115. Mzazi ananufaika na matendo mema anayofanyiwa na mwanawe

4 – Matendo mema anayoyatenda mtoto mwema, basi wazazi wake hupata ujira wake kama yeye bila ya kupunguziwa chochote katika ujira wake, kwa sababu mtoto ni matokeo ya juhudi na riziki yao. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَأَن لَّيْسَ لِلْإِنسَانِ إِلَّا مَا سَعَىٰ

“… na mtu hatopata [malipo] isipokuwa yale aliyoyafanyia juhudi.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika kilicho halali zaidi ambacho mtu anakila ni kutokana na kazi yake mwenyewe na hakika mtoto wake ni katika kazi yake.”

Ameipokea Abu Daawuwd (2/108), an-Nasaa’iy (2/211), at-Tirmidhiy (2/287) ambaye ameifanya kuwa ni nzuri, ad-Daarimiy (2/247), Ibn Maajah (2/430), al-Haakim (2/46), at-Twayaalisiy (1580) na Ahmad (6/41, 126, 127, 162, 173, 193, 201, 202, 220). al-Haakim amesema: “Ni Swahiyh kwa masharti ya al-Bukhaariy na Muslim” na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Hata hivyo kuna makosa katika Hadiyth hii kwa nyanja kadhaa ambazo haziwezi kufafanuliwa hapa kwa urefu.

Hadiyth hii inayo nyingine inayoipa nguvu kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Amr. Ameipokea Abu Daawuud, Ibn Maajah na Ahmad (2/179, 204, 214) kwa cheni ya wapokezi nzuri. Isitoshe yale yanayofahamishwa na Aayah na Hadiyth hapo juu yanatiwa nguvu na Hadiyth maalum kuhusu kunufaika kwa mzazi kutokana na matendo mema ya mtoto mwema kama vile kutoa swadaqah, kufunga, kuacha huru mtumwa na mfano wake. Hizi ni miongoni mwa Hadiyth hizo:

1 – ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza:

”Mwanamume mmoja alisema: “Hakika mama yangu amekufa ghafla [pasi na kuusia] na nadhani kama angeweza kusema basi angetoa swadaqah. Je, atapata thawabu nikitoa swadaqah kwa niaba yake [na mimi napata thawabu]?” Akasema: “Ndio, [mtolee swadaqah].”

Ameipokea al-Bukhaariy (3/198, 5/399–400), Muslim (3/81, 5/73), Maalik katika ”al-Muwattwa´” (2/228), Abu Daawuud (2/15), an-Nasaa’iy (2/129), Ibn Maajah (2/160), al-Bayhaqiy (4/62, 6/277–278) na Ahmad (6/51). Tamko ni la al-Bukhaariy katika riwaya moja na ziada ya mwisho ni yake katika riwaya nyingine. Ibn Maajah anayo ziada ya pili na Muslim anayo ziada ya kwanza.

2 – Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

”Sa´d bin ´Ubaadah – ndugu wa wana wa Saa´idah – mama yake alifariki dunia wakati yeye hayupo, akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Hakika mama yangu amefariki nami nikiwa sipo. Je, atanufaika nikitoa swadaqah kwa niaba yake?” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Ndiyo.” Akasema: “Basi nashuhudisha kuwa bustani ya al-Mukhraaf ni swadaqah kwa ajili yake.”

Ameipokea al-Bukhaariy (5/297, 301, 307), Abu Daawuud (2/15), an-Nasaa’iy (2/130), at-Tirmidhiy (2/25), al-Bayhaqiy (6/278), Ahmad (3080, 3504, 3508) na tamko ni la Ahmad.

3 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

”Mwanamume mmoja alimwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Baba yangu amekufa na ameacha mali na hakuacha wasia. Je, nimfidie kwa kutoa swadaqah kwa niaba yake?” Akasema: “Ndiyo.”

Ameipokea Muslim (5/73), an-Nasaa’iy (2/129), Ibn Maajah (2/160), al-Bayhaqiy (6/278) na Ahmad (2/371).

4 – ´Abdullaah bin ´Amr ameeleza:

”Hakika al-´Aasw bin Waa-il as-Sahmiy aliacha wasia ya kuachiwa huru watumwa 100 kwa niaba yake. Basi mtoto wake Hishaam akawaachia huru 50 ambapo mtoto wake mwingine ´Amr akataka kuwaachia huru wengine 50 waliobaki. Akasema: “Ngoja mpaka nimuulize Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Akamwendea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema: “Ee Mtume wa Allaah! Hakika baba yangu ameacha wasia ya kuwaachia huru watumwa 100. Hishaam amewaachia 50 na wamesalia 50. Je, niwaachie huru kwa niaba yake?” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Kama angekuwa muislamu mkawaachia huru au mkatoa swadaqah au mkamhijia basi ingemfikia thawabu hiyo.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

“Kama angelikuwa anakubali  Tawhiyd, mkafunga na kutoa swadaqah kwa niaba yake, basi yangemnufaisha.”

Ameipokea Abu Daawuud mwisho wa ”Kitab-ul-Waswayaa” (2/15), al-Bayhaqiy (6/279) ambaye tamko ni lake, Ahmad (6704) na riwaya nyingine ni yake pia. Cheni yake ya wapokezi ni nzuri.

[1] 53:39

  • Muhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 216-219
  • Imechapishwa: 02/08/2026