115. Dalili zinazoonyesha kuwa uchawi, kujifunza na kuufunza, ni ukafiri

Aayah hizi zinafahamsiha juu ya kwamba uchawi ni kufuru na ndio maana kaitumia mwandishi kama dalili kuonyesha kuwa uchawi ni kufuru na kwamba ni miongoni mwa vitenguzi vya Uislamu. Hilo ni kwa njia nyingi tu:

1- Maneno Yake:

وَمَا كَفَرَ سُلَيْمَانُ

“Sulaymaan hakukufuru… “

Bi maana hakufanya uchawi. Kwa kuwa uchawi ni kufuru na wala haimpasi kwa Mtume wa Allaah Sulaymaan.

2- Maneno Yake:

وَلَـٰكِنَّ الشَّيَاطِينَ كَفَرُوا يُعَلِّمُونَ النَّاسَ السِّحْرَ

”… lakini mashaytwaan ndio waliokufuru; wanafundisha watu uchawi.”

Ni dalili inayoonyesha kwamba kujifunza uchawi ni kufuru na kwamba ni katika mafunzo ya mashaytwaan na sio katika mafunzo ya Mitume (Swalla Alaahu ´alayhim wa sallam).

3- Maneno Yake:

وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ

”… lakini mashaytwaan ndio waliokufuru; wanafundisha watu uchawi na yaliyoteremshwa kwa Malaika wawili [katika mji wa] Baabil Haaruut na Maaruut. Na [hao Malaika wawili] hawamfundishi yeyote mpaka wamwambie kwanza: “Hakika sisi ni mtihani, hivyo basi usikufuru [kwa kufanya uchawi].”

Kwa msemo mwingine ni kwamba wanamwambia asijifunze uchawi. Kwa sababu yule mwenye kujifunza uchawi amekufuru. Ni dalili ioneshayo ya kuwa kujifunza uchawi ni kufuru.

4- Maneno Yake:

وَلَقَدْ عَلِمُوا لَمَنِ اشْتَرَاهُ مَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِنْ خَلَاقٍ

“Kwa hakika walielewa kwamba atakayenunua [huo uchawi] hatopata katika Aakhirah fungu lolote.”

Haya ni kwa haki ya kafiri. Kafiri ndiye ambaye Aakhirah, bi maana Peponi, hana fungu lolote. Ni dalili inayofahamisha kwamba uchawi ni kufuru kwa kuwa unamzuia mtu kuingia Peponi.

5- Maneno Yake:

وَلَوْ أَنَّهُمْ آمَنُوا وَاتَّقَوْا

”Lau wangeliamini na wakamcha Allaah.”

Hii ni dalili nyingine inayoonyesha kwamba uchawi unapingana na imani na kumcha Allaah. Hizi ni sehemu katika Aayah hii ambazo zote zinaonyesha kuwa uchawi, kujifunza nao na kuufunza ni kufuru na kwamba mwenye kuuchagua basi hakika amechagua kufuru badala ya imani na hivyo amekuwa kafiri. Jengine ni kwamba hana fungu lolote Peponi na kuwa mwenye kujifunza uchawi imani kwake imebatilika:

وَلَوْ أَنَّهُمْ آمَنُوا وَاتَّقَوْا

”Lau wangeliamini na wakamcha Allaah.”

Hii ni dalili inayofahamisha kwamba uchawi unapingana na imani na kwamba ni kichenguzi moja cha UIslamu. Hii ndio sababu ya Shaykh (Rahimahu Allaah) kuitumia Aayah hii kama dalili.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 148-149
  • Imechapishwa: 31/01/2019