26 – Ahmad bin Sulaymaan bin Hadhlam ad-Dimashqiy ametukhabarisha: Ja´far bin Muhammad al-Qalaaniysiy ametuhadithia: Abu Salamah Yaziyd bin Khaalid bin Murshid ametuhadithia: Sulaymaan bin Hayyaan ametuhadithia: Ibn Abiy Dhubaab al-Madiyniy ametuhadithia: Sa´iyd al-Maqburiy na Yaziyd bin Hurmuz amenikhabarisha, kutoka kwa Abu Hurayrah… Vivyo hivyo kutoka kwa Muhammad bin ´Amr, kutoka kwa Abu Salamah, kutoka kwa Abu Hurayrah… Vivyo hivyo kutoka kwa Daawuud bin Abiy Hind, kutoka kwa ash-Sha´biy, kutoka kwa Abu Hurayrah, ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Allaah alimuumba Aadam kwa mkono Wake, akampulizia kutoka katika roho Yake na akawaamrisha Malaika wamsujudie. Ndipo akapiga chafya na kusema: ”Himdi zote njema anastahiki Allaah.” Ndipo Mola wake akamwambia: ”Akurehemu Mola wako. Waendee Malaika wale kule na uwaambie: ”Amani ya Allaah iwe juu yenu.” Akawaendea na kuwatlea salamu, ambapo wakasema: ”Nawe amani na rehema za Allaah ziwe juu yako.” Kisha akarejea kwa Mola wake, aliyesema: ”Haya ni mamkizi yako na mamkizi ya kizazi chako kati yao.” Halafu akamshika mikono Yake – na mikono Yake yote miwili ni ya kulia – na akaifungua. Ndani yake kulikuwa na sura ya kizazi chake chote. Kila mtu alikuwa ameandikiwa muda wake wa kuishi. Yeye mwenyewe alikuwa ameandikiwa miaka elfu. Akawaona watu wenye nuru ambapo akasema: ”Ee Mola, ni kina nani hawa watu wenye nuru ya kung´aa?” Akasema: ”Hawa ni Manabii (au Mitume) ambao nimewatumiliza kwa waja Wangu (au viumbe Wangu).” Miongoni mwao alikuwepo bwana mmoja ambaye alikuwa na nuru zaidi na hakuandikiwa isipokuwa tu kuishi miaka arobaini.” Akasema: ”Ee Mola, vipi huyu, ndiye mwenye nuru ya ziada katika wao na hakuandikiwa isipokuwa tu kuishi miaka arobaini?” Akasema: ”Hayo ndio Nimeandika.” Akasema: ”Ee Mola! Mzidishie miaka sitini kutoka katika umri wangu.” Wakati Allaah alipomfanya kukaa Peponi na baadaye akamteremsha ardhini, kama Allaah alivyotaja ndani ya Qur-aan, akajiwa na kifo, ambapo akasema: ”Mbona umenijilia mpema.” Kifo kikasema: ”Nimefanya nini?” Akasema: ”Nimebakiza miaka sitini ya kuishi.” Kikasema: ”Hakuna chochote kilichobaki katika umri wako. Ulimuomba Mola wako amwandikie mwanao Daawuud.” Ndipo akasema: ”Sijafanya hivo kabisa.” Akasahau na kizazi chake pia kikasahau. Akakanusha na kizazi chake pia kikakanusha. Kuanzia wakati huo kukawekwa kitabu na kukaamrishwa kuwepo ushahidi. Baada ya hapo Muusa akakutana naye na kusema: ”Wewe ndiye Aadam. Allaah amekuumba kwa mkono Wake, akakupulizia kutokana na roho Yake, akawaamrisha Malaika kukusujudia na akakukaza Peponi, ambapo ukatufanya tutolewe Peponi kutokana na dhambi yako.” Ndipo Aadam akamwambia: ”Wewe ndiye Muusa ambaye Allaah (´Azza wa Jall) amekuteua kwa ujumbe na maneno Yake na akakupa Tawraat ambayo ndani yake kuna ubainifu wa kila kitu. Ni lini uliona kuwa Allaah ameandika Tawraat kabla ya kuniumba mimi?” Akasema: ”Miaka arobaini kabla.” Akasema: ”Hukuona ndani yake kwamba Aadam akamuasi Mola wake na akapotoka?” Akasema: ”Ndio.” Akasema: ”Je, unanilaumu kwa kitendo ambacho Allaah aliniandikia miaka arobaini kabla ya Yeye kuniumba?” Aadam akamshinda Muusa.”

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Ishaaq bin Mandah (afk. 395)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah, uk. 53-55
  • Imechapishwa: 09/06/2026
  • Taaliki: ´Allaamah ´Aliy bin Naaswir al-Faqiyhiy