11. Uwajibu wa kuamini na kuthibitisha majina na sifa za Allaah

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Kumuamini Allaah ina maana ni pamoja na kuamini yale aliyojisifia Mwenyewe katika Kitabu Chake na kwa yale aliyomsifia kwayo Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) bila ya upotoshaji, ukanushaji, kuzifanyia namna wala kufananisha. Bali wao wanaamini yafuatayo kuhusiana na Allaah (Subhaanah):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)

Hawakanushi kutoka Kwake yale ambayo amejisifu Mwenyewe na wala hawapotoshi maana ya maneno kuyatoa mahala pake. Hawaharibu majina ya Allaah na Aayah Zake. Hawaainishi maana Yake halisi, hawazifananishi na kuzilinganisha sifa Zake na sifa za viumbe Wake. Hakika Yeye (Subhaanah) hana mshirika wala mwenza na wala halinganishwi na viumbe Wake (Subhaanahu wa Ta´ala).

Kwani, hakika Yeye (Subhaanah) ni Mjuzi zaidi wa kujijua Mwenyewe na wengine na ni Mkweli zaidi kwa Kauli na Maneno yaliyo bora na ya wazi kuliko Viumbe Vyake.”

MAELEZO

Kumuamini Allaah ina maana ni pamoja na kuamini yale aliyojisifia Mwenyewe… – Kunaingia katika kumuamini Allaah mtu kuamini yale majina ambayo Allaah amejiita kwayo, kwa mfano al-Hakiym [Mwingi wa hekima], al-´Aziyz [Mwenye nguvu], Rawuf [Mpole], ar-Rahiym [Mwenye kurehemu], al-Qadiyr [Muweza] na mengineyo.

… na kwa yale aliyomsifia kwayo Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)… – Vilevile mtu kuamini yale majina na sifa ambazo Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemsifu kwazo katika Hadiyth Swahiyh. Ni wajibu kumthibitishia nayo Allaah. Kwa mfano yaliyokuja katika Hadiyth Swahiyh:

“Allaah anawacheka watu wawili ambapo mmoja wao kamuua mwenzake. Halafu wote wawili wanaingia Peponi.”[1]

“Hakika Mola Wangu leo amekasirika khasira ambayo hajapatapo kukasirika namna yake hapo kabla na hatokasirika mfano wake baada yake.”[2]

Bi maana siku ya Qiyaamah. Kuna sifa nyenginezo nyingi za Allaah (Jalla wa ´Alaa) ambazo zimekuja katika Qur-aan na Sunnah safi. Ahl-us-Sunnah wanaziamini na wakati huo huo wanaziitakidi. Wanaamini kuwa hakuna anayelingana Naye, hana mwenza wala hana mshirika. Vilevile halinganishwi na viumbe Vyake (Subhaanahu wa Ta´ala). Yeye ana majina mazuri na sifa kuu. Ahl-us-Sunnah hawafananishi sifa Zake na sifa za viumbe Vyake (Jalla wa ´Alaa). Wanajua kuwa sifa Zake zinalingana na Yeye na hazifanani na sifa za viumbe Vyake (Subhaanahu wa Ta´ala). Hana mwenye kulingana Naye:

هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا

“Je, unamjua mwenye jina kama Lake?” (19:65)

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

“Na wala hana yeyote anayefanana [kulingana] Naye.” (112:04)

فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

Basi msimfanyie Allaah waliolingana naye [washirika] na hali ya kuwa nyinyi mnajua [kuwa hana].” (02:22)

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanathibitisha sifa na majina ya Allaah kwa njia inayolingana Naye (Subhaanahu wa Ta´ala). Hawazipingi sifa Zake na hawayapotosho maneno kuyaondosha mahala pake stahiki. Bali wao wanaamini majina na sifa zote zilizokuja katika Qur-aan na Sunnah kwa njia inayolingana na Allaah.

Wanafanya hivo bila pasi na Tahriyf, upotoshaji. Upotoshaji maana yake ni kuyapotosha maneno, inafanywa hivo ima kwa kuzidisha au kwa kupunguza.

Wanafanya hivo pasi na kuzikanusha sifa Ta´twiyl. Maana yake ni kuikanusha sifa, kuipindisha au kupindisha maana yake.

Wanafanya hivo bila pasi na Takyiyf, kuzifanyia namna. Kwa mfano hawasemi “Allaah amelingana namna hii”, “Allaah hushuka namna hii”, “Allaah hukasirika namna hii”.

Wanafanya hivo bila pasi na Tamthiyl, kufananisha. Hawasemi “Allaah hukasirika mfano wa hivi”, “Allaah amelingana mfano wa hivi”, “Allaah husikia mfano wa hivi”, “Allaah huona mfano wa hivi”.

Badala yake wanamthibitishia Allaah majina na sifa zake kwa njia inayolingana Naye. Hawabadilishi, hawapotoshi, hawampigiii mfano, hawakanushi na hawaainishi namna. Kanuni yao katika hilo ni ifuatayo:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)

[1] al-Bukhaariy (2826) na Muslim (1890).

[2] al-Bukhaariy (3340) na Muslim (194).

 

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com