108. Hoja yao ya mwisho wanayoweza kuja nayo

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Hoja yao ya mwisho ambayo wale wajuzi wao zaidi wanaweza kutumia ni maneno Yake (Ta´ala):

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

“… na wala haiwi awe na yeyote anayefanana na kulingana Naye.”[1]

هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا

“Je, unamjua yeyote mwenye jina kama Lake?”[2]

MAELEZO

Haitoshi kujengea hoja kwa Aayah za kukanusha; zipo Aayah zinazothibitisha. Kwa mfano Allaah (Ta´ala) anasema:

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ۚ

”Allaah, hapana mungu wa haki isipokuwa Yeye, Aliyehai daima, Mwenye kusimamia kila kitu.”[3]

Hapa kunathibitishwa uhai na usimamizi wa mambo.

وَهُوَ السَّمِيعُ البَصِيرُ

“… Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[4]

Huu ni uthibitisho.

وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

”Na Allaah ni Mjuzi wa kila kitu.”[5]

Huu ni uthibitisho.

Tawhiyd inayohusiana na majina na sifa za Allaah inategemea kuthibitisha na kukanusha; kuyathibitisha majina na sifa za Allaah na kukanusha kufanana na kupigiwa mfano. Kwa mfano Allaah aliposema:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ وَهُوَ السَّمِيعُ البَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[6]

Hapa kumekusanywa kati ya kukanusha na kuthibitisha; kunakanushwa kufanana na kushabihishwa na huku kunathibitishwa majina na sifa za Allaah. Hii ndio kanuni ya Qur-aan. Ama kutegemea makanusho peke yake mosi ni upotofu, pili ni jambo halifahamishwi na Qur-aan na Sunnah.

Wanaojifanya kuwa na akili ni wale wanaojifanya kuwa werevu ilihali sio werevu. Mfumo wa Ahl-ul-Bid´ah ni kuwa wanachukua baadhi ya maandiko na wanayaacha mengine. Wanachukua yale wanayofikiria kuwa yanasapoti ´Aqiydah yao na wanaacha yale yanayoenda kinyume na ´Aqiydah yao. Amesema (Ta´ala):

فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ

”Basi wale ambao katika nyoyo zao mna upotevu hufuata zile zisizokuwa wazi ili kutafuta fitina na kutafuta kuzipotosha.”[7]

Wanazichukua zile Aayah zisizokuwa wazi na kuziacha zile ambazo ziko wazi. Mwanazuoni aliyebobea anayachukua maneno ya Allaah yote, anafanya baadhi kuyafasiri mengine na kuyarejesha baadhi yakayafasiri mengine. Anayarejesha yale yasiyokuwa wazi katika yale ambayo yako wazi. Hafanyi sehemu ya Qur-aan ikagongana na nyingine; anaifanyia kazi Qur-aan yote. Wakati wapotofu wanapojengea hoja kwa dalili zinazomtakasa Allaah kufanana na viumbe, kwa sababu ndivo wanavyodai kuwa zinafahamisha hivo, tunasema kuwa majina na sifa za Allaah havifahamishi kile mnachofikiria. Kuthibitisha majina na sifa za Allaah hakulazimishi kumfananisha Allaah na viumbe Wake katika majina na sifa Zake. Dalili ya hilo ni kwamba Allaah Yeye mwenyewe amejithibitishia majina na sifa Zake na sambamba na hilo akajikanushia Mwenye kufanana na chochote. Kwa hivyo sisi tunazithibitisha kwa njia inayolingana na utukufu Wake. Majina Yake si kama majina mengine, sifa Zake si kama sifa zingine. Sisi tunazifanyia kazi dalili zote. Hatuchukui baadhi na tukaacha zingine, kama mnavofanya nyinyi.

[1] 112:1-4

[2] 19:65

[3] 02:255

[4] 42:11

[5] 49:16

[6] 42:11

[7] 3:7

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 158-159
  • Imechapishwa: 09/09/2024