109 – Anapasa kuwafariji kwa maneno anayodhani kuwa yatawafariji, kupunguza huzuni yao na kuwasaidia wawe na subira na ridhaa. Ikiwa anajua Hadiyth sahihi basi azitumie katika kufanya hivo. Vinginevyo aseme maneno mazuri yasiyopingana na Shari´ah. Kumepokelewa Hadiyth kadhaa juu ya hilo:

1 – Usaamah bin Zayd (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Mmoja wa wasichana zake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimpelekea ujumbe kwamba mtoto wake wa kiume au wa kike.” [Imekuja katika upokezi mwingine: ”Umayyah bint Zaynab.”] yuko katika hali ya kufa na kwamba anatakiwa kuja. Akamtumia ujumbe amtolee salamu na amwambia:

إن لله ما أخذ، و (لله) ما أعطي، وكل شئ عنده إلى أجل مسمى فالتصبر، ولتحتسب

”Hakika ni Chake Allaah kile alichokichukua na ni Chake Allaah alichotoa na kila kitu Kwake kina muda uliopangwa. Basi afanye subira na atarajie malipo kutoka Kwake.”

Lakini akamtumia ujumbe tena aje na akasisitiza. Hivyo akasimama (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaenda basi tuukaenda naye. Mtoto akawekwa juu ya mapaja yake au kwenye mapaja yake na alikuwa akivuta pumzi zake za mwisho [kana kwamba iko kwenye mfuko]. Mingoni mwa waliokuwepo hapo ni Mu´aadh bin ´Ubaadah, [Mu´aadh bin Jabal], Ubayy [bin Ka´b], nadhani na [Zayd bin Thaabit na wanaume wengine]. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akatokwa na machoiz. Sa´d akasema: ”Ni kitu gani hiki, ee Mtume wa Allaah, ilihali wewe ndiye umekataza kulia?” Akasema: ”Hii ni rehema ambayo Allaah huiweka kwenye nyoyo ya waja Wake. Hakika hapana vyenginevyo Allaah humrehemu miongoni mwa waja Wake wale wenye rehema.'”

Ameipokea al-Bukhaariy (3/120-122), Muslim (3/39), Abu Daawuud (2/58), an-Nasaa’iy (1/263), Ibn Maajah (1/280), al-Bayhaqiy (4/65-68-69) na Ahmad (5/204-206-206-206-206) na tamko ni lake, hivyo hivyo tamko la pili, ziada ya kwanza, ya saba na ya nane, ambazo zote ziko kwa al-Bayhaqiy. Nyongeza ya pili ni ya al-Bukhaariy na Muslim, an-Nasaa’iy, al-Bayhaqiy, ya tatu pia ni ya kwao, vivyo hivyo ya nne na ya tano zote isipokuwa Muslim, ya sita ni ya al-Bukhaariy na an-Nasaa´iy.

Ijapokuwa namna hii ya rambirambi ilitajwa kwa ajili ya mtu ambaye yuko katika hali ya kukata roho, kumfariji mtu ambaye tayari amekufa inafaa zaidi, kama linavyoonyesha dalili. Kwa ajili hiyo an-Nawawiy amesema katika “al-Adhkaar” na kwingineko:

“Hadiyth hii ndiyo bora zaidi ya kutoa rambirambi.”

2 – Buraydah bin al-Huswayb (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwatembelea na kuwaulizia hali ya Answaar. Ikamfikia khabari ya mwanamke wa Answaar aliyefiwa na mwanawe pekee na akahuzunika sana. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaenda kwake [akiwa pamoja na Maswahabah wake. Alipofika karibu na mlango wa mwanamke mwanamke yule akaambiwa: ”Mtume wa Allaah anataka kuingia kukupa mkono wa pole. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaingia ndani na kusema: ”Imenifikia khabari kuwa umepatwa na huzuni kubwa. Mche Allaah na uwe na subira.” Mwanamke yule akasema: ”Ee Mtume wa Allaah! [Kwa nini nisihuzunike] ilihali mimi ni mwanamke tasa, sina watoto wengi na huyu alikuwa wa pekee?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Tasa ni yule ambaye mtoto wake hubaki hai.” Kisha akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): ”Hakuna mwanamume au mwanamke yeyote muislamu ambaye amefiwa na watoto watatu na [akataraji malipo kutoka kwa Allaah] isipokuwa kwa ajili yao Allaah atamwingiza Peponi.” ´Umar akasema [Ambaye alikuwa upande wa mkono wa kulia wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): ”Namtoa fidia baba yangu na mama yangu, vipi kuhusu watoto wawili?” Akasema: ”Na wawili pia.”

Ameipokea al-Haakim (1/384) ambaye amesema: ”Cheni yake ya wapokezi ni Swahiyh.”

adh-Dhahabiy ameafikiana naye.

Bali Hadiyth hiyo ni kwa mujibu wa masharti ya Muslim. Wasimulizi wote ni wa Swahiyh, ingawa mmoja wao yuko na udhaifu upande wa hifdhi yake. Hata hivyo Hadiyth yake hii haishuki chini ya kiwango chake cha kuwa nzuri. al-Haythami amepokea katika “al-Majma’” (3/8) Hadiyth mfano wa hiyo na ziada ni kutoka kwake na akasema: ”Ameipokea al-Bazzaar na wanaume wake ni watu wa Swahiyh.”

3 – Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoingia kwa Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anh) baada ya kufiwa na mumewe Abu Salamah:

اللهم اغفر لابي سلمة، وارفع درجته في المهديين، واخلفه في عقبه في الغابرين، واغفر لنا وله يا رب العالمين، وافسح له في قبره، ونور له فيه

“Ee Allaah! Msamehe Abu Salamah, muinue daraja yake kati ya walioongoka, mrithishe katika kizazi chake, msamehe yeye na sisi, ee Mola wa walimwengu, mpanulie kaburi lake na muwekee nuru humo.”

Ameipokea Muslim na wengineo. Imekwishatangulia kwa ukamilifu wake katika masuala ya 17, ukurasa wa 12.

4 – Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomfariji ´Abdullaah bin Ja´far baada ya kufiwa na baba yake:

اللهم اخلف جعفرا في أهله، وبارك لعبد الله في صفقة يمينه، قالها ثلاث مرات

“Ee Allaah! Mpe Ja´far mrithi mwema kwa familia yake na mbariki ´Abdullaah katika biashara ya mkono wake wa kulia.” Alisema hivo mara tatu.”

Ameipokea Ahmad kwa cheni ya wapokezi Swahiyh katikati ya Hadiyth ambayo itakuja kwa ukamilifu wake katika suala linalofuata.

Kuna Hadiyth nyingine kuhusu tanzia, ambazo nilipuuza kuzitaja kutokana na udhaifu wake. Nimebainisha hilo katika kuwa ”at-Ta’liqaat al-Hiyaad”, ikiwa ni pamoja na Hadiyth ya maandishi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Mu´aadh bin Jabal akimpa pole kwa kifo cha mwanawe, ambayo imezuliwa. Hivo ndivo alivosema ad-Dhahabiy, al-´Asqalaniy na wengineo. ash-Shawkaniy alishangazwa na hilo na Swaddiyq Hasan Khaan akamfanyia ufuatiliaji ambapo akaifanya kuwa nzuri kwa kumfuata al-Haakim. Kwa hivyo usidanganyike na hilo. Kwa maana kila farasi hujikwaa, bali wanajikwaa sana.

  • Muhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 206-208
  • Imechapishwa: 29/07/2026