11. Haniyfiyyah ndio dini ya Ibraahiym (صلى الله عليه وسلم)

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Tambua – Allaah Akuongoze katika utiifu Wake – kwamba Haniyfiyyah ndio dini ya Ibraahiym; nako ni kule
kumuabudu Allaah Pekee hali ya kumtakasia Yeye Dini. Hilo Allaah Amewaamrisha watu wote na Amewaumba kwa lengo hilo. Allaah (Ta´ala) Amesema:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na wanadamu isipokuwa waniabudu.” (adh-Dhaariyaat 51 : 56)

Maana ya “waniabudu” ni wanipwekeshe.

Kubwa Aliloamrisha Allaah ni Tawhiyd, nayo ni kumpwekesha Allaah kwa ´ibaadah. Kubwa Alilokataza Allaah ni Shirki, nako ni kuomba wengine pamoja Naye. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote.” (an-Nisaa´ 04 : 36)

MAELEZO

Amesema (Rahimahu Allaah):

“Tambua – Allaah kuongoze katika utiifu Wake… “

na akikusanya mafunzo na du´aa. Amesema (Rahimahu Allaah):

“… kwamba Haniyfiyyah ndio dini ya Ibraahiym; nako ni kule kumuabudu Allaah Pekee hali ya kumtakasia Yeye dini.”

Kuhusu hilo Allaah amesema kumwambia Mtume wake:

ثُمَّ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ أَنِ اتَّبِعْ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ۖ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ

“Kisha Tukakufunulia Wahy kwamba fuata imani safi kabisa na ya asli ya Ibraahim na hakuwa miongoni mwa washirikina.” (16:123)

Haniyfiyyah ni imani ambapo Allaah anaabudiwa na kupendwa kikweli na inayotupilia mbali shirki. Mtu ambaye ni Haniyf ni yule mwenye kumwelekea Allaah, kuvipa mgongo vyengine vyote na anampwekeshea Allaah ´ibaadah. Hivyo ndivyo alivyokuwa Ibraahiym na wafuasi wake, hivyo ndivyo walivyokuwa Mitume wengine na wafuasi wao. Amesema (Rahimahu Allaah):

“Hilo Allaah Amewaamrisha watu wote na Amewaumba kwa lengo hilo.”

Amewaamrisha kumpwekesha Allaah kwa nia safi. Amewaumba ili wamuabudu. Amewaamrisha wamuabudu Yeye pekee katika swalah zao, swawm, du´aa, khofu, matarajio, vichinjwa, nadhiri zao na aina nyenginezo zote za ´ibaadah. Yote anatakiwa afanyiwe Allaah pekee. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ

“Mola wako amehukumu kwamba: “Msiabudu yeyote isipokuwa Yeye pekee.”” (17:23)

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

“Wewe pekee ndiye tunakuabudu na Wewe pekee ndiye tunakuomba msaada.” (01:05)

فَاعْبُدِ اللَّـهَ مُخْلِصًا لَّهُ الدِّينَ

“Basi mwabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia Yeye dini.” (39:02)

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ

“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu.” (02:21)

Watu wameumbwa kwa ajili ya ´ibaadah hii; wamuabudu Allaah pekee, kutekeleza maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na wanaadamu isipokuwa waniabudu.” (51:56)

Bi maana wampwekeshe katika ´ibaadah na kumkhusisha kwa kutekeleza maamrisho na kujiepusha na makatazo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 18-19
  • Imechapishwa: 15/10/2016