. Sampuli mbili za mwisho zinawakilishwa na mapote yaliyopinda hii leo ingawa watajinasibisha na Uisalmu.
[1] ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin ´Abdir-Rahmaan bin Muhammad bin ´Abdillaah bin Baaz alizaliwa 1330-12-20 mjini wa Riyaadh. 1350 alipoteza uwezo wake wa kuona. Alihifadhi Qur-aan kabla ya kubaleghe, alibobea katika elimu za Shari´ah na akateuliwa kuwa Qaadhiy mwaka wa 1350. Maisha yake yalikuwa yakisheheni elimu, utafiti, kufunza na kutunga. Alijifunza elimu kupitia wanazuoni wengi, wakiwemo Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Latwiyf bin ´Abdir-Rahmaan Aalush-Shaykh, Swaalih bin ´Abdil-´Aziyz bin ´Abdir-Rahmaan Aalush-Shaykh, Sa´d bin Hamad bin ´Atiyq, Hamad bin Faaris, Muhammad bin Ibraahiym bin ´Abdil-Latwiyf Aalush-Shaykh na Sa´d Waqqaas al-Bukhaariy. Mwaka wa 1381 aliteuliwa kuwa makamu wa raisi wa chuo kikuu cha Madiynah na mwaka wa 1390 kuwa raisi katika chuo hichohicho. Mwaka wa 1395 kutokana na amri ya mfalme aliteuliwa kuwa raisi wa idara ya tafiti za kielimu, kutoa fatwa na ulinganizi. Mwaka wa 1414 kwa amri ya mfalme aliteuliwa kuwa mtoa fatwa wa nchi nzima Saudi Arabia.
Mbali na hayo alikuwa ni mjumbe wa baraza la Kibaar-ul-´Ulamaa na raisi wa kamati ya kudumu ya utafiti wa kielimu na utoaji fatwa, raisi wa World Muslim League, raisi wa baraka kuu la kimataifa la misikiti, raisi wa chuo cha Fiqh Makkah na mjumbe wa baraza kuu la chuo kikuu cha Kiislamu Madiynah.
Miongoni mwa vitabu vyake ni mijeledi ishirini na tatu iliyokusanya vitabu, vijitabu, Ruduud na maelezo.
Alikufa (Rahimahu Allaah) 1420-10-28 Twaaif, Saudi Arabia, na baadaye akazikwa Makkah. Allaah amlipe Pepo. Baada ya kufa kwake ndipo maoni ya kimajanga ya wajinga yakaaanza kuenea katika vyombo vya mawasiliano.
[2] 1:6-7
- Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 266-270
- Imechapishwa: 25/08/2024
- Taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)