107. Kisimamo cha Ramadhaan kimemalizika, lakini ´ibaadah ya kusimama usiku kuswali inaendelea

Ingawa kimemalizika kisimamo cha mwezi wa Ramadhaan lakini kusimama usiku kuswali bado kunaendelea katika kila usiku miongoni mwa nyusiku za mwaka, jambo ambalo limethibiti kupitia matendo na maneno yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa al-Mughiyrah bin Shu´bah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia:

“Ilikuwa inatokea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anasimama au anaswali mpaka zinapasuka nyayo zake za miguu.” Anapoambiwa husema: “Je, nisiwe ni mja mwenye kushukuru?”

´Abdullaah bin Salaam (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Enyi watu, enezeni salamu, lisheni chakula, waungeni ndugu na swalini usiku wakati watu wamelala hivyo mtaingia Peponi kwa amani.”[1]

Ameipokea at-Tirmidhiy na akasema:

“Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah bora baada ya faradhi ni swalah ya usiku.”

Swalah ya usiku inajumuisha swalah zote za kujitolea na Witr. Mtu ataswali Rak´ah mbilimbili. Atapochelea alfajiri basi ataswali Witr ambapo atawitirisha yale aliyoswali. Akitaka pia ataswali kwa namna tuliyotaja katika kikao cha nne[2].

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea katika “as-Swahiyh” zao kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mola wetu (Tabaarak wa Ta´ala) hushuka kila usiku katika mbingu ya chini ya dunia pale kunapobaki theluthi ya mwisho ya usiku na anasema mpaka kuingie alfajiri: “Nani anayeniomba Nimuitikie? Ni nani anayeniuliza Nimpe? Ni nani anayenitaka msamaha Nimsamehe?”

[1] Ameipokea Imaam Ahmad pia na kuna nyingine inayoitia nguvu na kuifanya kupanda katika ngazi ya kuwa Swahiyh.

[2] Tazama https://firqatunnajia.com/19-namna-mbalimbali-ya-kuswali-swalah-ya-witr/

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 228-229
  • Imechapishwa: 02/04/2024