Swali 111: Je, Salafiyyah ni kipote kama mapote mengine na mtu anasemwa vibaya kwa kujinasibisha nayo?

Jibu: Salafiyyah ndio kundi lililookoka. Nao ndio Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na sio kipote kama mapote mengine. Mambo yalivyo ni kwamba wamekusanyika juu ya Sunnah na dini. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Hatokuacha kuwepo kikundi kutoka katika ummah wangu hali ya kuwa ni chenye kushinda juu ya haki. Hakitodhurika na wale wenye kuwakosesha nusura wala wale wenye kwenda kinyume nao mpaka ifike amri ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) wakiwa katika hali hiyo.”[1]

”Mayahudi wamegawanyika makundi sabini na moja. Manaswara wamegawanyika makundi sabini na mbili.  Na Ummah wangu utagawanyika katika mapote sabini na mbili. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu.” Wakasema: ”Ni lipi hilo, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: ”Ni lile linalofuata yale ninayofuata mii hii leo na Maswahabah zangu.”[2]

Salafiyyah ni kundi lilioko juu ya ´Aqiydah ya Salaf na walioshikamana na yale aliyokuwemo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake. Sio kipote kama mapote mengine yaliyopo hii leo[3]. Hakika mambo yalivyo ni kwamba ni kundi la tangu hapo zamani ambalo limerithiwa kuanzia wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Litaendelea kuwa lenye kushinda juu ya haki mpaka kisimame Qiyaamah.

[1] Muslim (3/1037).

[2] Ibn Maajah (3992), at-Tirmidhiy (2641) na Abu Daawuud (4596). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Mishkaat-ul-Maswaabiyh” (171).

[3] Salafiyyah wanapambana na uvyamavyama kwa kila namna na kila njia. Sababu iko wazi sana kwa vile Salafiyyah inajinasibisha na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amekingwa na kukosea. Ambaye ametoka nje ya ulinganizi wao hatumwiti kuwa ni Salafiy. Ambaye atadai kuwa ni Salafiy basi ahakikishe kuwa kweli anawafuata Salaf. Vinginevyo jina halibadilishi uhalisia wa mambo.

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 256-257
  • Imechapishwa: 20/08/2024
  • Taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy