111. Maswahabah wanatajwa kwa njia nzuri pekee

Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Asiweko yeyote katika Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) atakayetajwa isipokuwa kwa njia nzuri. Magomvi yaliyotokea baina yao yanatakiwa kunyamaziwa. Wao wana haki zaidi ya kutafutiwa nyudhuru.

MAELEZO

Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kuwasifu Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na asitajwe yeyote katika wao isipokuwa kwa njia nzuri. Kwa sababu Allaah amewasifu, akawatapa na akawaridhia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msiwatukane Maswahabah wangu. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi ya Muhammad imo mikononi Mwake lau mmoja wenu atajitolea dhahabu mfano wa mlima wa Uhud basi hatofikia vitanga viwili vya mikono vilivyojazwa na mmoja wao wala nusu yake.”[1]

Kila mtu, wakiwemo Maswahabah, wanatumbukia katika magomvi. Hata hivyo Allaah amewatunuku Maswahabah fadhilah kwa njia ambayo hawachafuliwi kwa magomvi yaliyowatokea. Wakati kunapotea fitina baadhi ya watu hujizuia na kutojiingiza ndani yake, wengine huingia ndani kutokana na ijitihadi zao na kujaribu kuizima. Kwa ajili hiyo haitakiwi kwa mtu kuingia ndani ya magomvi yao isipokuwa kwa lengo la kuwapa udhuru.

Maswahabah inapokuja kwa mtu mmojammoja hawakukingwa na makosa, lakini jumla ya Maswahabah wamekingwa na makosa na maafikiano yao ni hoja. Lakini kama mtu mmojammoja wanaweza kutumbukia kwenye makosa  na akasamehewa kwa sababu mbambali ikiwa ni pamoja na tawbah, fadhilah za uswahabah na ubora wa matendo matukufu. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kati ya mapokezi haya yaliyokuja kuna ambayo ni ya uongo, na kuna ambayo yamezidishwa juu yake na kupunguzwa, na kuna ambayo yamebadilishwa kinyume na sura yake ya kihakika na ndani yake kuna ya sahihi ambayo wamepewa udhuru kwayo. Ima walikuwa ni wenye kujitahidi baada ya kuifikia haki wakapatia, au walikuwa ni wenye kujitahidi baada ya kuifikia haki wakakosea.

Wao pamoja na hivyo hawaitakidi ya kwamba kila mmoja katika Maswahabah kakingwa na madhambi makubwa au madogo. Bali kinyume chake kuna uwezekano wakafanya madhambi kwa ujumla. Wana haki ya kutangulizwa na fadhila ambazo zinafanya wanasamehewa kwa lile wangelolifanya – ikiwa wamefanya kitu. Wanasamehewa hata madhambi ambayo yasingelisamehewa kwa mwengine yeyote baada yao, kwa kuwa wana mema mengi ambayo hana yeyote wa baada yao, na ambayo vilevile yanafuta makosa yao. Kumethibiti kwa kauli ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba wao ndio karne bora[2] na kwamba akitoa Swadaqah mmoja wao kiasi cha Mudd ina uzito zaidi kuliko inayotolewa na aliye baada yao, hata kama huyu atatoa dhahabu sawa na kiasi cha mlima wa Uhud. Ikiwa mmoja wao atapitikiwa na dhambi, atakuwa ima katubia kwa dhambi hiyo, au kaleta mema ambayo yameifuta au amesamehewa kwa fadhila za kutangulia kwake, au (kasamehewa) kwa uombezi wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – na hakuna ambaye ana haki zaidi kwa uombezi wake isipokuwa wao – au kapewa mtihani kwa majaribio ya duniani ambayo yamefuta dhambi yake. Ikiwa madhambi haya yaliyofanywa yanafanywa namna hii, vipi kwa mambo ambayo walikuwa ni wenye kujitahidi kuifikia haki? Ikiwa wamepatia wana ujira mara mbili na wakikosea wana ujira mara moja na kosa lao limesamehewa. Isitoshe, matendo mabaya yaliyofanywa na baadhi yao ni machache mno na yasiyokuwa na maana ukilinganisha na fadhila za nafasi yao na mema yao, kama kwa mfano kumuamini Allaah na Mtume Wake, na kupigana Jihaad katika njia ya Allaah, Hijrah, nusra, elimu yenye manufaa na matendo mema n.k.

Yule atakayetazana maisha71 ya Maswahabah kwa elimu na uwazi na fadhila Alizowaneemesha Allaah kwazo, basi atajua kwa yakini ya kwamba wao ndio viumbe bora baada ya Mitume. Kamwe hakukuwahi kuwepo na hakutokuwepo mtu mfano wao. Wao ndio wasomi wa wasomi katika Ummah huu – ambao ndio bora wa wabora na wa karimu kwa Allaah.”[3]

Imekuja katika Hadiyth:

“Allaah aliwatazama watu wa Badr na akasema: “Fanyeni mtakacho, hakika nimekusameheni.”[4]

Kwa hivyo wanasamehewa kutokana na kutangulia kwao, fadhilah na matendo yao matukufu.

[1] al-Bukhaariy (3673) na Muslim (2541).

[2] al-Bukhaariy (2652) na Muslim (2535).

[3] al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 13

[4] al-Bukhaariy (3007).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 83-84
  • Imechapishwa: 02/09/2021