112. Maiti ananufaika na du´aa anayoombewa na watu

114 – Mambo ambayo maiti hunufaika nayo kutokana na matendo ya wengine ni yafuatayo:

1 – Du´aa ya muislamu kwa ajili yake iwapo yatatimia masharti ya kukubaliwa. Hilo ni kutokana na maneno Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Na wale waliokuja baada yao ni wenye kusema: “Mola wetu! Tusamehe sisi na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo kwa wale walioamini – Mola wetu! Hakika ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.”[1]

Kuhusu Hadiyth ni nyingi sana. Baadhi yake zimeshatangulia na zingine zitakuja kuhusu kuyatembelea makaburi na du´aa ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa ajili yao. Aidha amri yake kuhusu hilo. Miongoni mwayo ni maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Du´aa ya mtu muislamu kwa ajili ya ndugu yake kwa siri hukubaliwa. Kichwani mwake kuna Malaika aliyekabidhiwa, kila anapomwombea ndugu yake kheri, basi Malaika huyo husema: ”Aamiyn nawe upate mfano wa hilo.”

Ameipokea Muslim (8/86-87) ambaye tamko ni lake, Abu Daawuud (1/240) na Ahmad (6/452) kupitia kwa Abud-Dardaa´ (Radhiya Allaahu ´anh).

Bali swalah ya jeneza yote ni dalili juu ya hilo, kwani sehemu kubwa yake ni du´aa kwa ajili ya maiti na kumuombea msamaha, kama ilivyotangulia kubainishwa.

[1] 59:10

  • Muhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 213
  • Imechapishwa: 02/08/2026