Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Miongoni mwa Sunnah za lazima ambazo mwenye kuacha kipengele chake na akaacha kuikubali na kuiamini hawi katika watu wake. Miongoni mwa Sunnah hizo ni kuamini Qadar, kheri na shari yake na kusadikisha Hadiyth juu yake. Maswali kama “Kwa nini?” na “Vipi?” hayatakiwi kuulizwa. Kinachotakiwa ni kusadikisha na kuamini tu.”

MAELEZO

Imaam Ahmad amesema:

“Miongoni mwa Sunnah za lazima ambazo mwenye kuacha kipengele chake na akaacha kuikubali na kuiamini hawi katika watu wake.”

Zingatieni haya! Sentesi hii ni muhimu sana. Hapa Imaam Ahmad atataja misingi ambayo ni muhimu sana mwenye kutoiamini hawi ni katika Ahl-us-Sunnah. Ina maana ya kwamba anaacha mzunguko wa Sunnah na kuwa ni katika watu wa Bid´ah. Hivyo zingatieni haya! Amesema:

“Miongoni mwa Sunnah za lazima ambazo mwenye kuacha kipengele chake na akaacha kuikubali na kuiamini hawi katika watu wake.”

Janga kubwa ni kukanusha vyote au angalau vingi katika hivyo. Kutokuikubali ina maana ya kwamba anairudisha. Amesema:

“… hawi katika watu wake.”

Ikiwa sio katika Ahl-us-Sunnah ina maana ya kwamba anakuwa katika Ahl-ul-Bid´ah wadh-Dhwalaal. Mnajua kuwa Bid´ah imegawanyika katika kubwa na ndogo, shirki, ukafiri na majanga. Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Bid´ah ni yenye kutokamana na kufuru na inapelekea katika hilo.”

Bid´ah imejengwa juu ya matamanio na upotevu:

أَفَرَأَيْتَ مَنِ اتَّخَذَ إِلَـٰهَهُ هَوَاهُ وَأَضَلَّهُ اللَّـهُ عَلَىٰ عِلْمٍ وَخَتَمَ عَلَىٰ سَمْعِهِ وَقَلْبِهِ وَجَعَلَ عَلَىٰ بَصَرِهِ غِشَاوَةً فَمَن يَهْدِيهِ مِن بَعْدِ اللَّـهِ ۚ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ

“Je, umemuona yule aliyejifanyia matamanio yake kuwa ndio mungu wake na Allaah akampotoa juu ya kuwa na elimu na akapiga muhuri juu ya masikio yake na moyo wake na akaweka kifuniko juu ya macho yake? Basi nani atamuongoza baada ya Allaah? Ni kwa nini hamkumbuki?”[1]

Tunaomba kinga kwa Allaah juu ya kufuata matamanio. Ndio maana Ahl-us-Sunnah wamewaita Ahl-ul-Bid´ah kuwa ni “Ahl-ul-Ahwaa”, watu wa matamanio. Kwa sababu wameenda kinyume na dini ya Allaah na wakafuata matamanio yao. Mfano wa watu hawa ni Khawaarij, Raafidhwah, Mu´tazilah, Jahmiyyah, Murji-ah, Suufiyyah, Huluuliyyah, watu wa Wahdat-ul-Wujuud, waabudu makaburi na watu mfano wao. Bid´ah na upotevu wote huu yanaenda kinyume na Qur-aan na Sunnah pamoja na misingi na kanuni za ´Aqiydah.

Imaam Ahmad amesema:

“Miongoni mwa Sunnah hizo ni kuamini Qadar… “

Asiyeamini Qadar sio katika Ahl-us-Sunnah. Ameacha moja katika vipengele vikubwa na vya msingi vya ´Aqiydah. Kuamini Qadar ni nguzo miongoni mwa nguzo za imani. Ni jambo limethibitishwa na Qur-aan na Sunnah. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

وَكُلَّ شَيْءٍ أَحْصَيْنَاهُ فِي إِمَامٍ مُّبِينٍ

“Kila kitu tumekirekodi barabara katika kitabu kinachoweka wazi.”[2]

Allaah ana ujuzi juu ya kila chenye kupitika na amekiandika katika Ubao uliohifadhiwa. Dalili nyingine ya Qadar ni:

إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ

“Hakika Sisi tumekiumba kila kitu kwa makadirio.”[3]

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) alimtuma Jibriyl kwenda kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ili ahakikishe misingi na nguzo za Uislamu. Jibriyl aliuliza:

“Ni nini Uislamu?” Akajibu: “Uislamu ni kushuhudia ya kwamba hapana mungu mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji Nyumba ukiwa na uwezo wa kufanya hivo.”

Kisha akauliza:

“Ni nini imani?” Akajibu: “Imani ni kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Wake, siku ya Mwisho na kuamini Qadar; kheri na shari yake.”[4]

Nguzo tano mbali na Qadar zimetajwa kwa pamoja katika Qur-aan. Imani ya kuamini Qadar imetajwa katika Aayah za Qur-aan zilizojitenga. Misingi ya imani imetajwa kwenye Aayah nyingi ikiwa ni pamoja na:

آمَنَ الرَّسُولُ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْهِ مِن رَّبِّهِ وَالْمُؤْمِنُونَ ۚ كُلٌّ آمَنَ بِاللَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّن رُّسُلِهِ ۚ وَقَالُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۖ غُفْرَانَكَ رَبَّنَا وَإِلَيْكَ الْمَصِيرُ

 “Mtume ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake na waumino. Wote wamemuamini Allaah na Malaika Wake na Vitabu Vyake na Mitume Wake – hatutofautishi baina ya yeyote kati ya Mitume Wake – na wakasema: “Tumesikia na tumetii. Tunakuomba msamaha, Mola wetu, na Kwako ndipo mahala pa kuishia.”[5]

Wakati fulani Qadar inatajwa katika Aayah zilizojitenga na wakati mwingine zote zinatajwa kwa pamoja. Zote zimetolewa dalili na Qur-aan na Sunnah, kama alivyothibitisha hilo Jibriyl na Hadiyth ya ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh).

[1] 45:23

[2] 36:12

[3] 54:49

[4] al-Bukhaariy (50) na Muslim (8).

[5] 02:285

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 373-374
  • Imechapishwa: 23/07/2017