Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Jengine ni kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kuwa ummah wake utagawanyika makundi 73. Aliyajua yatayopitika.

MAELEZO

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza juu ya yatayopitika katika mustakabali. Allaah ndiye amemfunulia hayo kwa ajili ya manufaa ya watu. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ

”Wala hawakizunguki chochote katika elimu Yake isipokuwa kwa akitakacho.”[1]

عَالِمُ الْغَيْبِ فَلَا يُظْهِرُ عَلَىٰ غَيْبِهِ أَحَدًا إِلَّا مَنِ ارْتَضَىٰ مِن رَّسُولٍ

”Mjuzi wa mambo yaliyofichikana na wala hamdhihirishii yeyote ghaibu Yake, isipokuwa yule aliyemridhia ambaye ni Mtume.”[2]

Wakati mwingine Allaah anamfunulia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kitu katika mambo yaliyofichikana yanayohusiana na yaliyopita na yatakayokuja huko mbele kwa ajili ya manufaa na dini yao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametueleza kuhusu mustakabali na akasema kuwa ummah utawaganyika:

“Na ummah wangu utagawanyika mapote sabini na tatu. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu.” Wakasema: “Ni lipi, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Ni lile litakalofuata mfano wa yale niliyomi mimi hii leo na Maswahabah zangu.”[3]

Wale walioendelea kushikamana na haki ndio waliookoka. Kuhusu ambao wameiacha haki wako Motoni. Baadhi yao wako Motoni kutokana na ukafiri wao, wengine wako Motoni kutokana na upotofu na dhambi zao. Hawako katika kiwango kimoja. Yule ambaye ataingia Motoni kwa sababu tu ya dhambi yake, ataadhibiwa humo kisha baadaye atatolewa. Ni miongoni mwa wale waumini watenda madhambi. Hadiyth ni kwa njia ya matishio na haina maana kuwa kila anayeenda kinyume ni kafiri na kwamba atadumishwa Motoni milele. Kubaki kwao Motoni kunatofautiana. Wako ambao watabaki humo hali ya kudumishwa humo milele na wengine watakuwemo humo kwa kipindi fulani tu. Hawa wa mwisho ni wale waumini watenda madhambi.

Kwa kifupi ni kwamba kila ambaye anaenda kinyume na yale aliyokuwemo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake anaingia ndani ya mapote yanayopingana na watu wa haki. Ametishiwa kuingia Motoni. Habaki juu ya haki. Hakuna wenye kuokolewa isipokuwa wale walioendelea kushikamana na njia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haya aliyotueleza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kwa ajili ya matahadharisho ya kwenda kinyume na yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), pia ni matahadhirisho ya kufarikiana na mahimizo ya kuwa na umoja juu ya haki na kushikamana na njia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake.

[1] 2:255

[2] 72:26-27

[3] Ibn Maajah (3992), at-Tirmidhiy (2641) na Abu Daawuud (4596). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Mishkaat-ul-Maswaabiyh” (171).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 164-165
  • Imechapishwa: 09/09/2024