11. Washirikina wa kale ni werevu zaidi kuliko washirikina wa leo

Washirikina wa kale walitambua maana ya neno hili kuliko walivyotambua watu hawa. Wao walipata kuelewa kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowataka kusema:

“Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah.”

basi ametaka kutoka kwao kuacha kuyaabudu masanamu na badala yake kumwabudu Allaah pekee. Ndio maana wakasema:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ

“Amewafanya waungu kuwa ni mungu Mmoja?  Hakika hili ni jambo la ajabu sana!”[1]

Watu wa Huud walisema:

أَجِئْتَنَا لِنَعْبُدَ اللَّـهَ وَحْدَهُ وَنَذَرَ مَا كَانَ يَعْبُدُ آبَاؤُنَا

“Je, umetujia ili tumwambudu Allaah pekee na tuyaache yale waliyokuwa wakiabudu baba zetu?”[2]

Watu wa Swaalih walisema:

أَتَنْهَانَا أَن نَّعْبُدَ مَا يَعْبُدُ آبَاؤُنَا

“Je, unatukataza kuabudu wale wanaowaabudu baba zetu?”[3]

Watu wa Nuuh walisema:

وَقَالُوا لَا تَذَرُنَّ آلِهَتَكُمْ وَلَا تَذَرُنَّ وَدًّا وَلَا سُوَاعًا وَلَا يَغُوثَ وَيَعُوقَ وَنَسْرًا

“Wakasema: “Msiwaache waungu wenu na wala msimwache Wadd na wala Suwaa´ na wala Yaghuuth na Ya’uuq na Nasr.”[4]

Haya ndio waliyoelewa makafiri kutokana na maana ya “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah” na kwamba inatakiwa kuacha kuyaabudu masanamu na badala yake mtu amwabudu Allaah Mmoja pekee. Kwa ajili hii ndio maana wakakataa kuitamka. Kwa sababu haikutani pamoja na kuabudu al-Laat, al-´Uzza na Manaatah.

Lakini waabudu makaburi hii leo hawaelewi mgongano huu. Utawaona wataitamka na huku bado wanaendelea kuwaabudu wafu.

Baadhi yao wanafasiri kwamba ´mungu` (الإله) maana yake ni yule ambaye ni muweza wa kuvumbua, kuumba na kufanya kupatikane kwa kitu[5]. Kwa msemo mwingine “hapana mungu isipokuwa Allaah” maana yake inakuwa “hapana muweza wa kuumba isipokuwa Allaah”, jambo ambalo ni kosa lililo baya. Mwenye kufasiri hivo basi hakuzidisha juu ya kile walichokikubali makafiri. Wao walikuwa wakikubali ya kwamba hapana muweza wa kuumba, kuruzuku, kuhuisha na kufisha isipokuwa Allaah pekee. Hivyo ndivyo Allaah ametaja kuhusu wao. Pamoja na hivyo hakukuwafanya wakawa waislam.

Ni kweli kwamba haya ambayo wanataja yanaingia ndani ya maana ya shahaadah. Lakini hayo si malengo ya neno hili.

Kushirikisha katika ´ibaadah ni pale ambapo mtu ataifanya au kutekeleza kitu katika hayo kumfanyia asiyekuwa Allaah. Tayari tumekwishaonyesha hapo kabla namna ilivyozuka ardhini. Bado mpaka hivi sasa inaendelea kwa viumbe – isipokuwa yule aliyerehemewa na Allaah.

[1] 38:05

[2] 07:70

[3] 11:62

[4] 71:23

[5] Kama ilivyotajwa katika vitabu vya I´tiqaad juu ya mfumo wa wanachuoni wa falsafa. Kwa mfano tazama ”Risaalat-ut-Tawhiyd” ya Muhammad ´Abduh.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Haqiyqat-it-Tawhiyd, uk. 17-19
  • Imechapishwa: 26/03/2019