Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Miongoni mwa Sunnah ni kuwapenda Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kutaja mazuri yao na kuwaombea rehema, kuwaombea msamaha, kujiweka mbali na kutaja kasoro zao na tofauti iliotokea kati yao, kuamini ubora wao na kutambua kutangulia kwao. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا

”Na wale waliokuja baada yao wanasema: “Mola wetu! Tusamehe sisi na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala usijaalie katika nyoyo zetu mafundo kwa wale walioamini.”[1]

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّـهِ ۚ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ

”Muhammad ni Mtume wa Allaah na wale walio pamoja naye ni wakali kwa makafiri wanahurumiana baina yao.”[2]

MAELEZO

Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) wana fadhilah kubwa juu ya Ummah huu kwa sababu walisimama kwa kumnusuru Allaah na Mtume Wake na wakapambana katika njia ya Allaah kwa mali zao na nafsi zao na wakahifadhi dini ya Allaah kwa kuhifadhi Kitabu Chake na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kiujuzi, kimatendo na hali ya kuzifunza mpaka zikaufikia Ummah zikiwa safi kabisa.

Allaah amewasifu ndani ya Kitabu Chake kitukufu sifa kuu pale aliposema katika Suurah “al-Fath”:

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّـهِ ۚ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ ۖ تَرَاهُمْ رُكَّعًا سُجَّدًا يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا ۖ سِيمَاهُمْ فِي وُجُوهِهِم مِّنْ أَثَرِ السُّجُودِ ۚ ذَٰلِكَ مَثَلُهُمْ فِي التَّوْرَاةِ ۚ وَمَثَلُهُمْ فِي الْإِنجِيلِ كَزَرْعٍ أَخْرَجَ شَطْأَهُ فَآزَرَهُ فَاسْتَغْلَظَ فَاسْتَوَىٰ عَلَىٰ سُوقِهِ يُعْجِبُ الزُّرَّاعَ لِيَغِيظَ بِهِمُ الْكُفَّارَ ۗ وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ مِنْهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا

“Muhammad ni Mtume wa Allaah. Na wale walio pamoja naye ni wakali zaidi dhidi ya makafiri wanahurumiana baina yao. Utawaona wakirukuu na wakisujudu wakitafuta fadhilah na radhi kutoka kwa Allaah. Alama zao dhahiri zi katika nyuso zao kutokana na athari za sujudu. Huo ni mfano wao katika Tawraat na mfano wao katika Injiyl kama mmea umetoa chipukizi lake, likautia nguvu kisha likawa nene, kisha likasimama sawasawa juu ya shina lake liwapendezeshe wakulima ili kuwakasirisha makafiri. Allaah amewaahidi wale walioamini na wakatenda mema miongoni mwao msamaha na ujira mkubwa.”[3]

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alihami heshima yao pale aliposema:

“Msiwatukane Maswahabah wangu. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi ya Muhammad imo mikononi Mwake lau mmoja wenu atajitolea dhahabu mfano wa mlima wa Uhud basi hatofikia viganja viwili vya mikono vilivyojazwa na mmoja wao wala nusu yake.”

Kuna maafikiano juu yake.

[1] 59:10

[2] 48:29

[3] 48:29

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 149-150
  • Imechapishwa: 15/12/2022