11. Qur-aan ni maneno ya Allaah na haikuumbwa kwa njia zake zote

Abu Muhammad ´Abdur-Rahmaan bin Abiy Haatim amesema:

2- Qur-aan ni maneno ya Allaah na haikuumbwa kwa njia zake zote.

MAELEZO

Qur-aan ni maneno ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Qur-aan na Sunnah vinathibitisha kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah na kwamba Allaah anazungumza kwa maneno ya milele. Kuna dalili nyingi zisizoweza kudhibitiwa. Kile tunachosoma ni maneno ya Allaah. Kile tunachoandika ni maneno ya Allaah. Kile tunachohifadhi ni maneno ya Allaah. Vifaa vyote hivi vimeumbwa na sio maneno ya Allaah.

Maneno ya Allaah ni katika sifa Zake kama mfano wa ujuzi, uwezo, matakwa, usikizi na uoni Wake. Kule kuwa Kwake ni Muumba na Mruzukaji ni katika majina na sifa Zake. Hakuna anayefanana na majina na sifa Zake. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) anazungumza pale anapotaka na vile anavyotaka, pasi na kufanyia namna, kufananisha, kukanusha wala kupotosha.

Allaah anazungumza kwa maneno ya milele kama tulivyosema:

قُل لَّوْ كَانَ الْبَحْرُ مِدَادًا لِّكَلِمَاتِ رَبِّي لَنَفِدَ الْبَحْرُ قَبْلَ أَن تَنفَدَ كَلِمَاتُ رَبِّي وَلَوْ جِئْنَا بِمِثْلِهِ مَدَدًا

“Sema: “Lau kama bahari ingelikuwa ni wino wa [kuandika] maneno ya Mola wangu, basi ingelimalizika bahari kabla ya kumalizika maneno ya Mola wangu japokuwa tungelileta [bahari nyingine] mfano wake kuwa wino.” 18:109

وَلَوْ أَنَّمَا فِي الْأَرْضِ مِن شَجَرَةٍ أَقْلَامٌ وَالْبَحْرُ يَمُدُّهُ مِن بَعْدِهِ سَبْعَةُ أَبْحُرٍ مَّا نَفِدَتْ كَلِمَاتُ اللَّـهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

“Lau kama miti yote iliyomo katika ardhi ingelikuwa kalamu na bahari [ikafanywa kuwa wino] [na] juu yake ikaongezewa bahari saba zengine, yasingelimalizika maneno ya Allaah. Hakika Allaah ni Mwenye nguvu kabisa, Mwenye hikmah wa yote.” 31:27

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ameumba ulimwengu huu kukiwemo mbingu, ardhi, Malaika, majini, watu, miti, mawe, bahari, mito, samaki na vinginevyo kwa maneno Yake:

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ

“Hakika amri Yake anapotaka jambo huliambia: “Kuwa!” – nalo huwa.” 36:82

Hii ni miongoni mwa dalili yenye kuthibitisha kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) anazungumza na kuongea. Ameiita Qur-aan kuwa ni maneno Yake:

وَإِنْ أَحَدٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّىٰ يَسْمَعَ كَلَامَ اللَّـهِ

“Ikiwa mmoja wa washirikina akikuomba umlinde, basi mlinde mpaka asikie maneno ya Allaah.” 09:06

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) anaita. Alimwita Muusa:

إِذْ نَادَاهُ رَبُّهُ بِالْوَادِ الْمُقَدَّسِ طُوًى

“Mola wake Alipomuita kwenye bonde takatifu la Twuwaa.” 79:16

وَإِذْ نَادَىٰ رَبُّكَ مُوسَىٰ أَنِ ائْتِ الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ

“[Unakumbuka] pindi Mola wako Alipomwita Muusa [na kumwambia]: “Nenda kwa watu madhalimu.” 26:10

وَيَوْمَ يُنَادِيهِمْ أَيْنَ شُرَكَائِي قَالُوا آذَنَّاكَ مَا مِنَّا مِن شَهِيدٍ

“Siku Atakayowaita: “Wako wapi [sasa] washirika Wangu?” Watasema: “Tunakiri Kwako hapana miongoni mwetu awezaye kushuhudia [hayo kuwa wapo].” 41:47

Wito hauwi isipokuwa kwa sauti yenye kusiskika.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qurrat-ul-´Aynayn bi Tawdhwiyh Ma´aaniy ´Aqiydat-ir-Raaziyayn, uk. 21-22
  • Imechapishwa: 15/10/2016